The House of Favourite Newspapers

SIRI KIBAO VIBENTENI KUMWAGWA NA MASTAA ZAFICHUKA

DAR ES SALAAM: Jipu limepasuka pwaaa, aisee! Siri za vibenteni (wanaume waliozidiwa umri na wanawake wao) kumwagwa na mastaa wa kike imefichuka; Amani limedokezwa. 

 

Katika miaka ya hivi karibuni kuliibuka wimbi la wanawake wengi, hasa mastaa wenye umri mkubwa kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na vijana wadogo (vibenteni), lakini sasa mambo yamebadilika.

 

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba, kwa sasa wanawake au mastaa hao hawataki tena uhusiano wa sampuli hiyo. Mahojiano ya gazeti hili yaliyofanywa na baadhi ya wanawake hao kwa sharti la kutotajwa majina gazetini ndiyo yaliyobumburua siri nyuma ya vibenteni hao kupigwa chini.

 

SIRI YA KWANZA

Wahusika hao kwa nyakati tofauti walieleza kuwa, inahitajika kuwa na moyo wa chuma ili kuishi na kibenteni. “Ni kweli wana nguvu na miili yao imejengeka vizuri, lakini inahitaji kuwa na moyo wa chuma hasa kwa sisi ambao ni watu wazima kwa sababu akili zao hazijakomaa, wana utoto mwingi, hawajui maisha na hawawezi kulea watoto ambao tayari mtu umeshazaa na mwanaume mwingine. Kinachotokea unajikuta ukimlea yeye kama unavyolea mwanao,” alisema mmoja wa mastaa waliowahi kuwa na kibenteni kisha wakawamwaga.

 

SIRI YA PILI

Ilibainika kwamba, pamoja na kwamba vibenteni wana nguvu kwenye eneo la tendo la ndoa ukilinganisha na watu wazima, lakini baadhi wanaamini kwamba vijana wadogo hawawezi kuwapa ulinzi wa kutosha.

 

“Raha ya kuwa na mwanaume bwana lazima akuzidi umri na hata umbo, akisema hataki kitu fulani kunamamlaka fulani, lakini kwa kibenteni yeye ndiye anayehitaji ulinzi au kusimamiwa badala yeye asimamie familia,” alisema staa mwingine aliyemwagana na kibenteni wake miezi kadhaa iliyopita.

 

SIRI YA TATU

Ilibainika kwamba, mbali na kutoa dozi ya tendo la ndoa, vibenteni hawajui kumbembeleza mtu mzima hivyo mwanamke kutoliwazika vya kutosha ukilinganisha na wanapokuwa na wakubwa wenzao. “Hawajui kubembeleza badala yake wewe unajikuta ukifanya kazi ya kumbembeleza yeye, mapenzi ni kubembelezana na siyo kurukiana tu kama kuku,” alisema mwingine aliyeonekana kukinaishwa na kibenteni wake.

 

SIRI YA NNE

Kwa kuwa bado damu zao zinachemka, imeelezwa kuwa vibenteni wamekuwa wakiwapa taabu sana wanawake wao kwani mara nyingi wamejikuta wakiwalinda wasikwapuliwe na wadogo wenzao.

“Sasa unakuta badala ya ku-concentrate kutafuta maisha unaanza kukimbizana na ‘serengeti boy’ asiibiwe na wasichana wa saizi yake hadi unaona aibu. “Kuliko kujipa shida hizo zote nikaona bora kumpiga chini, nikawa na mtu mzima mwenzangu, mambo yanakweda vizuri sasa,” alisema staa maarufu wa Bongo Muvi na kuongeza:

 

SIRI YA TANO

“Unajua kuna jambo ambalo watu wengi hawalijui, lakini kuna shida nyingine kubwa linapokuja suala la heshima hasa kwenye mijumuiko maalum. “Siyo siri, ilikuwa ni ngumu sana kwenda na kibenteni wangu kwenye hafla za heshima maana watu wanakushangaa upo na mtoto sehemu ambayo kila mwanamke yupo na mumewe wa rika lake au aliyemzidi umri. Hapo ndipo nikaona bora niachane na kibenteni nitafute mtu wangu wa kwenda naye kwenye hafla za heshima.

 

SIRI YA SITA

“Jambo lingine ni kwamba kibenteni akishajua una pesa, basi hafanyi kazi badala yake anataka wewe uwe unampa pesa kila siku. Kwa kifupi anakufanya ATM, unajikuta hata kile ulichotafuta miaka yote kinatapanywa na mtu asiye na uchungu na maisha. Sasa katika hali kama hiyo ni bora uachane naye maana anakuwa kama kupe ambaye kazi yake kubwa ni kukunyonya tu damu hadi iishe.”

 

MTAALAM AFUNGUKA

Akizungumzia sababu ya tabia ya kupenda vijana wadogo kisha kuachana nao, Mtaalam wa Saikolojia ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Chris Mauki alisema kuwa, chanzo cha jambo hilo kilitokana na binadamu kupenda kufanya vitu vilivyokatazwa na kutamani kuona itakuwaje.

 

“Ilikuwa ni tamaa tu ya kibinadamu ya kutaka kuona matokeo yatakuwaje na kweli wameona siyo mazuri. “Unajua hiyo kitu ilikuwa inawaondolea heshima kutokana na kutokuwa na mipaka kati yao. Kwa mfano kama unaweza kutoka kimapenzi na kijana au mtoto uliyemzidi miaka zaidi ya kumi kwa visingizio hivi na vile, unadhani kuna nafasi ya heshima hapo?” Alihoji Dk Mauki.

 

MASTAA WALIOMWAGANA NA VIBENTENI

Baadhi ya mastaa waliomwagana na vibenteni waliokuwa nao kwenye mapenzi kwa sababu mbalimbali zikiwemo zilizotajwa hapo juu ni pamoja na mwigizaji Aunt Ezekiel ambaye hivi karibuni alimmwaga mzazi mwenzake ambaye ni dansa wa Wasafi Classic Baby (WCB), Moses Iyobo ‘Moze’ anayedaiwa kuwa na umri mdogo kuliko yeye.

 

Wengine ni mwigizaji Irene Uwoya aliyemmwaga msanii wa Bongo Fleva, Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’ aliyekuwa amemwacha nyuma karibia miaka kumi na ushee na mwigizaji Jacqueline Wolper aliyempiga chini staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ ambaye naye alikuwa amempita umri. Mwaka jana, mwanamama Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ alimmwaga staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ aliyekuwa amemzidi umri kwa zaidi ya miaka kumi.

 

Wengine waliowamwaga vibenteni ni pamoja na msanii wa Bongo Fleva, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ ambaye alimpiga chini msanii mwenzake, Naftal Mlawa ‘Nuh Mziwanda’ aliyekuwa mdogo kwake na Faidha Omary ‘Sister Fei’ ambaye alimpiga chini kibenteni wake, Hollystar. Mwigizaji Wema Isaac Sepetu alimmwaga Idris Sultan aliyekuwa amempita umri huku Wastara Juma naye akimwaga aliyekuwa kibenteni wake, Bond Bin Sinan.

 

IYOBO AFUNGUKA

Wakati hayo yakiendelea, Moze Iyobo yeye amekiri kufungasha virago vyake na kuondoka kwenye nyumba aliyokuwa akiishi na mzazi mwenzake Aunt maeneo ya Mwanyamala jijini Dar. Katika mahojiano na gazeti hili, Iyobo alifunguka kila kitu;

 

Amani: Mambo vipi Iyobo?

Iyobo: Poa, niambie…

Amani: Kuna tetesi kwamba umepanga kumfanyia Aunt kitu mbaya ambacho hatakisahau kwenye maisha yake na kitu chenyewe inasemekana una mpango wa kumdhulumu mali zake kama nyumba ya Kigamboni, kiwanja cha Bunju na gari analotembelea, hii imekaaje?

 

Iyobo: (Kwa mshangao) unajua sijui kwa nini watu wameamua kunizushia mambo yote hayo, kiukweli mimi sina mpango wa kufanya hayo mambo kabisa. Kwanza kwa nini nifanye? Na ili iweje? Hizo stori hazina ukweli wowote ule ila kuna watu wameamua tu kunichafua ili nionekane mbaya.

Amani: Unajisikiaje unapoona Aunt anamposti huyo mpenzi wake mpya kwenye akaunti yake ya Instagram?

 

Iyobo: Najisikia poa tu kwa sababu mimi na Aunt tumeshaachana na sasa hivi yeye ni mke wa mtu, kwa hiyo kwangu naona kawaida tu.

Amani: Vipi kuhusu mtoto wenu Cookie? Huoni kama atakosa malezi ya baba na mama?

Iyobo: Hapana, binti yetu bado tunamlea vizuri tu na wala hakuna tatizo lolote.

Amani: Hivi bado unaishi naye kwenye lile ghorofa au ulishahama?

 

Iyobo: Siwezi nikaendelea kuishi na mke wa mtu, nilishahama, sasa hivi ninaishi kivyangu.

Amani: Inasemekana pia tangu uingie Wasafi hadi sasa huna gari lako mwenyewe, je, ni kweli?

Iyobo: (Anacheka) watu bwana, yaani hapa ninavyoongea na wewe nipo njiani naendesha gari langu, sasa hizo habari za kwamba mimi sina gari zimetoka wapi?

 

Amani: Ni kweli kwamba una mpango wa kwenda Kenya nyumbani kwa kina Melisa (mpenzi mpya), kwa ajili ya kujitambulisha?

Iyobo: Jamani siyo kweli, wewe umeshawahi kuona nimeposti kitu kama hicho kwenye akaunti yangu? Mimi sina huo muda.

Comments are closed.