The House of Favourite Newspapers

Kujiamini kupita kiasi ni tatizo

0

KILA kitu kinapaswa kuwa na kiasi hata vitabu vitakatifu vinatutaka kuwa hivyo, kujiamini ni jambo zuri sana katika maisha ya mwanadamu lakini kujiamini kwa kupitiliza au kufanya kitu chochote kwa kupitiliza si vizuri na matokeao yake huwa ni kinyume kwa maana ya kukosea kile ulichopanga kukifanya.

Katika maisha ya kujifunza ni vizuri kujifunza kila siku bila kuchoka au kujiamini kuwa jambo fulani unaliweza na kulielewa kwa kiasi kikubwa kiasi cha kutotaka kujifunza zaidi kuhusu jambo hilo au mada ya somo husika.

Wanafunzi wengi wamejikuta wakiingia katika mkumbo wa kujiamini kupita kiasi lakini wamejikuta mara kadhaa wakishindwa kufaulu vizuri mitihani yao kwa kuwa walijitathmini vibaya kwa kujiona kwamba wanafahamu somo fulani kumbe ndivyo sivyo.

Nitakupa mfano mmoja ulio hai, mtu aliyesoma masomo ya uhasibu miaka ya 80 ni tofauti na yule aliyesoma miaka ya 2000 kwani, nyenzo na maarifa yameongezeka zaidi kuliko miaka ya nyuma, kwa miaka ile mhasibu alikuwa akitumia zaidi kalamu, karatasi na maarifa yake, lakini kwa kizazi hiki matumizi makubwa ni ya kimtandao zaidi kwa maana nyingine mhasibu wa zamani akitaka kwenda na wakati tulio nao inampasa arudi tena darasani japo kwa muda mchache ili aweze kusoma masomo ya kompyuta ili kuwa sawa na ulimwengu wa dot Com

Hivyo basi ni vema mwanafunzi akatambua kuwa njia pekee ya kujitathmini na kujiamini ni kupitia mitihani yake tu na si kitu kingine kwa kuwa wapo wengine waliojiamini kuwa wanaweza jambo fulani lakini wakiwa kwenye mitihani wanajikuta wamesahau kabisa kuhusu mada fulani japo kuwa walikuwa wakilifahamu vizuri somo hilo.

Jenga kujiamini lakini pia tengeneza utaratibu wa kuhakikisha kila baada ya muda fulani unapitia kile ulichojifunza ili kujikumbushia, kwa kufanya hivyo utakuwa ni mwanafunzi bora na mwenye uelewa zaidi kwani unavyozidi kujikumbusha ndivyo kitu kile kinazidi kukaa akilini, wakati mwingine kinakuongezea pia upeo wa kufikiria zaidi.

usichoke kujifunza na kujikumbusha kila unapohitaji kufanya hivyo, tukutane wiki ijayo kwenye mada nyingine.

Leave A Reply