The House of Favourite Newspapers

Miaka Minne Ndani ya Mapango ya Amboni – 32

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Nikaona msemaji huyo alikuwa amepoteza mada yetu. Nikawarudisha katika mada.

 “Sasa kwenu ni wapi?” nikamuuliza yule mtu aliyekuwa akijieleza.

 “Kwetu ni Barabara ya Tisa mkabala na Msikiti wa Ijumaa.” 

Yule mtu naye alitupa anuani yake.

 SASA ENDELEA…

Baada ya kumsikiliza yeye tulimsikiliza mtu mwingine wa tatu ambaye alisema alikuwa ametoka Arusha.

“Nilikuja kumsalimia dada yangu anayeishi hapa Tanga. Na ndipo nilipokuja kutembelea haya mapango ya Amboni. Kumbe balaa lilikuwa linatusubiri,” alituambia.

“Dada yako anaishi wapi?” nikamuuliza.

“Anaishi eneo la Nguvumali.”

Tukakubaliana kwamba kama tutapona sote itakuwa sawa lakini kama mmoja wetu atauawa, watakaobaki watatoa taarifa zake polisi.

“Hata kama atasalimika mmoja atatoa taarifa za wenzake,” nikawaambia wenzangu.

“Tulifanya kosa hatukuchukua anuani za wenzetu waliouawa,” mwenzetu mmoja akasema.

“Tulijisahau na pia hatukujua kuwa vifo vingeendelea lakini kwa sasa inabidi tuchukue tahadhari,” nikamwambia.

Tukaendelea kupumzika katika ile sehemu huku kila wakati tukitupa macho yetu kuangalia kule tulikotokea. Ilikuwa ni kwa sababu ya hofu kwamba Kaikush angeweza kutufuata kule kule.

Tulikuwa tumepumzika kwa takriban saa mbili, tukaamua tuendelee na safari.

Tuliinuka tukaanza tena kuchapa mwendo. Tulitembea mwendo mrefu tukitarajia kutokea pale mahali ambapo palikuwa na njia mbili, moja ikiwa upande wa kulia na nyingine upande wa kushoto.

Tulikuwa na imani kwamba kama tutashika njia ya upande wa kushoto ingeweza kutupeleka mahali ambapo tungekuta mlango wa pango hilo.

Lakini licha ya kutembea mwendo mrefu hatukuweza kutokea tena mahali pale tulipokuwa tunapataka.

Tulishindwa kuelewa kama njia ile tuliyokuwa tunaipita haikuwa ile tuliyoipita mwanzo ambayo ilitokea katika ile sehemu yenye njia mbili.

Tulipoanza mwendo wetu tulikuwa tukitembea kwa kasi lakini taratibu kasi yetu ilipungua. Mtu moja kati ya wale wenzangu wawili alikuwa akiweweseka muda wote.

Kuweweseka kwake kulikuwa ni kwa kuropoka maneno yaliyohusu habari zake binafsi.

Alikuwa akieleza kwamba alikuwa na mchumba wake aliyeitwa Ashura ambaye mpaka anakuja Tanga alikuwa amebakisha wiki mbili tu wafunge ndoa.

Alisema alikuwa anajuta kuja Tanga kwani kama asingekuja, yale yaliyomkuta yasingemtokea.

“Mimi najua kuwa sitapona tena humu, nitakufa tu. Buriani mchumba wangu. Hutaniona tena,” alikuwa akijisemea peke yake.

Akaendelea kusema. “Sijui ni kitu gani kilichoniponza mpaka nikaja Tanga.”

Mimi na mwenzangu tulikuwa tukimtazama na kumsikiliza. Kikubwa alicholalamikia ni kumkosa mchumba wake ambaye alikuwa afunge naye ndoa baada ya wiki mbili.

Wakati yeye akimkumbuka Ashura, mimi nilimkumbuka mke wangu ambaye tulikuwa na mwaka mmoja tangu tuoane.

Nilikuwa nimemuacha London na alikuwa mja mzito wa miezi sita. Nilijiambia kama nitakufa mle mapangoni, mke wangu atasumbuka sana kwani alikuwa akinitegemea mimi kwa kila kitu.

London si kwao, familia yake ilikuwa Zanzibar. Watu wa karibu yake huko London walikuwa ni marafiki na majirani tu. Hatukuwa na ndugu yeyote.

Mbali ya usumbufu atakaoupata, niliendelea kujiambia, atajifungua mtoto asiye na baba wa kumtunza na kumpa elimu bora kinyume na matazamio yangu kwamba mtoto wangu atakayezaliwa nitampa elimu bora.

Sikujua yule mwenzetu wa tatu aliyekuwa kimya alikuwa akiwaza nini. Bila shaka na yeye alikuwa na lake alilokuwa anawaza. Kwa vile alikuwa amejikaza kiume hakupenda kudhihirisha mawazo yake.

Ghafla tulijikuta tumetokea mahali ambapo hewa ilibadilika na kuwa nzito. Hata kupumua kwetu kulikuwa ni kwa shida.

“Jamani huku tunakokwenda naona hakuna usalama,” nikawaambia wenzangu.

“Naona hewa imebadilika ghafla,” yule mwenzetu aliyekuwa akiweweseka akasema.

“Ni kweli, hewa imekuwa nzito,” mwenzetu wa tatu akamalizia.

Tukasimama.

“Tusiendelee kwenda, tutakosa hewa kabisa,” nikawaambia wenzangu.

“Mimi pia naona hivyo , tunaweza kufa,”  yulealiyekuwa akimkumbuka mchumba wake akasema.

“Basi turudini nyuma,” nikawambia.

Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye gazeti hilihili Jumanne ijayo.

Leave A Reply