The House of Favourite Newspapers

Jinsi ya Kumtambua Mwanaume wa Kukuoa!

WANAWAKE wengi wanateseka penzini kwa kutowatambua vizuri wanaume wenye mapenzi ya dhati.

Wengi hujikuta kwenye maumivu makali kwa sababu ya kuingia kwenye uhusiano na watu wasiokuwa na mapenzi ya dhati.

Wanaingia kwenye uhusiano na matapeli wa mapenzi kwa kutojua. Wanawekeza nguvu zao zote.

Mwanamke anautoa moyo wake kwa asilimia mia bila kujua mwanaume anayempa moyo wake hana mapenzi ya dhati.

Tatizo hili huchangiwa na hofu kubwa waliyonayo wanawake. Wengi wanapoona umri unawatupa mkono na akitazama watu wa umri wake wote wameolewa basi huchanganyikiwa.

Anaugawa moyo wake kama sadaka na kujikuta akiambulia maumivu kila uchwao.

Anaingia kwenye uhusiano na mwanaume ambaye ni muongo. Anaficha makucha yake, unaamini anakupenda kumbe wala. Mwizi tu. Ukiondoka anakung’ong’a. Pembeni anakuwa na wanawake wengine ambao nao anawadanganya vilevile.

Ukitaka kumtambua mwanaume mwenye mapenzi ya dhati, kwanza kabisa usithubutu kumpa moyo wako wote katika kipindi cha awali. Penzi linapoanza kuchipukia, ni vigumu sana kumtambua mtu kama ana mapenzi ya dhati.

Unaweza kushiriki naye baadhi ya vitu lakini kadiri muda unavyozidi kuyoyoma, utambaini tu kama ana mapenzi ya dhati au la.

Penzi la dhati halijalishi kipato, halijalishi zawadi kubwa lakini kuna vitu vidogovidogo ambavyo ukiviona kwa mwanaume basi ujue kweli anakupenda.

Mwanaume mwenye mapenzi ya dhati anakueleza misingi ya uhusiano wenu tangu awali. Anapenda kutafakari pamoja na mwanamke wake kila hatua wanayopiga.

Anaisimamia mikakati yake. Anakueleza ukweli kwa kila jambo.

Furaha yake si tendo tu pekee, mwanaume mwenye mapenzi ya dhati hata baada ya tendo ataendelea kuzungumza na wewe kuhusu maisha. Ataendelea kukushirikisha katika mipango yake ili kwa pamoja muweze kufikia kilele cha mafanikio yenu, ndoa na hata watoto.

Ukiona mwanaume anakuthamini kabla tu ya tendo na mkishafanya hana habari na wewe jua huyo mwanaume hana mapenzi ya dhati na wewe. Anakutumia tu kama chombo cha starehe na baada ya muda atakuacha solemba.

Mwanaume mwenye mapenzi ya dhati anajali. Unapomtazama machoni pindi mnapokuwa naye, anafurahia uwepo wako. Anachanganyikiwa na kukuhitaji ikiwezekana kila wakati. Penzi la dhati linajionesha tu, mtazame anavyokujali na kukuthamini.

Lazima ajivunie kuwa na wewe. Anakuwa huru kukutambulisha kwa ndugu, jamaa na marafiki. Hapati kigugumizi pindi mnapokuwa pamoja. Anayestahili kukutambulisha, atafanya hivyo kwa furaha na upendo wa hali ya juu.

Anaguswa kukujengea misingi ya kuwafahamu ndugu zake kwani anakuhitaji si kwa muda mfupi bali anakuhitaji kwa maisha yake yote. Anakuwa mkweli kwa kila jambo. Hakufichi kitu. Anakupa ratiba yake ya siku na ikibadilika atakueleza.

Anakueleza ratiba yake ili wewe kama mpenzi wake ujue. Anakutengenezea mazingira ya uaminifu kiasi kwamba hata akiwa mbali hutilii shaka. Unaamini anakuthamini. Hawezi kukusaliti. Unapokuwa na mtu wa aina hiyo, taratibu unaweza kumkabidhi moyo wako.

Mwanaume mwenye mapenzi ya dhati, hakudharau. Anakuheshimu kama mtu ambaye una nafasi katika maisha yake. Ukiona mwanaume anakudharau, hakupi heshima unayostahili basi jua hana mapenzi ya dhati kwako.

Kwa leo naishia hapo.

Comments are closed.