The House of Favourite Newspapers

Joto la Mapenzi – 43

0

ILIPOISHIA…
Ambe aliwaeleza angefika pale saa mbili usiku baada ya kukatazwa na Mabina kwa kuamini hata kama kuna kitu kitakwenda tofauti wangeweza kukabiliana nacho hata kukimbilia tofauti na mchana.
Mzee Mtoe wasiwasi ulimjaa kutokana na kuona muda unakatika bila kuonekana Ambe, kujifanya ana hamu na mkwewe alimfuata Koleta kupata uhakika.
“Vipi mwenzio atakuja?”
ENDELEA NAYO…

“Ndiyo baba.”
“Mbona muda unakatika au anakuja usiku wa manane?”
“Baba mbona saa mbili haijafika?”
“Kwa hiyo una uhakika anakuja?”
“Kama kungekuwa na tatizo wangenijulisha lakini atakuja.”
“Sawa basi mi’ natoka kidogo nitarudi kabla ya muda huo.”
“Baba usiende mbali basi.”
“Sipo mbali sijui hata robo saa itatimia nitakuwa nimerudi.”
“Sawa baba.”
Mzee Mtoe baada ya kupata uhakika alimpigia simu mkuu wa polisi awasogeze vijana wake karibu na nyumba yake.
“Mkuu wasogeze vijana wako karibu wataingia muda si mrefu.”
“Usiwe na wasiwasi wapo hapo tangu asubuhi kila kitu kipo sawa usihofu lazima wakamatwe.”
“Sawa mkuu, basi mimi narudi kujifanya nawasubiri wageni.”
Baada ya kupanga mipango yake na kuwa na uhakika nyumba yake imezungukwa na askari waliokuwa wapo tayari kumtia Ambe na Mabina mikononi.
Majira ya saa mbili kamili Ambe alifika nyumbani kwa mzee Mtoe akiwa peke yake bila rafiki yake Mabina. Koleta alifurahi kumuona mpenzi wake nyumbani kwao.
“Karibu sana mpenzi wangu.”
“Asante.”
“Karibu baba,” mzee Mtoe alikwenda kumkumbatia kuonesha hana kinyongo.
“Asante baba, shikamoo.”
“Marahaba mwanangu.”
“Shikamoo mama.”
“Marahaba mwanangu karibu sana.”
“Asante sana mama nimekaribia.”
“Shikamoo baba,” Junior alimsogelea baba yake na kumkumbatia. Koleta aliangalia kwa furaha jinsi familia yake ilivyompokea Ambe bila kujua kuna mpango mzito uliofanywa na baba yake.
“Vipi shemeji yupo wapi?”
“Amepata dharura.”
“Kwa hiyo hatakuja?”
“Hawezi.”
“Jamani ningefurahi siku tukufu kama hii angekuwepo na yeye.”
“Siku nyingine.”
“Jamani mpenzi siku ya leo kwangu ni muhimu kuliko kitu chochote.”
“Ni kweli lakini wa muhimu ni mimi kuliko yeye hata akikosekana hakitaharibika kitu.”
“Sina maana hiyo wewe ni zaidi ya kila kitu.”
“Usiwe na wasiwasi, baada ya hapa tuna kazi ndefu sana, kwanza isingekuwa vizuri wazazi kuniomba radhi mbele yake.”
“Lakini kweli mpenzi wangu kumbe ulifanya hivyo kwa makusudi.”
Mabina alimkatalia Ambe kuongozana baada ya machale kumcheza kwa kuogopa kujiingiza kwenye mdomo wa mamba wakati wanamuona amefumbua mdomo.
“Ambe we tangulia nitakavyokuja huwezi jua kuna kitu gani tusichokijua nimekuwa na maisha ya kigaidi toka nilipoishi kwa mara ya pili. Elewa ule unaweza kuwa mtego. Naweza nisionekane mpaka utakapotoka salama.”
“Kwa hiyo utaniacha peke yangu?”
“Nipo wa wewe mpaka tone la mwisho nimekueleza akifanya ujanja wowote sitasita kumpoteza mkweo.”
“We akifanya ujanja wowote fanya uwezavyo,” Ambe alimpa ruhusa Mabina kufanya lolote.
“Poa nakutakia safari njema.”
Waliagana kwa Ambe kwenda peke yake na Mabina kubakia mjini, japo Ambe hakuamini sana kama wazazi wa Koleta wanaweza kumgeuka lakini moyoni alijawa na wasiwasi wa kulipukiwa bomu peke yake.
Moyoni alijiapiza kabla ya kukamatwa atahakikisha anamuua Koleta na mzee Mtoe ili akanyongwe.Kabla ya kuingia kwenye gari kuelekea ukweni aliitazama bastola yake kiunoni iliyokuwa imetulia.
Baada ya kuwa na uhakika na silaha yake alipanda gari moja kwa moja hadi nyumbani kwao na Koleta na kupokelewa kwa furaha na bashasha toka kwa wazazi wote kitu kilichompa uhakika kuwa uhasama umekwisha. Akiwa bado anazungumza na mpenzi wake mzee Mtoe aliuliza:
“Si nimesikia unakuja na rafiki yako vipi mmefikia wapi?”“Amepata dharura.”
“Kwa hiyo?”
“Kuhusu nini tena baba?”
“Kwa hiyo haji tena?”
”Ndiyo.”
“Ooh! Umevuruga kila kitu.”
“Kivipi baba ikiwa mtu wa muhimu ni mimi?”
“Ooh! Siyo mbaya, basi endelea na mazungumzo na mwenzako nipo ndani mara moja jisikie upo kwenu.”
“Nashukuru mzazi wangu.”Mzee Mtoe alikwenda hadi chumbani kwake na kumjulisha mkuu wa polisi kuwa mtuhumiwa amefika.”
“Mheshimiwa mtuhumiwa amefika.”
“Tumemuona mbona yupo peke yake?”
“Amesema mwenzake amepata dharura.”
“Kwa hiyo tufanyaje?”
“Kwa nini tusimuache aondoke ili tuweze kumkamata na mwenzake.”
“Hapana hatuwezi kumuacha huyohuyo atatuonesha mwenzake yupo wapi ikiwezekana usiku huu tukimpa kibano atatupeleka alipomuacha mwenzake.”
“Basi hakuna tatizo sasa tutafanyaje kumkamata.”
“Usiwe na haraka ianzeni sherehe na onesha uchangamfu mkubwa ili asijue nini kinaendelea.”
Mama Koleta aliyekuwa akiingia ndani alishtuka mazungumzo ya mumewe na kumfanya anyate na kuweza kusikia ubaya wa mumewe kutaka kumkamatisha mpenzi wa mtoto wao.
Alijikuta akishika mdomo huku mapigo ya moyo yakimwenda mbio akikumbuka kauli ya mwanaye kama baba yake akimgeuka lazima damu ingemwagika.
Alitamani kumweleza mumewe asifanye vile lakini aliamini kabisa kama askari wamezunguka nyumba asingeweza kumsikiliza.
Alitoka haraka hadi sebuleni na kuwakuta mwanaye Koleta na mpenzi wake pamoja na mtoto wao walikuwa katika mazungumzo ya furaha.
Roho ilimuuma sana kuona dakika chache hali itakuwa mbaya sana mle ndani kwa watu wengine kupoteza uhai kwa ubishi wa mumewe.
Bila kujielewa machozi yalimtoka mkono ukiwa shavuni. Koleta aliyekuwa akizungumza na Ambe katika hali ya furaha alishtushwa na hali ya mama yake kushika tama huku akiwa ameuegemea mlango wakati muda mfupi alikuwa na furaha.
Koleta alinyanyuka hadi kwa mama yake ambaye alikuwa mbali kimawazo huku machozi yakimtoka. Koleta alishtuka na kumuuliza mama yake:
“Mamaa, kuna nini?”
Mama yake badala ya kumjibu alimkumbatia na kulia kilio cha kwikwi.
“Mama kuna nini?” Koleta alizidi kuchanganywa na mama yake.“
Naomba twende chumbani kwako,” mama yake alisema kwa sauti ya kilio.
Koleta bila kuongeza neno alikwenda chumbani kwake, walipofika alitaka kujua mama yake kipi kimemsibu.
“Mama kuna nini tena, mbona unanitisha?”
“Mwanangu nakuomba usifanye lolote.”
“Kuhusu nini tena mama?”
“Baba yako mbishi.”
“Kafanya nini tena?”
“Amewaita polisi waje wamkamate mpenzi wako.”
“Mamaa!”
“Kweli kabisa nimemkuta baba yako akiita polisi waje wamkamate, sijui hata itakuwaje?”
“Mama unasema kweli?”
“Nimemsikia kwa masikio yangu akiwaeleza waje, kumbe aliwaeleza watakuwa wapo wawili na wakimshika mpenzi wako watamtesa ili amtaje mwenzake.”
“Mama sikubali, namfuata.”
Je nini kitaendelea?
Tukutane wiki ijayo.

Leave A Reply