The House of Favourite Newspapers

Kaze: Mbona Bado, Mtafurahi Sana Yanga

0

BAADA ya kupata ushindi katika mchezo wake wa kwanza, Kocha Mkuu wa Yanga, Mrundi Cedric Kaze, amesema kuwa amefurahishwa na kuridhishwa na matokeo ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania huku akiahidi kuwapa furaha zaidi mashabiki wa timu hiyo.

 

Kauli hiyo aliitoa mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara walipocheza dhidi ya Polisi juzi kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar.

 

Kocha huyo alipata ushindi huo akiwa amekaa kwa mara ya kwanza kwenye benchi la timu hiyo akichukua nafasi ya Mserbia, Zlatko Krmpotic aliyesitishiwa mkataba.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Kaze alisema kuwa licha ya kupata ushindi, amepanga kuendelea kuboresha maeneo yenye upungufu kuelekea mchezo ujao dhidi ya KMC watakaoucheza kesho Jumapili kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

 

Kaze alisema kuwa bado anataka kuona timu yake ikiendelea kucheza soka safi la pasi na kasi wakati timu ikiwa na mpira kama walilolicheza juzi dhidi ya Polisi Tanzania.

 

Aliongeza kuwa amefurahishwa na baadhi ya wachezaji aliowaanzisha katika kikosi chake cha kwanza waliocheza mchezo huo ambao ndani ya siku nne alizokaa nao walionekana kushika falsafa huku akiamini katika mchezo ujao watacheza soka safi la kuvutia zaidi.

 

“Nimepokea pongezi nyingi  kutoka kwa mashabiki wa Yanga wakinipongeza kwa timu kuonyesha mabadiliko kidogo hasa timu ikiwa na mpira ngumu kuupoteza huku tukishambulia goli la wapinzani muda wote.

 

“Niwaambie mashabiki wa Yanga kuwa, huo ni mwanzo tu bado mengi yanakuja kama unavyofahamu nimekaa na timu muda mchache kwa siku nne ambazo ni ndogo, hivyo kuna vitu vya kuboresha ili kuhakikisha timu inacheza soka lile ninalolitaka mimi la pasi nyingi na kasi.

 

“Hivi sasa nazifanyia kazi baadhi ya sehemu zenye upungufu ikiwemo safu ya ushambuliaji ambayo yenyewe inaonekana kushindwa kutumia nafasi nyingi na hiyo ni kutokana na timu kutokuwa na muunganiko mzuri tunapofika goli la mpinzani.

 

“Kingine ni kuwa timu inakuwa haina haraka kutafuta mpira pale tunapopoteza. Tumefanya mazoezi kwa siku nne tu, naamini mambo mengi yatakuwa sawa kadiri tunavyoendelea kujiimarisha. Bado tuna mechi nyingi hadi kufikia kumaliza msimu, hivyo tunajipanga kukabiliana na mchezo mmoja mmoja,” alisema Kaze.

 

Jeshi laifuata KMC kibabe, Carlinhos ndani Ofisa Habari wa Yanga, Hassa Bumbuli amesema msafara wa wachezaji 27 akiwemo Carinhos, na viongozi wa benchi la ufundi 10 na mwenyekiti wa timu hiyo, Mshindo Msolla ambaye ndiye mkuu wa msafara utaondoka leo alfajiri kwenda Mwanza kwa ajili ya mechi yao ya ligi dhidi ya KMC itakayopigwa kesho Jumapili.

 

“Kikosi kinaondoka kesho Jumamosi alfajiri kuelekea jijini Mwanza na wachezaji 27 na benchi la ufundi 10 hii ni kutokana na mapendekezo ya uongozi na benchi la ufundi walivyokubaliana kuwa kikosi chote kiende ili mwalimu apate muda wa kukiangalia kikosi chake.”

Wilbert Molandi, Dares Salaam

Leave A Reply