The House of Favourite Newspapers

The Angel Of Darkness 21

0

Shambulizi kubwa la kigaidi linatokea kwenye kituo kikubwa cha biashara nchini Kenya, Kikuyu Mall na kusababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Wakenya, Watanzania na watu wengine kutoka mataifa mbalimbali.

Miongoni mwa wahanga wa tukio hilo la kikatili, wamo Watanzania, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam, mkewe, Asia Mustafa na watoto wao mapacha waliokuwa bado wachanga, Arianna na Brianna.

Kwa bahati mbaya, Ndaki na mkewe wanapoteza maisha katika tukio hilo, maiti zao na za Watanzania wengine zinasafirishwa mpaka nchini Tanzania ambako hatimaye wanazikwa.

Pacha wa kwanza, Arianna anapatikana na kurejeshwa nchini Tanzania ambako anakabidhiwa kwa ndugu zake. Bado haifahamiki pacha mwingine, Brianna yuko wapi na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Upande wa pili, mwanamke mwenye upungufu wa akili, Mashango anamuokota Brianna kwenye shambulizi hilo na baadaye anahamia kwenye kitongoji cha watu maskini, Mathare, pembezoni kidogo mwa Jiji la Nairobi, mahali anakoweka makazi yake.

Maisha yanazidi kusonga mbele huku mtoto huyo japokuwa alikuwa mdogo, akimpa changamoto kubwa za kimaisha Mashango. Baadaye Brianna anaanza masomo na kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo maisha ya Mashango yanavyoanza kubadilika.

Anaanza kufanya biashara ya mbogamboga na matunda na kuishi maisha ya kawaida kama binadamu wengine. Hata hivyo bado kuna watu ambao hawaamini kwamba mwanamke huyo amepona, wanamfanyia fitina za hapa na pale na kusababisha akamatwe na mgambo wa Jiji la Nairobi.

Hata hivyo anaonekana hana hatia. Wanamuachia lakini kwa bahati mbaya, wakati akirejea kwenye eneo lake la biashara anapata ajali mbaya ya kugongwa na gari na kupoteza maisha papo hapo. Hilo linakuwa pigo kubwa kwa maisha ya Brianna.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Mzee Michael na mkewe hawakujua kilichokuwa kikiendelea kwa Arianna, kila siku walikaa naye lakini hawakugundua kwamba msichana huyo alibadilika kwa kiasi kikubwa.

Walipokuwa naye, Arianna alionyesha kuwa na nidhamu ya hali ya juu huku muda mwingi akijifanya kusoma, yote hayo alifanya kwa kuwa alitaka kuwatia upofu wasijue kile alichokuwa akikifanya nyuma ya pazia.

Akamalizia darasa la sita na kuingia darasa la saba. Hapo ndipo alipojiona kumaliza kila kitu, alipojiangalia, alijiona kuwa msichana mkubwa aliyekuwa na uhuru wa kuamua kufanya kitu chochote kile alichotaka.

Mabadiliko makubwa aliyoyaonyesha shule yaliwafanya walimu kumuagiza kuwaleta wazazi wake shuleni, ila kitu alichokifanya, watu aliwaopeleka shuleni aliosema kwamba walikuwa wazazi wake, haikuwa hivyo, aliwalipa watu na kwenda shule, kila kitu kilichoendelea bado kilikuwa siri kubwa.

“Hivi Arianna binti yangu! Mbona umebadilika hivi?” aliuliza mwalimu Mwajuma, kwa kumwangalia usoni mwake tu, ungeona ni jinsi gani alikuwa na maumivu mazito juu ya mabadiliko ya msichana huyo.

“Nani? Mimi?” aliuliza Arianna huku akijua mahali hapo walikuwa wao wawili tu.

“Ndiyo! Hebu niambie tatizo nini.”

“Hakuna tatizo mwalimu.”

“Hapana Arianna, kuna tatizo sehemu, hebu niambie. Usizungumze nami kama mwalimu wako, zungumza nami kama mzazi wako, niambie tatizo nini,” alisema mwalimu Mwajuma.

“Hakuna tatizo mwalimu. Kungekuwa na tatizo ningekwambia.”

“Sawa! Kama hakuna tatizo, nenda japokuwa najua kuna kitu, haiwezekani ubadilike hivyo,” alisema mwalimu Mwajuma.

Arianna aliondoka huku akijua kwamba alimficha mwalimu Mwajuma pasipo kujua kwamba mwalimu huyo alifahamu kila kitu.

Alipoingia shuleni hapo kipindi cha nyuma, alikuwa na uwezo mkubwa darasani ila kwa sababu alianza kuharibikiwa hata uwezo wake wa darasani ukaanza kushuka. Hakuacha kuvuta sigara, hakuacha kubana boda, ndani ya wiki moja, siku nne alizitumia kujificha huku ni siku moja tu ndiyo aliyoingia darasani, tena hakukaa sana, alikaa kwa saa nne kisha kuondoka zake.

“Fatuma…”

“Unasemaje?”

“Hiyo unayonusa ni nini? Maziwa?”

“Hapana! Hii inaitwa poda!”

“Poda? Ya kupaka?”

“Hapana! Hebu sogea,” alisema Fatuma huku akimwambia amsogelee.

 Hiyo haikuwa poda kama alivyofikiria, hayo yalikuwa madawa ya kulevya ambayo Fatuma aliyanunua kutoka kwa wahuni aliokuwa akiishi nao jirani. Huo ulikuwa mwanzo wa Arianna kujifunza kutumia madawa hayo.

Alianza kwa kuvuta kama alivyofanya Fatuma lakini baada ya miezi miwili, akaanza kuyatumia kwa kujichoma sindano. Mpaka kufikia hatua hiyo, hata ule unafiki alioufanya nyumbani ukakoma, haukufanyika tena, akajiweka wazi hali iliyomfanya hata mzee Michael, mkewe na ndugu zake wengine kumshangaa.

“Unasemaje?” aliuliza shangazi yake aliyeitwa kwa jina la Dora.

“Hatumuelewi kabisa Arianna kwa sasa!”

“Kivipi?”

“Yaani kama anatumia madawa ya kulevya hivi!”

“Anatumia madawa ya kulevya?”

“Ndiyo! Yaani anatuchanganya sana.”

“Na shule anakwenda?”

“Ndiyo!”

“Mna uhakika anafika?”

“Yaani sijui tuseme vipi, ngoja tukaangalie.”

Huo ndiyo uamuzi waliouamua, hawakutaka kuendelea kusubiri, walitakiwa kupata taarifa kutoka shule kwamba msichana huyo alikuwa akifika shule au aliishia njiani.

Njiani,  kila mmoja alionekana kuwa na mawazo, maneno aliyoyaongea shangazi yake Arianna, Dora yaliwazibua masikio yao na kuona kwamba kama Arianna alikuwa amebadilika, sehemu ya kwanza kabisa ambayo ingewafanya kufahamu mwanzo wake ilikuwa shule.

Walipofika hapo, walimu wakawashangaa, hawakuwahi kuwaona, walikuwa wageni machoni mwao. Hata walipojitambulisha kwamba walikuwa walezi wa Arianna, hakukuwa na aliyeamini kwani kipindi ambacho walimtaka kuwaita wazazi wake, kulikuwa na watu waliofika hapo.

“Hapana! Wazazi wake tunawajua,” alisema mwalimu Mwajuma huku walimu wote wakishangaa.

Hapo ndipo mze Michael na mkewe walipopata kazi ya ziada kumzungumzia Arianna tangu siku ya kwanza alipochukuliwa na Hans, alipotoroka na mkewe mpaka wao walipomchukua na kuishi naye.

Historia yake iliwashangaza walimu wote, hawakujua kwamba msichana kama Arianna alipitia maisha maisha yale waliyokuwa wakiambiwa. Kwa kiasi fulani wakawaamini watu hao kwani siku zile za kwanza Arianna kufika shuleni hapo uwezo wake darasani ulikuwa mkubwa mno.

“Mmh! Inawekana!”

“Ndiyo hiyo! Yupo wapi?” aliuliza mzee Michael.

“Arianna! Hayupo. Hii wiki ya pili hajafika shuleni,” alijibu mwalimu Mwajuma, mzee Michael na mkewe wakapigwa na mshtuko, hawakuamini kile walichojibiwa kwamba msichana huyo hakuwa amefika shule kwa wiki ya pili.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

Leave A Reply