The House of Favourite Newspapers

Ni Zaidi Ya Unyama, Mtoto Miaka 3 Abakwa Hadi Kufa

DUNIA katili na inawezekana kabisa hizi ni dalili ya siku za mwisho! Ndiyo kauli inayoweza kukutoka unaposoma madai haya ambayo ni zaidi ya ukatili juu ya mtoto kubakwa hadi kufa, Risasi Mchanganyiko lina mkasa huu wa kukutoa machozi.

 

NI TABATA-KINYEREZI

Tukio hilo la kusikitisha lilijiri wiki iliyopita ambapo mtoto huyo (jina linahifadhiwa kwa sababu za kimaadili), mkazi wa Tabata-Kinyerezi jijini Dar kabla ya kuhamia kwa mama yake maeneo ya Majumba- Sita, Ukonga jijini Dar ambapo alidaiwa kufanyiwa ‘unyambilisi’ huo uliosababisha kupoteza na mtu anayedaiwa ni wa kufikia.

 

BIBI ASIMULIA KWA UCHUNGU

Akilisimulia Risasi Mchanganyiko mkasa huo mzito huku akiwa na uchungu wa kumpoteza mjukuu wake, bibi wa mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina moja Nlay au Mama Ngonyani alisema kuwa, tukio hilo lilijiri Alhamisi ya wiki iliyopita.

 

Alisema, akiwa nyumbani kwake, Tabata-Kinyerezi, Dar, alipigiwa simu na mwanaye aliyemtaja kwa jina moja la Cathy ambaye alimjuza kuwa mtoto wake (mjukuu) anaumwa mno.

 

Alisema, baada ya binti yake kumwelezea tatizo la mjukuu wake huyo ambaye walikuwa wamempeleka mkoani Morogoro kwa ajili ya matibabu. Anasimulia; “Nilipigwa na mshangao mkubwa maana ninavyojua mwanangu anaishi na mtoto wake maeneo ya Majumba-Sita kule Ukonga (Dar), sasa iweje mtoto azidiwe na kupelekwa Morogoro!

 

“Mwanangu alinipigia simu na kunisisitiza niwafuate huko walipo ambapo jambo hilo mimi lilinishinda, lakini baada ya muda nikasikia hukohuko walipo mtoto amezidiwa sana hivyo wamekodi gari la wagonjwa (ambulance) na kumleta Dar katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.”

APOTEZA MAISHA MUHIMBILI

Aliendelea kusimulia kuwa mjukuu wake huyo alianza matibabu, lakini Jumamosi iliyopita alipoteza maisha kwenye Hospitali ya Muhimbili katika kifo hicho kilichoacha utata mzito.

 

MJUMBE SERIKALI YA MTAA

Akizungumzia tukio hilo lililoacha simanzi kubwa, Mjumbe wa Shina Namba 50 Mtaa wa Kingezi-Kifuru, Kinyerezi jijini Dar ambako ndiko nyumbani kwa bibi wa mtoto huo, Halima Sheshe alithibitisha kutokea tukio hilo kwenye eneo lake na kusema;

 

“Baada ya kutokea tukio hili, nilifika msibani na kuongea na bibi wa marehemu (Nlay) ambaye aliniambia mjukuu wake amefariki dunia kwa kubakwa na mtu aliyedai ni mtu wa kufikia ambaye anashikiliwa na polisi.”

 

MWANANDUGU

Katika kuendelea kupata undani wa tukio hilo, wanahabari wetu walizungumza mmoja wa wanandugu wa familia hiyo ambaye alisema utata zaidi uliibuka kabla ya kifo cha mtoto huyo ambaye alikuwa akitokwa na uchafu puani uliodaiwa kusababishwa na kuingiliwa kimwili.

 

Kufuatia utata huo, ndugu huyo alisema ilibidi mtuhumiwa huyo ashikiliwe na jeshi la polisi, akidaiwa kuhusika na tukio hilo. Baada ya kusikiliza kila upande, mwanahabari wetu walimtafuta Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Kamishna Msaidizi (ACP) Zuberi Chembera ambaye alisema tukio hilo bado halijamfikia mezani kwake na kuomba atafutwe baadaye.

 

Kamanda huyo alipotafutwa baadaye alimwambia mwandishi wetu alikuwa bado hajarudi ofisini na kumuomba kuzidi kuwa na subira. Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni kamanda huyo alikuwa hajalirudia gazeti hili.

 

MAZISHI

Mazishi ya mtoto huyo ambayo yalitawaliwa na vilio kila kona yalifanyika wikiendi iliyopita katika Makaburi ya Kingezi-Kifuru, Kinyerezi jijini Dar

Hata hivyo, gazeti hili linaahidi kufuatilia sakata hilo hadi kujua hatma yake

STORI: NEEMA ADRIAN NA RICHARD BUKOS, DAR

Comments are closed.