The House of Favourite Newspapers

Mamilioni Yamwagwa Yanga

 BAADA ya Yanga kung’olewa rasmi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, neema ya fedha imewawakia baada ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kuwalipa fedha zilizokuwa zimesalia kutokana na ushiriki wao katika Hatua ya Makundi.

 

Yanga ilishiriki katika hatua hiyo na kushika nafasi ya nne kwenye Kundi D ambapo mchezo wao wa mwisho walifungwa bao 1-0 dhidi ya Rayon Sports nchini Rwanda. Baada ya kuingia katika hatua hiyo, Yanga ilitakiwa kupewa mgao wa shilingi milioni 600 kutokana na kushika nafasi ya nne lakini kama ingeshika nafasi za juu zaidi ingepata zaidi ya fedha hizo.

 

Taarifa za awali zilieleza kuwa walilipwa nusu ya kiwango walichotakiwa kupata ambacho ni zaidi ya Sh milioni 150 na baadaye ikaelezwa kuwa watatumiwa fedha nyingine kimafungu.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Omari Kaya alisema kuwa ni kweli timu zote zilizokuwa zikishiriki katika makundi hayo zilitarajiwa kulipwa baada ya hatua ya kwanza ya makundi kumalizika, lakini anashangazwa na kiasi ambacho kimeandikwa kwenye mitandao kuwa wao ndicho wamelipwa.

“Kwa yeyote anayefuatilia vizuri utaratibu wa Caf atakuwa anafahamu kuwa siku zote fedha zitokanazo na michuano hiyo huwa zinalipwa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza huwa ni baada ya michezo ya kwanza tu kuanza, lakini awamu inayofuata inalipwa baada ya hatua ya makundi hayo kumalizika na kwenda awamu ya pili.

 

“Sijui hizo figa za kwamba Yanga imelipwa milioni 150 watu wamezitoa wapi maana katika mazungumzo yangu kwenye runinga hakuna sehemu nilipotaja kiasi zaidi ya kusema ni kweli tunatarajia kulipwa baada ya kuondolewa katika hatua hiyo nba tayari tumeshalipwa.

 

“Hakuna ubishi kuwa Caf wamekuwa wakilipa fedha hizo katika kila hatua na kwamba huwa zinaongezeka kutokana na hatua ambayo timu husika inamaliza hasa katika nafasi za juu kama ilivyo sasa kwa timu tulizokuwa nazo kundi moja. “Maneno ya mtandaoni kwa mtu asiyejua vizuri utaratibu wa malipo hayo ya Caf yanaweza kuivuruga klabu kama shabiki akielewa vibaya kwani, kwa kiwango ambacho nimeona kimeandikwa mtandaoni ni dhahiri kabisa kuwa kuna watu wanapotosha kwa lengo la kutuvuruga.

 

“Ninachoweza kukisema hapa ni kwamba, mimi kama katibu hakuna sehemu hata moja ambayo nimetaja kiasi kilichoingia kwa maana sihusiki na mambo ya akaunti ya timu ila ukweli ni kwamba ilikuwa lazima tulipwe baada ya kumalizika kwa hatua tuliyokuwa tukishiriki,” alisema Kaya. Yanga ilikuwa kundi moja na USM Alger (Algeria), Gor Mahia (Kenya) na Rayon Sports (Rwanda), zilizosonga mbele ni Rayon Sports na USM Alger.

Yanga inaweza kutumia kiasi hicho cha fedha kilichoingia kulipa mishahara kwa wachezaji na watendaji ambao wamekuwa wakidai malipo yao hayo mara kwa mara, kulipia kambi na safari mbalimbali katika msimu huu wa 2018/19. Kingine ni kuwa wiki mbili zilizopita iliripotiwa kuwa Yusuf Manji amerejea klabuni hapo na alisaini barua akiwa mwenyekiti wa Yanga ya kumpa pole Rais John Magufuli kutokana na kupata msiba.

 

Kitendo hicho cha kusaini barua kiliwaaminisha wanachama wa Yanga kuwa kiongozi wao huyo amerejea na maisha yanaweza kuwa mazuri, kwani tangu alipoandika barua ya kujiuzulu hali ya kiuchumi iliyumba klabuni hapo.

Comments are closed.