The House of Favourite Newspapers

Diamond hongera kwa kuyamaliza na ‘mshua’, lakini isiishie studio

Mzee Abdul Juma.

MIONGONI mwa habari zinazoendelea kutrendi kwa kasi kubwa kwenye mitandao ya kijamii, ni tukio la msanii mahiri wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kumaliza tofauti kati yake na baba yake, mzee Abdul Juma.

 

Kwa kipindi kirefu, kilio cha mashabiki wa msanii huyu pamoja na wadau wengine wa masuala ya burudani, ilikuwa ni kwa Diamond kumsamehe baba yake na kumsaidia kwa sababu yupo kwenye kipindi kigumu, anasumbuliwa na matatizo ya muda mrefu ya miguu na anahitaji msaada wa matibabu.

 

Lakini si hivyo tu, Mzee Abdul kama mzazi, licha ya mapungufu ambayo yamewahi kutokea kati yake na mwanaye ambayo hata yeye mwenyewe kwa kinywa chake amekuwa akikiri, anastahili kula jasho la mwanaye kwa sababu yeye ndiye baba mzazi, bila yeye leo kusingekuwa na mtu anaitwa Diamond.

Baada ya manung’uniko ya mzee huyo kwa kipindi kirefu, hatimaye usiku wa Jumanne, mambo yalifikia tamati baada ya Diamond na baba yake kukutanishwa studio, kila mmoja akatema ‘nyongo’ na mwisho wakapatanishwa na kukubaliana kuuanza ukurasa mpya!

 

Hakuna picha inayovutia kama ile inayomuonesha Diamond na baba yake wakikumbatiana baada ya kumaliza tofauti zao! Kwa kipindi kirefu, mimi mwenyewe nimekuwa nikimtolea uvivu Diamond mara kadhaa na kumweleza umuhimu wa kumsamehe baba yake na kufungua ukurasa mpya kwa sababu mwisho wa siku, mzazi atabaki kuwa mzazi.

 

Kiungwana, mtu akifanya jambo ambalo ulikuwa ukitamani sana litokee, huna budi kumpongeza, kwa nafasi ya kipekee kabisa, NAKUPONGEZA Diamond kwa kuamua kuyamaliza na ‘mshua’ wako, maisha ndivyo yanavyotaka na hata maandiko matakatifu yanatukumbusha kwamba baba na mama ni Mungu wa pili hapa duniani.

 

Naamini hata yale magumu aliyokuwa akipitia Diamond kutokana na nafsi ya mzazi wake kusononeka, sasa yatafanywa kuwa mepesi, ile amani ya moyo ambayo wote wawili walikuwa wakiikosa kwa kipindi kirefu, sasa imepatikana na bila shaka hata malaika wa heri, walishangilia usiku ule Diamond na baba yake walipokumbatiana na kukubaliana kumaliza tofauti zao.

 

Kwa mzee Abdul, bila shaka umesikia anachokitaka mwanao, mambo ya ‘kuchoreshana’ kwenye vyombo vya habari yamekuwa yakimuumiza sana na amelieleza hilo mbele yako, ni matumaini yangu kwa kuwa wewe ni baba na una busara, utaachana nayo kwa sababu sasa ameamua kukusaidia.

 

Kwako Diamond, najua ulichokisema kumhusu baba yako ulikimaanisha na wala hukuwa na nia ya kutafuta ‘attention’ kwa watu, bali umedhamiria kweli kufungua ukurasa mpya na baba yako. Chondechonde, tekeleza ulichokiahidi, msaidie baba yako na isiwe kwamba baada ya kumalizana studio, basi biashara ikawa imeishia hapohapo.

 

Wewe pia ni baba, najua unayaelewa maumivu ya kuzuiwa au kushindwa kuwa karibu na wanao, ifanye furaha aliyoionesha ‘mshua’ wako pale studio iwe ya kudumu, maisha yenyewe mafupi haya.

 

Nawatakia kila la heri kwenye ukurasa mpya wa maisha mlioufungua, msimpe tena nafasi ‘yule mwovu’ akajiinua katikati yenu! All the best!

Za chembe Lazima Ukae NA HASHI-POWER,

Comments are closed.