The House of Favourite Newspapers

Uchunguzi: Kansa Sasa Janga La Kitaifa! – 2

DAR ES SALAAM: Wiki iliyopita tulianza kutoa ripoti ya uchunguzi wetu juu ya ugonjwa wa kansa au saratani ambavyo umegusa familia zilizo nyingi na sasa inaonekana ni janga la kitaifa.

Kwa mujibu wa Dokta Makere tuliyezungumza naye wiki iliyopita alieleza ni kwa jinsi kansa zilivyo za aina nyingi, zaidi ya 100 ambazo zimekuwa zikitafuna binadamu ili zipate kumwangamiza.

 

Ndiyo kwanza ripoti hii imeanza, kama unataka kujua ukubwa wa janga hili na mamlaka kupitia Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto chini ya Waziri Ummy Mwalimu zinachukua hatua gani, tuwe pamoja.

 

Dokta Makere anasema kansa ni muunganiko wa magonjwa ambayo mara zote husababishwa na uzalishwaji wa seli za mwili kupita kiasi kinachohitajika na seli hizo huendelea kujigawa kupita kiasi na kutengeneza kiasi kikubwa kuliko mwili unavyoweza kuhimili.

 

Anasema ukuaji huu wa seli hizi unaweza kusababisha vimbe mbalimbali katika mwili na uvimbe unavyokuwa mkubwa unasababisha kubanwa kwa baadhi ya viungo muhimu mwilini kama vile neva, mishipa ya damu, ubongo, mapafu na vingine na kutofanya kazi yake vizuri.

 

SI KILA UVIMBE NI KANSA

Kama alivyoeleza mtaalam huyo, kuna kansa za aina nyingi mno. Tafiti za kisayansi zinaonesha zaidi ya aina 100 za kansa zinawapata watu na kwa kawaida huwa ni vigumu sana kutambua pale unapoanza. Mara nyingi mgonjwa anajitambua baada ya ugonjwa kukomaa mwilini.

 

Kwa kuwa kansa ni ugonjwa ambao kwa kawaida huwa unakuja kwa kujificha, ni vigumu mno kwa mtu kujitambua kama ana ugonjwa huu au yupo katika hatari ya kushambuliwa na ugonjwa huu kutokana na uelewa mdogo hadi pale anapopata uvimbe, lakini si kila uvimbe ni kansa.

 

Dokta Makere anasema dalili kama uvimbe, kutokwa damu sehemu mbalimbali za mwilini ambako si kwa kawaida, kukohoa na kikohozi kisichokwisha, kupoteza uzito kwa kasi na mabadiliko katika mfumo wa mmeng’enyo wa chakula, ukiona dalili hizi, hupaswi kuzifumbia macho, huenda ukawa hatarini kuugua kansa.

 

Madoamadoa na uvimbe mpya kwenye ngozi au kingo za ngozi kubadilika umbile au muonekano wake halisi na hata rangi, ni ishara ya kansa ya ngozi.

Kingine ni vipele vikubwa ambavyo huwa vinavimba na ukivitomasa unahisi ugumu sana ndani yake na vinaambatana na maumivu ya kawaida.

 

Daktari huyo anasema vipele hivi vinaweza kutokea sehemu yoyote ya mwili na kwa muonekano wake havifanani kabisa na vipele vya magonjwa ya ngozi ya kawaida. Kama unaona kwenye ngozi una alama ambazo unahisi si za kawaida, ni vizuri kumuona daktari ili akufanyie vipimo vya ngozi.

 

“Daktari ataondoa sehemu ndogo ya ngozi yako na kuifanyia vipimo ili kuangalia uwezekano wa uwepo wa seli za saratani katika ngozi yako. Kipimo hiki cha kuondoa sehemu ya ngozi kitaalamu kinaitwa ‘Biopsy’.

 

“Kwa wanawake, mabadiliko kwenye matiti, si kila mabadiliko yanayotokea kwenye matiti yanaashiria kansa. Lakini pia bado ni muhimu sana kuwasiliana na daktari kuhusu mabadiliko yoyote yanayojitokeza kwenye matiti ili ayafanyie uchunguzi.

 

“Mjulishe daktari kuhusu uvimbe wa aina yoyote, mabadiliko katika chuchu ikiwemo kuziba kwa chuchu, uwepo wa rangi nyekundu au kuhisi ugumu au maumivu kwenye matiti kwa jumla. Daktari atakufanyia kipimo cha X-Ray kwenye titi. Kipimo hiki kwa kitaalam kinaitwa Mammogram. Kipimo hiki kinatumika kuchunguza kansa ya matiti kwa wanawake ambao hawana dalili za kansa ya matiti.

 

“Kujaa gesi mfululizo, mara nyingi unaweza kuhisi unajaa gesi tumboni, yaweza kuwa ni aina ya vyakula unavyokula au kiafya hata msongo mkubwa wa mawazo pia una uhusiano mkubwa na matatizo ya kujaa gesi.

 

“Lakini pia kama hali hii inadumu kwa muda mrefu inaweza kusababisha uchovu, kupungua uzito na maumivu ya mgongo, basi ni vema kupatiwa vipimo. Kujaa gesi kwa muda mrefu kwa wanawake ni ishara kubwa ya kansa ya mayai ya uzazi (ovarian cancer).

 

“Ili kuchunguza aina hii ya kansa, daktari anachunguza sehemu za ndani za via vya uzazi kama mlango wa kizazi (cervix), mayai ya uzazi (ovaries), mrija wa falopia (fallopian tube), mfuko wa uzazi (uteras) na uke (vagina). Kipimo hiki kitaalam kinaitwa ‘pelvic examination’.

 

“Matatizo wakati wa haja ndogo, wanaume wengi hupatwa na matatizo ya njia za mkojo kadiri umri unavyokuwa mkubwa. Wale wanaoingia katika rika la uzee ndio wahanga hasa. “Matatizo haya ni kama kujisikia kukojoa mara kwa mara, mkojo kuvuja matone machache hata kabla ya kwenda haja, lakini hata pia njia ya mkojo kuwa dhaifu.

 

“Kwa kawaida hizi ni ishara kuwa tezi dume imeongezeka ukubwa wake wa kawaida au imepata uvimbe hivyo kuashiria kansa ya tezi dume. Ni vema kumuona daktari haraka na ni muhimu pia kufanyiwa vipimo maalum vya damu ambavyo kitaalam vinaitwa Prostate Specific Antingen Test (PSA).

“Kipimo hiki ni maalum kwa ajili ya kuchunguza kansa ya tezi dume,” anaendelea kueleza daktari huyo.

Itaendelea wiki ijayo.

Stori: WAANDISHI WETU,Ijumaa

Comments are closed.