The House of Favourite Newspapers

Chuzi Ndo Hilo, Hakuna Kuonja!-18

0

ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA:

Baba Shua alipokosa meseji yoyote yenye kutia shaka, aliizima, akairudisha simu kwenye chaja kisha akatoka sebuleni. Alikaa akisikiliza maji yanavyomwagika bafuni mkewe akioga lakini hakusikia…

“Mh! Huyu amekwenda bafuni kweli au..?”

JIACHIE SASA…

Baba Shua wakati ameshtuka hivyo, mama Shua alitoka chumbani kwa Musa haraka. Akanyata mpaka uani, akazama bafuni.

Baba Shua alitoka sebuleni, aketembea, naye kwa kunyata mpaka uani. Akasimama.

Mama Shua alipozama bafuni, alianza kuoga maana alitoka uwanjani, hivyo lazima awe msafi.

Baba Shua aliposikia maji ‘chwaa’ akatingisha kichwa kwa maana ya kukubali…

“Maana usikute mtu kasema anakwenda kuoga kumbe ameingia kwa mwanaume wake,” alisema moyoni baba Shua huku akirudi sebuleni.

Musa alianza kuona njia nyepesi ya kumpata mama Shua…

“Kumbe hata kwangu hapahapa nyumbani inawezekana? Sasa kuna haja gani ya kupoteza pesa hotelini?” alijihoji Musa.

“Basi itakuwa nikimhitaji na’mbuku mapema ili ajipange jinsi ya kumpiga chenga mumewe.”

***

Mama Shua aliingia chumbani, akajifuta na kupanda kitandani huku akijifanya hana habari na mumewe.

***

Ilikuwa usiku wa saa saba, baba Shua alishtuka akiwa amelala kuangalia juu au chali. Akamwamsha mke wake …

“Mama Shua…”

“Abee,” mama Shua aliitika haraka sana. Ilionekana hata yeye hakuwa amelala usingizi…

“Hivi unajijua kwamba umebadilika nyendo zako?”

“Mimi sijabadilika, ila wewe mawazo yako yanasema hivyo.”

“Mh! Mawazo yangu yanasema hivyo…ama kweli wanawake mwalimu wenu kipofu! Hivi unadhani wewe uliyekuwa na mimi mwaka jana ndiye nakuona yuleyule wa mwaka huu?”

“Si ndiyo maana nimesema mawazo yako.”

“Mawazo yangu ee? Sawa bwana, mawazo yangu, usiku mwema,” mama Shua alilala zake.

Mama Shua hakutaka kunyoosha maneno wala kuweka sawa hali hiyo. Kwake akaona ni sawasawa tu. Alishalewa penzi la Musa.

***

Asubuhi kulikucha, mama Shua kama kawaida yake, anakuaga wa kwanza kutoka uani na binti yake, Shua na kumkuta msichana wa kazi akiwa wa kwanza kutoka kuliko yeyote ndani ya nyumba hiyo.

Baba Shua siku hiyo alichelewa kidogo, wakati mkewe ametoka kuoga, yeye ndiyo akaenda kuoga.

Musa siku hiyo alipotoka, hakukutana na mama Shua wala Shua mwenyewe, ila msichana wa kazi wa mama Shua alikuwa akifagia…

“Mchumba wangu yuko wapi?” alimuuliza msichana wa kazi…

“Kaingia ndani na mama yake.”

“A…haa! Kaamka poa lakini?”

“Eee.”

***

Musa ndiye aliyekuwa wa kwanza kufika nje, akawa anavaa viatu tayari kwa kuondoka. Mara akafuata mama Shua. Baba Shua alisimama mlangoni akisikiliza…

“Za asubuhi?” alisalimia Musa…

“Salama, mzima wewe?”

“Mimi mzima, naona kumekucha.”

“Eee…ndiyo unaondoka?” aliuliza mama Shua…

“Eee…”

“Nitapata lifti?” mama Shua aliomba lifti huku akiwa hajui kama mume wake anasikiliza…

“Itakuaje sasa? Utaeleweka?”

“Ah! Achana naye huyu.”

Baba Shua alimwomba Mungu amsaidie katika kusimamia uvumilivu wake ili asijitokeze akiamini kwamba anaweza kufanya jambo baya kuliko inavyofikiriwa…

“Eee Mungu, nipe uvumilivu kwa ushahidi huu,” alijisemea moyoni baba Shua huku macho yake yakiwa kwa Shua kitandani.

“Teh! Teh! Teh!” alicheka Musa kwa kicheko kile cha ‘da! Jamaa namwibia hivihivi anaona’.

Musa ndiye aliyeanza kutoka, mama Shua akachelewa  nje kidogo akijifanya anaweka sawa gauni lake jekundu alilovaa siku hiyo.

Baba Shua hakutoka nje, alikwenda kukaa kwenye kitanda na machozi yakaanza kumchuruzika kiasi kwamba alijuta, si kumuoa mwanamke huyo bali hata kukutana naye siku ya kwanza…

“Hivi kumbe ameumbwa hivi? Hakuna haja ya kuelimishana tena, dawa yake ni kuamua kuachana naye tu,” alisema moyoni baba Shua, akasimama, akapiga ishara ya msalaba kifuani kama kuashiria kwamba, anamuachia Mungu.

Kwa upande wake mama Shua, alishangaa kutomwona mumewe akitoka ili kumsindikiza kwa macho kama ilivyo kawaida yake…

“Huyu vipi? Mbona hatoki wakati mimi nataka kuondoka?” alijiuliza mama Shua, akarudi ndani, tena mpaka chumbani…

“Mi naondoka,” aliaga Mama Shua huku macho yake yote yakiwa kwenye simu. Aliamini Musa atamtumia meseji.

Baba Shua hakumjibu mkewe, alikaa kitandani. Alikuwa akimuangalia tu!

Ilibidi mama Shua atoke mbio kuwahi lifti huku moyoni akijua kwamba mumewe ana kitu moyoni…

“Au jana alijua niliingia chumbani kwa Musa? Lakini hapana, asigeweza kuacha kuniambia. Lakini lazima ana jambo ndani ya moyo wake.”

Mama Shua alipanda gari la Musa huku akiwa hana amani. Pia alipanda kimachale sana akiangalia nyuma. Aliamini mumewe anaweza kutokea ghafla…

Je, nini kitaendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda, siku ya Jumatatu.

Leave A Reply