The House of Favourite Newspapers

The Angel of darkness -18

0

angel_of_darkness_by_renutheartist-d4yb93pShambulizi kubwa la kigaidi linatokea kwenye kituo kikubwa cha biashara nchini Kenya, Kikuyu Mall na kusababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Wakenya, Watanzania na watu wengine kutoka mataifa mbalimbali.

Miongoni mwa wahanga wa tukio hilo la kikatili, wamo Watanzania, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam, mkewe, Asia Mustafa na watoto wao mapacha waliokuwa bado wachanga, Arianna na Brianna.

Kwa bahati mbaya, Ndaki na mkewe wanapoteza maisha katika tukio hilo, maiti zao na za Watanzania wengine zinasafirishwa mpaka nchini Tanzania ambako hatimaye wanazikwa.

Pacha wa kwanza, Arianna anapatikana na kurejeshwa nchini Tanzania ambako anakabidhiwa kwa ndugu zake. Bado haifahamiki pacha mwingine, Brianna yuko wapi na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Upande wa pili, mwanamke mwenye upungufu wa akili, Mashango anamuokota Brianna kwenye shambulizi hilo na baadaye anahamia kwenye kitongoji cha watu maskini, Mathare, pembezoni kidogo mwa Jiji la Nairobi, mahali anakoweka makazi yake.

Maisha yanazidi kusonga mbele huku mtoto huyo japokuwa alikuwa mdogo, akimpa changamoto kubwa za kimaisha Mashango. Baadaye Brianna anaanza masomo na kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo maisha ya Mashango yanavyoanza kubadilika.

Anaanza kufanya biashara ya mbogamboga na matunda na kuishi maisha ya kawaida kama binadamu wengine. Hata hivyo bado kuna watu ambao hawaamini kwamba mwanamke huyo amepona, wanamfanyia fitina za hapa na pale na kusababisha akamatwe na mgambo wa Jiji la Nairobi.

Hata hivyo anaonekana hana hatia. Wanamuachia lakini kwa bahati mbaya, wakati akirejea kwenye eneo lake la biashara anapata ajali mbaya ya kugongwa na gari na kupoteza maisha papo hapo. Hilo linakuwa pigo kubwa kwa maisha ya Brianna.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO

…Maisha yalibadilika, hayakuwa kama yale yaliyopita kwa Arianna, hakuwa na maisha mazuri kama kipindi kile ambacho Hans na mkewe walikuwa wakimtunza. Kipindi hiki, hata kula kwake ilikuwa ni kwa shida sana.

Hans alikimbia na mkewe, alipokimbilia, hakukuwa na mtu aliyefahamu na hivyo kuacha jukumu kubwa la kumlea Arianna likiwa kwa mjomba wake aliyejulikana kwa jina la Michael Msaki.

Mzee Michael hakuwa na maisha mazuri sana, aliishi maisha ya kawaida na familia yake, kila siku, alikuwa mtu wa kula milo miwili, asubuhi na usiku au wakati mwingine kubadilika na kula mchana na usiku.

Arianna hakuyazoea maisha hayo, hakuwahi kuishi katika maisha ya shida, yalimsumbua na kumfanya kuwa na mawazo kipindi chote, hata shuleni, hakuwa na furaha, mawazo yalimsonga na hata afya yake ilibadilika kabisa.

Kwa kuwa hakukuwa na fedha na hata shule aliyokuwa akisoma ya ‘International’, mzee Michael na mkewe wakashindwa kulipia ada, hivyo Arianna akafukuzwa na kwenda kusoma katika shule ya kawaida ambayo ilijulikana kama shule za Kayumba.
“Ila ataweza kusoma huko?” aliuliza mke wa Michael.

“Itabidi iwe hivyo, hatuna hela ya kumsomesha alipokuwa akisoma, itabidi tu azoee kusoma huko,” alisema mzee Michael.

Kila kitu kilibadilika, shule aliyokwenda kusoma Arianna haikuwa ile iliyotawaliwa na watoto waliokuwa wakizungumza Kingereza tu, huko alipokwenda kusoma, ilikuwa shule iliyojaza watoto wengi wa uswahilini ambao kwao, kutukana ilikuwa kawaida, kupigana na hata kufanya mambo mengine yaliyoonekana kuwa ya kijinga ilikuwa kawaida sana.

Miaka ikakatika, alipoingia darasa la sita, mwaka mmoja kabla ya kumaliza darasa la saba, Arianna akampata rafiki wa kike aliyetokea kuwa naye karibu sana, huyu aliitwa Fatuma, kutokana na tabia yake mbaya shuleni, wanafunzi wengi walimuita Fatuma Mapepe aliyekuwa akiishi Tandale Kwamtogole.

Japokuwa alikuwa na umri mdogo lakini Fatuma hakuwa kama wanafunzi wengine, alikuwa na tabia mbaya, chafu ambazo hazikumpendeza mtu yeyote yule aliyekuwa akiishi naye.

Alikuwa na umri wa miaka kumi tu lakini alikuwa mvutaji mkubwa wa sigara, kutembea na wanaume wengi na hata siku nyingine kutokwenda kabisa shule, alikuwa akibana boda kuendelea na maisha yake, aliporudi nyumbani, wazazi walijua kwamba alitoka shuleni.

Huyo ndiye akawa rafiki mkubwa wa Arianna. Kila walipokuwa, walikuwa pamoja, walitembea pamoja na hata muda wa kwenda nyumbani walikwenda pamoja pia. Kila mtu aliyemuona Arianna akiwa na Fatuma, alichukia kwani walijua tu kwamba msichana huyo ilikuwa ni lazima kuharibikiwa.

Walimu hawakutaka kuona jambo baya likitokea, walichokifanya ni kumuita Arianna na kumkemea kutembea na Fatuma lakini hilo halikusaidia, alikemewa asubuhi ila walipoondoka, waliondoka pamoja.

Siku zikaendelea kukatika, taratibu naye Arianna akaanza kujifunza kuvuta sigara, alianza kwa shida, kukohoa sana lakini mwisho wa siku akajikuta akianza kuzoea.

Mbali na sigara, akaanza kunywa pombe kisiri, walikunywa siku walipokuwa wakibana boda, ingawa mara ya kwanza zilikuwa na ladha ya uchungu mdomoni mwake lakini mwisho wa siku akazoea na kuwa mnywaji mzuri wa pombe.
“Fatuma, nini hiyo?” aliuliza Arianna.
“Ipi? Hii?”
“Ndiyo!”

“Kwani hauijui?”
“Hapana! Ni sigara?”
“Hakuna! Hii inaitwa bangi!”
“Bangi?” aliuliza Arianna kwa mshtuko.
“Ndiyo! Ushawahi kuvuta?”
“Hapana! Ila nasikia ni mbaya!”

“Aliyekwambia alikudanganya! Ukivuta, inakuletea stimu, unajiona upo Marekani ukizungumza na Obama!”
“Kweli?”

“Kweli! Hebu piga pafu moja.”
“Ila naogopa!” Unaogopa nini bwana! Hebu jaribu!”
Maneno ya kishawishi aliyoongea Fatuma yakamuingia Arianna na mwisho kujikuta akichukua bangi ile na kuanza kuvuta kama alivyoambiwa. Moshi wake ulikuwa mzito mdomoni, hata ulipomuingia, haukuwa kama moshi wa sigara.

Alihisi moshi ule ukiingia katika mishipa yake na kusafiri mpaka ubongoni mwake, alipoendelea kuvuta hasa kwa kupuliza mara tano, akajikuta akiona vitu vya ajabuajabu mbele yake.

Kadiri siku zilivyozidi kuendelea mbele, Arianna alizidi kubadilika, nyumbani akaanza kuwa jeuri, alipoambiwa fanya hili, hakutaka kufanya, alichokuwa akikifikiria ni kuondoka kwenda kwa kina Fatuma kisha kufanya mambo yao.

Kwa sura yake nzuri, alionekana kuwa msichana mpole, asiye na makeke na hata yale mambo aliyokuwa akiyafanya, wengi walimuonea huruma kwa kuona kwamba angepotea kabisa maishani mwake.

Aliitwa na watu wengi, alishauriwa, aliambiwa abadilike, hakukubali, ulevi alioufanya ukamchanganya mpaka kufika kipindi kila mmoja akaona kwamba kwa kasi aliyokuwa nayo basi hata Fatuma asingeweza kwenda naye sawa, alionekana kuwa zaidi ya msichana huyo.

Kutoka maisha ya kishua, kupelekwa nyumbani na gari, kuwa na maisha bora, leo hii, Arianna alibadilika kabisa na kuwa mhuni wa kutupwa, maisha yake yalibadilika kwa asilimia mia moja huku uhuni ukizidi kumtawala kila siku na kumpotezea dira ya maisha yake.

Leave A Reply