The House of Favourite Newspapers

Rushwa, rushwa rushwa

0

Stewart Hall

Kocha wa Azam FC, Stewart Hall.

Sweetbert Lukonge  na Hans Mloli

UNAWEZA ukasema amejitoa mhanga, kwani bila kuogopa hatua zozote ambazo zinaweza kuchukuliwa dhidi yake, kwa ujasiri mkubwa, Kocha wa Azam FC, Stewart Hall, amefunguka kwamba anahisi Yanga ilitoa rushwa kwa mwamuzi Abdallah Kambuzi wa Shinyanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara baina ya timu hizo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, juzi Jumamosi.

Katika mchezo huo uliokuwa unawakutanisha vinara wa ligi hiyo, Stewart anahisi kulikuwa na mazingira ya rushwa, hasa kuhusiana na penalti ambayo waliipata Yanga dakika za mwishoni ambayo ilitokana na kipa Aishi Manula kugongana na kiungo mshambuliaji Simon Msuva.

Kocha huyo raia wa Uingereza awali ilielezwa aligoma kuzungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo lakini baadaye aliibuka kwenye mkutano huo na kuzungumza kwa jazba na kugonga meza kwa nguvu, akidai Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), linavilea vitendo vya rushwa.

Hata hivyo, penalti waliyoipata Yanga iliyopigwa na kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko iliota mbawa baada ya kupanguliwa na Manula.

Kitendo hicho cha kuamuliwa kupigwa kwa penalti, kilionekana kumkera Stewart na kujikuta akitoa maneno ya kashfa kwa Yanga lakini pia akilishtumu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwamba linavilea vitendo vya rushwa.

Kauli za Stewart zilionyesha wazi kuwa Yanga walitoa mlungula kwa mwamuzi ili waweze kushinda mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkubwa.

“Sijafurahishwa kabisa na maamuzi ya mchezo wa leo (juzi), TFF wanatakiwa kuachana na vitendo vya kulea rushwa na waamuzi wanatakiwa kujirekebisha,  kama hivyo bora ligi ibakie na Yanga pekee na sisi wengine tuondoke kwani haina faida ya kuendelea kushiriki ligi.

“Sina zaidi ya hayo na nimeyasema kutoka moyoni na wala siogopi mtu yeyote na naomba mkaandike hivyohivyo kama nilivyosema,” alisema Stewart kwa sauti ya juu iliyokuwa imetokana na kufura kwa hasira huku akipiga meza kwa nguvu akitumia mkono wake wa kushoto.

Hata hivyo, kabla ya Stewart kutoa kauli hiyo, taarifa za awali kutoka kwa Ofisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto, zilisema kuwa kocha huyo alikuwa amegomea kuja katika chumba cha mkutano na waandishi wa habari.

Kutokana na maneno ya kocha huyo, Pluijm aliyekuwa kwenye mkutano huo, alionekana kutofurahia kwani alikuwa akimshangaa huku akitikisa kichwa kisha akasema machache kuhusiana na hilo.

“Kama kocha hutakiwi kufanya hivyo, unatakiwa kuelewa kuwa ule ni mchezo na siyo vizuri kuhusisha na mambo ya rushwa, hata mimi sikufurahishwa na matokeo ya sare.

“Haimaanishi kuwa kama ulishinda mechi zote za nyuma hivyo ni lazima ushinde na huu wa leo (juzi), hivyo alipaswa kujua kuwa hayo ni matokeo na hutokea kwa kila timu,” alisema Pluijm.

Stewart aliwahi kufungiwa mechi tatu na TFF Januari 2013, kwa kosa la kuvua nguo na kutoa lugha chafu kwa mwamuzi. Pia alipigwa faini ya Sh laki tano. Ilikuwa ni baada ya mechi ya Azam dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Chamazi, iliyomalizika kwa Azam kushinda 3-1.

Leave A Reply