The House of Favourite Newspapers

Kwa rekodi hizi Yanga ni kiboko yao

0

Yanga-training.jpgKikosi cha timu ya Yanga wakifanya mazoezi.

Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

HAKIKA rekodi zinaonyesha kuwa Yanga ndiyo timu hatari zaidi kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu pamoja na kwamba ipo nafasi ya pili.SIMBA-YANGA-12.jpg Yanga inashika nafasi ya pili kwenye ligi hiyo baada ya kucheza michezo tisa, ikiwa nyuma ya vinara Azam kwa tofauti ya pointi mbili tu.

Yanga, Simba na Azam, ndizo timu zinazopewa nafasi kubwa zaidi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu na rekodi za ligi hiyo zinaonyesha kuwa Yanga wanaweza kufanya vizuri zaidi.

Kufungwa:

Katika michezo hiyo tisa, Yanga imeruhusu nyavu za lango lake kutikiswa mara tano tu, sawa na Azam ambayo ipo kileleni kwenye ligi hiyo, lakini Yanga ikiwa imefanikiwa kufunga mabao 22, ambayo ni mawili mbele ya Azam ambayo imefunga mabao 20.

Hii ina maana kuwa endapo kasi itakuwa kama ilivyo halafu Yanga na Azam wakalingana kwa pointi, basi vijana hao wa kocha Hans van Der Pluijm, watakuwa na nafasi ya kuongoza kwenye Ligi Kuu ya Vodacom kutokana na kuwa na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Wafungaji:

Yanga ambayo mshambuliaji wake Donald Ngoma anashika nafasi ya pili kwenye ufungaji, inaonekana kuwa timu yenye safu kali zaidi ya ufungaji kuliko nyingine zote kwenye ligi ya msimu huu.

Pamoja na Ngoma kuwa na mabao nane pia Amissi Tambwe anashika nafasi ya tano kwenye ufungaji akiwa amepachika mabao matano.

Hii inamaana kuwa Yanga pekee ndiyo timu ambayo ina wafungaji wawili kwenye tano bora ya chati hiyo, ikiwaacha vinara Azam ambao wameingiza mchezaji mmoja tu kwenye msimamo huo, Simba wakiwa pia wameingiza mmoja na Stand mmoja.

Hii inaonyesha kuwa Yanga inaweza kuwa na mfungaji bora mwishoni mwa msimu huu hata kama Ngoma ataondoka kwenye timu hiyo kabla msimu haujamalizika.

Dakika:

Mechi tisa za mwanzo zinaonyesha kuwa Yanga inaweza kuifunga timu yoyote kwa dakika yoyote ile uwanjani.

Timu hiyo imeweza kuzifunga timu kwenye dakika za mwanzoni sana, ukiwemo mchezo dhidi ya Coasta Union ambao walifunga bao dakika ya nane lakini pia wakafunga dakika ya tisa kwenye mchezo dhidi ya Toto African.

Ukitazama dakika za mwisho timu hiyo iliweza kufunga bao katika dakika ya 87 ilipovaana na JKT Ruvu na dakika ya tisini ilipovaana na Mtibwa na hii inaonyesha kuwa ni timu ambayo inaweza kupambana kuanzia mwanzo mpaka mwisho.

Nyumbani na ugenini:

Hofu kwa Yanga sasa siyo michezo ya ugenini bali ile ambayo wanacheza kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Pamoja na kupata sare moja kwenye Uwanja wa Taifa dhidi ya Azam na nyingine kwenye Uwanja wa Kambarage dhidi ya Mwadui, timu hiyo imeruhusu mabao matatu kwenye uwanja wake wa nyumbani na mawili ugenini.

Kufungwa mabao machache ugenini bado kunaonyesha kuwa timu hiyo inaweza kufanya vizuri tofauti na timu nyingi ambazo zimekuwa zikifanya vibaya ugenini.

Kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara timu nyingi zimekuwa zikizuiwa kutwaa ubingwa kutokana na kufanya vibaya kwenye michezo ya ugenini, hali ambayo wenyewe inawapa mwanga mzuri.

 

Leave A Reply