The House of Favourite Newspapers

Flora Mbasha akiri: Mwanangu si wa Mbasha!

0

Mwimbaji wa nyimbo za Injili, Flora Mbasha na aliyekuwa mumewe, Emmanuel Mbasha.

Waandishi wetu

OHOOO! Kimenuka tena. Mwimbaji wa nyimbo za Injili, Flora Mbasha amesema mwanaye mdogo (jina linahifadhiwa) hahusiani hata kidogo na aliyekuwa mumewe, Emmanuel Mbasha huku akidai kuwa anamtambua mwanaume huyo kama mzazi mwenzake kwa mtoto mmoja tu (Liz), Risasi Jumatano linakupa zaidi.

Akizungumza na waandishi wetu kwa njia ya simu mwishoni mwa wiki, Flora alisema amechoshwa na manenomaneno yanayosemwa juu yake na Emmanuel na kwamba kama mumewe huyo ameamua kumwaga ugali, yeye yupo tayari kumwaga mboga.

Mwimbaji huyo alisema kwamba kauli aliyoitoa hivi karibuni kuwa anampenda mumewe na kwamba yupo tayari kuishi naye haikutoka moyoni, isipokuwa alifanya hivyo kwa huruma tu, kwa sababu mwanaume huyo ni mtu katili, mwenye roho mbaya na asiyemuogopa Mungu.

“Mtu mwenyewe alimtelekeza mtoto (Liz) kwa zaidi ya mwaka mmoja, ni mtu mbaya sana, sina mapenzi na Mbasha hata kidogo, ni afadhali niolewe na chizi anayeokota makopo kuliko kurudiana na mtu katili na mnyama kama huyo, namheshimu kama mzazi mwenzangu kwa Liz,” alisema.

Mtoto anayedaiwa kuibua mazito.

“Huyo mwanaume hafai kabisa, ni katili, namfananisha na shetani, anajifanya mwema kwa watu wakati hajawahi kuiomba msamaha familia, sikubaliani kabisa na hukumu ya mahakama, ukweli anaujua kwamba alibaka na hata mkimtaka huyo binti mumhoji nitamleta, isitoshe sasa hivi hata mtoto wake hamjali, hajui anasoma vipi, hajawahi kulipa hata shilingi ya ada, mimi mwenyewe ndo nahangaika kumlea mwanangu Liz ambaye anasoma kidato cha kwanza.

“Hastahili kabisa kuitwa baba sababu mzazi mwenye akili hawezi kutelekeza familia hata kama tumegombana, nimemwachia nyumba niliyojenga kwa pesa yangu na pesa zote aliweka kwenye akaunti yake na zote nilimwachia lakini kashindwa kuihudumia familia.”

Flora anajulikana kuwa na watoto wawili, mdogo akiwa ni yule aliyezaliwa wakati wanandoa hao wakiwa katika mzozo uliosababisha watengane hadi hivi sasa. Alipoulizwa kwa nini anadai aliyekuwa mumewe kumtelekeza mtoto mmoja tu, badala ya wawili, alifunguka.

“Huyu mwanangu mdogo hausiki naye kabisa, tena asiwe anamtaja kabisa kwa sababu hamhusu, hajui hata matumizi yake yakoje, mengine kaka achana nayo tu,” alisema Flora.

Mwimbaji huyo mwenye kipaji alipoulizwa sababu za kufuta kesi ya kudai talaka, aliyoifungua hivi karibuni katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati anadai hamtaki na hawezi kurudiana naye, alisema alifanya hivyo baada ya kushinikizwa na mtu ambaye hata hivyo, alikataa kumtaja.

Mwimba Injili Bongo, Flora Mbasha.

Flora alisema familia yake haijaridhishwa kabisa na suala la kesi ya ubakaji iliyokuwa ikimkabili mumewe kumalizika kwa kuachiwa huru na kwamba wanajipanga kwa ajili ya kukata rufaa.“Hiyo kesi imeisha kisiasa, Mbasha aliwahi kukiri kuwa ni kweli alifanya kitendo hicho, iweje leo aonekane hana hatia? Tutakwenda kukata rufaa ili haki itendeke.”

Baada ya kuzungumza na Flora, mwandishi wetu alimtafuta Mbasha kwa lengo la kumuuliza kuhusu madai ya mtoto yule mdogo kutohusika naye kama alivyosema mkewe, naye bila ‘kutafuna maneno’, alisema hata yeye hamtambui huyo mtoto mdogo, ila anaomba arudishiwe mtoto wake mkubwa, Liz na maisha mengine yaendelee.

“Hata mimi simtambui huyo mwingine, ninachoomba anirudishie tu mtoto wangu mkubwa Liz, huyo mwingine sihusiki naye kabisa kama alivyosema, yeye (Flora) ndiye anajua mhusika wa huyo mtoto, lakini si mimi na wala hajakosea kusema hivyo, nililitambua hilo tangu zamani, anipe tu mwanangu wa kwanza,” alisema Mbasha.

Imeandikwa na Brighton Masalu, Mayasa Mariwata na Gladness Mallya

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

Leave A Reply