The House of Favourite Newspapers

Wanaposema tujiandae kupinga matokeo wao watakuwa wapi?

0

SIASA ndiyo habari inayotawala kwa sasa hapa nchini, ambapo Watanzania waliokuwa wakihofiwa kugawanywa kwa sababu mbili yaani udini na ukabila imeongezeka sababu ya tatu ambayo inaweza kuvuruga kabisa jitihada za amani ya nchi yetu ni uchama.

Wanasiasa wengi wamesahau kuweka mbele masilahi ya Tanzania na badala yake wametanguliza zaidi itikadi za vyama.

Watanzania wa sasa wamegawanywa katika vyama vya siasa ambapo mtu aliyekuwa na uhuru wa kushabikia chama fulani pengine kwa kumnadi mgombea wake hadharani, amegeuka adui wa wanachama wa chama kingine, ambapo mara kadhaa imeripotiwa watu kupigwa hadharani kisa wamevaa nguo za chama fulani au wengine kuzomewa.

Hali hiyo imesababisha hofu kwa watu ambao mwanzoni walifikiria demokrasia itawapa uhuru wa kufanya chochote wanachokitaka bila kuvunja sheria za nchi hususan kushabikia chama wanachokipenda na badala yake hiyo imekuwa kinyume chake na kuwafanya watu wanaoshabikia chama f’lani kuwa wahanga wa kisiasa kwa kuhatarisha maisha na mali zao.

Pengine hali hiyo inaweza ikawa si tatizo sana kitaifa lakini pale ambapo viongozi wa vyama husika wanapotoa kauli za kuchochea uhalifu huo ndipo ninapoona tatizo.

Nafahamu kuwa Watanzania wamekumbwa na upepo wa kisiasa ambao haukuwahi kuvuma hapo kabla, suala la mchuano mkali kati ya chama tawala na upinzani umejidhihirisha wazi na kuteka hisia za Watanzania ambao wengi wapo tayari kushiriki uchaguzi huu kwa kuwapigia kura wagombea wanaowataka.

Ukitazama kwa jicho la tatu utagundua kuwa Watanzania hao, wengi wao walikuwa hawajajiandaa na upepo huo ambapo wengine wamejikuta wakisombwa na kushiriki demokrasia hii ya vyama vingi pasipo kuwa na utashi wa dhati wa kutaka kuleta mabadiliko ya kweli zaidi ya wao kuwa na mihemko.

Tukatae katukatu kauli zinazoweza kuwatenga iwe kwa sababu ya ukabila, udini na hata hili jipya la uchama, ukabila na udini siku zote tumekuwa tukiupinga na hili la uchama tulipinge vikali.Kwa sasa Watanzania wameanza kutenganishwa na wanasiasa wasio wema kwa sababu mpya ambayo ni kigezo cha itikadi yake ya  chama, kimsingi wanasiasa wamekuwa siyo waoga tena, kusimama katika majukwaa ya mikutano yao na kuingizia maneno yanayochochea uvunjifu wa amani.

Ni dhahiri kuna baadhi ya wanachama wa vyama vya siasa wamepanga matokeo yao kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu. Ndiyo maana wanajaribu kuwashawishi Watanzania wajiandae kupinga matokeo ya uchaguzi kama hayatakuwa yale wao waliyopanga akilini mwao.

Kwa mantiki hiyo si sahihi, hiyo ni sawa na kuuliza swali la mbili mara mbili ukijibiwa kuwa ni nne unakataa, kwa sababu tu tayari akilini mwako ulishapanga jibu lako lazima liwe lile ulilolipanga na si vinginevyo.

Wanapotushawishi kupinga matokeo ya uchaguzi yatakayotangwaza kisheria na tume halali kwa mujibu wa katiba yetu, wanakuwa wamekusudia nini? Na wakati wanatutaka tupinge matokeo hayo wao watakuwa wapi? Mimi na wewe maisha yetu ni duni, ndege hatujawahi kupanda ila wanaotushawishi wana uwezo wa kwenda nje ya nchi kama wanavyokwenda Kariakoo. Amka!

Rai yangu kwa Watanzania wenzangu, shime tushikamane na tukatae maneno yenye nia ya uchochezi ndani yake katika uchagzui mkuu na hata baada ya kutangazwa kwa mshindi. Ni lazima tukubaliane na matokeo ya uchaguzi ujao kwa kujua katika ushindani kuna kushinda na kushindwa, hivyo ni lazima tujitambue la sivyo tutakuwa tunakosea sana kama tukishindwa tunakataa.

Kila chama kimejipanga katika kushindana lakini mwisho wa siku mshindi lazima awe mmoja kati ya vyama vyote hivyo.

Leave A Reply