The House of Favourite Newspapers

Bayo Na Imbori -27

0

Na Boniphace Ngumije

ILIPOISHIA:

Sudan na Gabriel kutoka kundi la kigaidi la Nato wanaona tangazo kwenye televisheni linaloeleza mtu au watu watakaofanikisha kumpata Imbori watazawadiwa dola 40, 000 za Kimarekani, vijana hao walihisi kupagawa kiasi hicho cha pesa kwao kilikuwa ni kikubwa mno na kwa kuwa walikuwa wanafahamu Imbori alipo waliamua kuingia mzigoni.
TAMBAA NAYO…
Baada ya kufika katika Msitu wa Keneth Bull, Sudan na Gabriel walielekea moja kwa moja mpaka sehemu waliyomtelekeza Imbori wakiwa na mategemeo ya kulamba dau nono la dola 40,000 lakini jambo la kushangaza hawakumkuta, walijaribu kumtafuta kila sehemu hawakufanikiwa kumuona.
“Ameenda wapi?” Sudan aliuliza.
“Siwezi kujua.”
“Du!”
Vijana hao wakiendelea kumtafuta Imbori kwa juhudi zao zote katika msitu huo mara walitahamaki baada ya kuliona kundi kubwa la wanyama wakali lililotokea mbele yao.
Kutokana na uoga uliowaingia waligeuka na kuanza kukimbia ili kujiokoa bila kufahamu jambo hilo lilikuwa kosa kubwa mno kutenda wakati kama huo wa hatari.
Lile kundi la wanyama lilianza kuwakimbiza na kufanikiwa kuwakamata, likaanza kuwashambulia bila huruma Sudan na Gabriel wote walipoteza maisha kwa kuliwa kikatili, baada ya wanyama hao kutosheka kula nyama na kufyonza damu waliondoka huku wakiiacha tochi pekee aliyokuwa ameshika Sudan kumsaidia kumulika ikiwaka, habari zao zikawa zimeishia hapo.
* * *
Imbori anaiokota tochi ya Sudan na kuanza kukimbia lakini ghafla alizungukwa na lile kundi la wanyama wakali lililowashambulia Sudan na Gabriel. Imbori alishindwa kukimbia aliishiwa nguvu, akawa anatetemeka tu huku akijua huo ulikuwa mwisho wake.
Kitendo chake cha kusimama kiliwafanya pia wanyama wale wasimame, wakawa wanamtisha kwa kuunguruma kwa milio mikali, jambo alilokuwa analishangaa msichana huyo hakuna hata mnyama mmoja aliyethubutu kumsogelea, akaanza kujiuliza kwa nini waliishia kuunguruma tu baadaye aligundua mwanga wa tochi aliyokuwa ameshika mkononi ulikuwa unamsaidia maana wanyama hao walikuwa wanauogopa.
Hiyo ikawa siri ya ushindi kwa Imbori, bila kufahamu ujasiri aliupata wapi alianza kusogea mbele huku akiwapiga wanyama hao kwa mwanga wa tochi hadi akatoweka katika eneo hilo akiwaacha wakimmezea mate, kutokana na giza kuanza kutanda kila kona ya msitu huo ilimbidi atafute mti aliouona unamfaa akapanda ili apumzike na kuendelea na safari yake siku iliyofuata.
* * *
“Habari za kazi?” Bayo alimsalimia mwanaume mrefu mwenye mwili wa wastani uliotoka kitambi, pia alikuwa amevaa miwani ya macho na mavazi meupe ya kidaktari.
“Nzuri, karibu.”
“Asante, naweza kuonana na Dk. Frank?”
“Unafahamiana naye?”
“Hapana.”
“Una mihadi naye?”
“Sina.”
“Ukimuona unamfahamu?”
“Hapana.”
“Shida yako hasa ni nini?”
“Kuonana naye.”
“Ili?”
“Nina maongezi naye muhimu.”
“Oke, nifuate.”
Bayo alianza kumfuata nyuma mwanaume huyo bila kufahamu ndiye Dk. Frank aliyekuwa anamtafuta, waliongozana hadi wakafika kwenye chumba kilichoandikwa mlangoni Daktari Mkuu, Dk. Frank aliufungua mlango wakaingia ndani.
Baada ya kuketi Dk. Frank alimweleza Bayo kuwa yeye ndiye hasa mtu aliyekuwa anamtafuta, kijana huyo alifurahi sana kukutana naye akaanza kumweleza shida yake iliyompeleka mahali pale.
Alipomaliza kumwelezea daktari huyo alikana kufahamu lolote lile kuhusu msichana na mwanaume waliyewahi kutekwa wakiwa kituoni hapo wala mtoto aliyefia kwenye chumba cha upasuaji miaka takriban mitatu iliyopita zaidi alimjia juu Bayo na kumwambia kama kuna jambo lolote baya alikuwa amepanga kulitenda kwake lingemtokea puani.
Bayo hakuwa na namna yoyote ile ya kulazimisha kuufahamu ukweli maana hakuwa na uhakika juu ya kuhusika kwa daktari huyo katika utekaji wake na mpenzi wake Imbori pamoja na kifo cha kichanga wao, lakini alijiapia moyoni ikiwa kweli alihusika kwa namna yoyote ni lazima siku moja angefahamu na kulipiza kisasi.
* * *
Baada tu ya kuondoka ofisini kwake bila kupoteza muda Dk. Frank alishika simu ya mezani kisha akabonyeza namba za Dickson na kumpa taarifa juu ya ujio wa Bayo.
Taarifa hizo zilizidi kumchanganya Dickson, alijiuliza iliwezekanaje mtu aliyeambiwa alikwishauawa miaka mitatu iliyopita na Kundi la KCK (Kid Can Kill) lakini hakuweza kupata jibu, aliamua kumpa taarifa pia rafiki yake Richard.
Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo.

Leave A Reply