The House of Favourite Newspapers

VIDEO: Biden Kuapishwa Rais wa 46 wa Marekani

0

RAIS Mteule wa Marekani, Joe Biden, ataapishwa leo Januari 20, 2021 na kuwa rais wa 46 wa Marekani akichukua usukani katika nchi ambayo imezongwa na migawanyiko mikubwa ya kisiasa na ambayo inaendelea kuathiriwa zaidi na janga la virusi vya corona.

 

Biden mwenye umri wa miaka 78 atakuwa rais wa Marekani mwenye umri mkubwa zaidi katika historia ya taifa hilo ambapo atakula kiapo cha urais mbele ya Jaji Mkuu wa Marekani, John Roberts, adhuhuri katika majira ya taifa hilo, akishika Biblia ambayo familia ya Biden imekuwa ikiimiliki kwa zaidi ya nusu karne.

Hata hivyo hafla ya kuapishwa kwake itahudhuriwa na idadi ndogo ya watu, yaani waalikwa pekee. Sherehe hiyo mjini Washington haitakuwa na shamrashamra kama za watangulizi wake kufuatia janga la COVID-19 na pia kutokana na hofu za kiusalama baada ya kisa cha wafuasi wa rais anayeondoka, Donald Trump, kuvamia majengo ya bunge (Capitol Hill) mjini Washington Januari 6.

Usalama waimarishwa

Maelfu ya wanajeshi kutoka kikosi cha ulinzi wa taifa nchini humo wamepelekwa katika mji mkuu wa Washington kushika doria na vilevile katika miji mingine kufuatia tahadhari iliyotolewa na idara ya upelelezi ya Marekani (FBI) kuwa kuna mipango ya watu wenye silaha kuandamana wakati wa kuapishwa kwa Biden.

“Tunaenda kushirikiana na kikosi cha ulinzi wa rais na FBI na wengine kuhakikisha tunafanya kila tuwezalo na tukishirikiana kila upande ili rais mteule na makamu wa rais mteule  waapishwe kwa njia salama,” amesema Jonathan Hoffman ambaye ni msemaji mkuu wa Pentagon.

 

Badala ya umati mkubwa wa wafuasi wa Biden kuhudhuria, kutakuwa na takriban bendera 200,000 na minara 56 ya taa kuashiria Wamarekani, majimbo na mamlaka mbalimbali nchini humo.

Sherehe hiyo itafanywa chini ya usalama wa hali ya juu, mahali ambapo wafuasi wa  Trump walivamia majengo ya bunge wiki mbili zilizopita, kufuatia gadhabu zao wakidai uchaguzi ambao Biden alishinda ulikumbwa na udanganyifu. Watu watano walifariki kufuatia vurugu hizo.

Leave A Reply