The House of Favourite Newspapers

Rich Mavoko na mkorogo wapi na wapi?

0

mavoko

BONGO Fleva inazidi kupaa na kupata hadhi ya kuwa ndiyo muziki wa Afrika Mashariki katika nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).

Kutoka enzi za Kwanza Unit hadi uzao wa akina Ruby, ni safari ndefu iliyozalisha wasanii wengi waliofanya vizuri na kutoa mchango wao katika kiwango cha kuridhisha. Na kati yao, ni kijana Rich Movoko ambaye kwa mashabiki wa muziki huu, ni jina kubwa lenye hadhi.

Ni kizazi cha Bongo Fleva kilichoibuka ‘enzi’ moja na akina Diamond Platnumz, yapata miaka saba au nane iliyopita. Sijawahi kuwa karibu na huyu dogo, lakini nikiri kuwa kazi zake nazisikia na zinafanya vizuri, hasa kibao chake cha hivi karibuni zaidi kiitwacho Pacha Wangu.

Kama utataka kuwaweka katika chati, utakutana na Rich Mavoko katika nafasi za juu akishindana na kina Ali Kiba, Diamond, Barnaba, Madee na wenzake wa namna hiyo. Ni mzuri na kwa kweli ana heshima yake katika muziki huu.

Lakini kuna jambo moja limekuwa likinitatiza kidogo kumhusu, hasa katika maisha yake binafsi. Labda kabla sijaenda mbali, niwakumbushe mastaa kuwa ukishakuwa mtu maarufu, suala la ‘privesi’ linaondoka. Ni vigumu kumkuta Mavoko anakula wali maharage kwa mama ntilie, ule wa buku jero, halafu useme hilo ni jambo binafsi!
Hiyo itakuwa ni habari kubwa, ingawa kuna watu wana hela kuliko yeye wanakula hapo, lakini kwa kuwa hawajulikani, hakuna anayejali.

Rich Mavoko inadaiwa anatumia mkorogo. Wakati anaibuka, hata yeye anajua kuwa alikuwa mweusi, lakini ukionana naye hivi sasa, ni mweupe. Wakati f’lani aliwahi kuwajibu wanaomsema kuhusu mkorogo, akisema kuwa hatumii madawa, isipokuwa labda tu kwa vile hali yake kimaisha ni nzuri, ndiyo maana na ngozi nayo inakuwa safi!
Utetezi dhaifu kabisa.

Kwamba kwa kuwa mambo yake yako vizuri, basi na ngozi nayo inabadilika rangi? Big no! Hakuna uhusiano kati ya fedha na rangi ya ngozi bila kujichubua. Alifanya hivyo Michael Jackson na dunia yote inajua, jinsi alivyoichukia ngozi yake nyeusi.

Kama suala ni hela, pale katika Ligi Kuu England kuna Mbrazil anaitwa Ramires, anakipiga Chelsea. Ana hela na kule anaishi sehemu wanazoishi wenye nazo, lakini kama utamchukua na kumtupa pale shimoni, sokoni Kariakoo na ukaambiwa jamaa anatokea Masasi, hakuna atakayehoji.

Mavoko anadaiwa kutumia cosmetics kali kama siyo mkorogo kujichubua. Naweza kusema hayo ni maisha yake binafsi, lakini kama nilivyosema, ukiwa staa, lolote litafuatiliwa. Kuna watoto wetu wanaangalia televisheni, walimuona akiwa mweusi, ghafla leo kawa ‘white’, watajiuliza na wakisikia kuna mchanganyiko wa madawa yanabadili rangi ya ngozi, wanaweza kushawishika.

Nimshauri mdogo wangu Rich Mavoko, kuwa international siyo kubadili rangi ya ngozi yako, ufanane na Mzungu. Fanya kazi nzuri na tengeneza menejimenti ya uhakika, utakuwa msanii wa kimataifa.

AY amefanya muziki kabla yake, amekuwa international kabla yake na ameshafanya kolabo kibao na mastaa wa Marekani, lakini kila siku rangi yake ya ngozi ni ileile, tena inazidi kuiva kiuweusi.

Madoido ya wasanii, hasa wa Bongo ni jambo la kawaida, lakini yasifikie wakati watu wakakuona limbukeni au uliyeathiriwa na ustaa. Tunao mastaa, ambao walidhani wao ni wajanja, wakaiga ujinga, leo ulimwengu unawacheka, wamepoteza hata kile kidogo walichokuwa nacho.

Mavoko bado kijana, kama kweli unatumia mkorogo kama inavyodaiwa achana nao, mashabiki wanataka kazi bomba na wala hawana haja na muonekano wako!

Leave A Reply