The House of Favourite Newspapers

MWENDAWAZIMU ALIYEFUFUKA – SEHEMU YA 1

GIZA nene na mvua kubwa iliyoambatana na upepo, haikumzuia wala kumpa rapsha kiumbe mmoja, mwanadamu, aliyekuwa amelala kifudifudi, ametulia tuli kwenye tawi la mti mkubwa ulio katikati ya miti mingi ndani ya msitu wa Goma nchini Kongo.

 

Kifuani mwa kiumbe huyo alikuwa amekumbatia bunduki aina ya ‘sniper rifle SVU’ ya masafa marefu. Jicho lake moja alikuwa amelifumba wakati jingine likichungulia kwa makini katika darubini yenye nguvu ya kuona mbali iliyokuwa katika bunduki hiyo kutoka nchi ya Urusi.

 

Mwanaume huyo wa miraba minne, alijituliza kwenye mtutu wa bunduki yake pasina kutikisika wala kupepesa kope la jicho lake. Kidole chake cha mkono wa kuume kilishika kifyatulio cha risasi, kidole hicho kikiwa tayari kufyatua muda wowote pale kitakapo agizwa kufanya hivyo.

 

Ingawa kulikuwa na giza nene na mvua kubwa ya upepo, hata hivyo kiona mbali cha bunduki ya ‘rifle SVU’ kiliweza kumwonesha mmiliki wake picha nzuri ya kung’aa, mahali popote alipotaka.

Jamaa huyo, alikuwa amevaa mavazi ya kiraia. Alikuwa kwenye shati kubwa jeusi na jinsi ya kaki iliyotapakaa tope, miguuni mwa kiumbe huyo alivaa viatu, ‘katambunga’ za Kimasai.

 

Alikuwa ni mpiganaji, askari wa msituni, Muasi, mwenye shani ya udunguaji. Apiganaye dhidi ya serikali yake, serikali aliyoamini imewasaliti wanyonge na kuwadhulumu wenye haki, waliamini keki yao ya nchi. Ilikimbizwa mlango wa nyuma na kuliwa na wajanja wachache.

 

Yeye na kundi lake (wapiganaji wenziye) walijitolea maisha yao, ikiwezekana hata kufa, lakini rais aliyekuwa madarakani ang’oke na serikali yake yote halafu wao waunde serikali yao, ambayo waliamini itakuwa ni serikali yenye siasa safi, haki na usawa kwa watu wote, masikini na matajiri. Watoto kwa wakubwa, wake kwa waume.

 

Lakini hadi kufika huko, mwanaume huyu na wenziye, waliamini ilikuwa ni lazima wajitoe kwa ajili ya kizazi chao. Ndio! Pamoja na wasiwasi juu ya mauti aliyonayo binadamu, lakini kwa mwanaume huyu, hawakuona njia nyingine ya kuikomboa jamii yao zaidi ya kuziweka rehani roho zao.

Akiwa pale katika tawi la mti, mdunguaji huyo alikuwa akiwaza kwamba:

 

Hatua za kulifikia kaburi lake zipo karibu mno, nukta yoyote anaweza kuwa maiti na mwili wake kuliwa na fisi kama inavyotokea kwa wenziye waliokwisha kufa.

Walikuwa wakiuawa kila siku dhidi ya Majeshi ya Serikali na yale ya Umoja wa Mataifa. Jeshi lao lilikuwa likipungua kwa kasi, hata hivyo, fikra za kurudi nyuma hazikuwepo kichwani mwao, walikuwa tayari kupambana hadi tone la mwisho la damu.

 

Sababu za kupigana zilikuwa ni nzito na zenye maana kubwa nafsini mwao. Aliamini akifa kwa ajili ya kizazi chake ni kifo cha heshima kuliko kufa kwa Malaria kitandani.

Kufa akiwa anapigania maslahi ya taifa lake ilikuwa ni jambo alilolipa nafasi kubwa kuliko uhai wake. Alifundishwa somo hilo tangu akiwa mdogo na somo likamwingia.

 

Uzalendo ulikuwa umetamalaki kifuani mwake, chuki dhidi ya wanajeshi wateteao serikali ya rais aliye madarakani kwa kivuli cha ‘walinda amani’ ilimuudhi mno moyoni.

Aliapa kumuua yeyote atakayeonekana kwenye ardhi ya Kongo akijitia kulinda amani.

“Nitaua” alinong’ona kimoyomoyo.

Matone ya mvua yalikuwa yakidondoka kwa nguvu na kujipigiza ardhini. Muanguko wa matone hayo alikuwa ameyaweka akilini kadiri mvua ilivyokuwa ikinyesha.

Katikati ya utulivu aliojitengenezea, ghafla aligutuka baada ya kusikia utofauti wa muanguko wa matone ya mvua. Akatega sikio na kujipa utulivu zaidi.

 

Naam! Akaisikia chakarachakara ijongeayo kwa kunyata. Mnyato huo ndio uliokuwa unaharibu mwenendo wa muanguko wa matone ya mvua chini ya mti ule.

Aliongeza umakini. Akatizama kila upande kupitia darubini iliyokuwa kwenye bunduki yake ya kijeshi. Lakini wapi! Hakufanikiwa kuona chochote. Mwanaume akachakarika. Mjongeo wa chakarachakara unatokea wapi?

Akageuza bunduki yake, upande wa nyuma. Hatimaye akafanikiwa kuona kitu. Ni mita kama mia moja, kulikuwa na kichaka kidogo kinacho tembea!.

 

“Lakini!!… lakini!!..lakini!!.. ni mbali, minyato hii iko karibu” Jamaa alinong’ona. Uso wake ulikuwa umesawijika kwa mashaka na wasiwasi.

Ni kweli. Umbali mdogo kulikuwa na kichaka kinachotembea. Yamkini alikuwa ni moja ya maadui zao, ambao wamekuwa wakiwindana kwenye misitu hiyo kila siku.

Hata hivyo, adui huyo alikuwa mbali. Minyato yake isingeweza kusikika kutokea pale alipo. Mtu aliyekuwa akimnyatia hakuwa mbali naye, alikuwa jirani mno. Huyu ni hatari zaidi. Yuko wapi?

Akahaha huku na kule kuangalia kupitia bunduki ya rifle SVU. Lakini wapi!

 

Sauti moja kichwani ikamwambia: Tizama chini ya mti huu. Akatupa jicho kule chini.

Lahaulaaa!! Hakuamini alichokiona.

Kulikuwa na mwanamke, ama binti mmoja aliyekuwa amebana nyuma ya mti huku akijisuka kujibanza kwenye mti huo. Alionekana ni kama anayekimbia maadui fulani. Uso wake ulijawa na hofu.

Mdunguaji wa juu ya mti, akiwa katika taharuki ya kuangalia kioja hicho chini ya mti aliokuwa amebana juu yake. Nukta ile ile, mara kitu kigumu kilichimba sentimita chache kutoka kichwani mwake na kuparaza gome la mti ule.

 

“Nimeonekana… Nashambuliwa!!!!” alibweka kama jibwa koko, lakini sauti ilimezwa na sauti ya matone ya mvua iliyoongeza kasi ya kunyesha.

Kwa wepesi, akajirusha kwenye tawi jingine. Almanusra aanguke kwa utelezi, lakini kwa umakini aliokuwa nao, akawa ameng’ang’ania tawi hilo kama nyani. Bunduki yake ya sniper rifle SVU ikining’inia kifuani kwake.

 

Harakaharaka akailaza mbele ya tawi lile tayari ili kuangalia anashambuliwa kutokea upande upi ili ajibu mashambulizi. Ila kabla hajafanikiwa mara akasikia yowe la uchungu likitoka kwa mtu aliyemwona chini ya mti ule.

“She was attacked!!!!..” alibweka tena kwa sauti akishuhudia yule mrembo akigaa gaa chini kwa maumivu huku damu ikimchuruzika.

Akaona kuendelea kupoteza sekunde za kumwangalia binti yule ni kupoteza muda dhidi ya adui. Akarudisha umakini kwenye bunduki yake. Hata hivyo alikwishachelewa. Alichelewa muda mrefu sana!!!!!!!

Je, nini kitaendelea? Usikose tena Jumatano kwenye Risasi Mchanganyiko.

 

ALLY KATALAMBULA | +255 687 750295

Comments are closed.