The House of Favourite Newspapers

Hofu ya kifo! Ulinzi wa Magufuli uimarishwe

0

DK.-MAGUFULI-2Rais Dk. John Pombe Magufuli alipofanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wiki kadhaa zilizopita.

Mwandishi wetu
Hofu ya kifo! Maisha ya Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli yamo hatarini hivyo inabidi ulinzi wake uimarishwe zaidi ya marais waliomtangulia, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin William Mkapa na Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.

Rais-Magufuli-9Rais Magufuli akimjulia hali mgonjwa.

Kauli hiyo imetolewa kwa nyakati tofauti na wananchi waliohojiwa na gazeti hili katika miji mbalimbali nchini baada ya kazi yake ya kutumbua majibu inayoendelea hivi sasa kuzidi kushika kasi.

UCHUNGUZI
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ulibaini kwamba, kazi ya kupambana na ufisadi uliokithiri nchini, maarufu kama ‘kutumbua majipu’ aliyoianzisha Rais Magufuli, pamoja na kumfanya apendwe na wananchi wa kawaida, inamuongezea idadi kubwa ya maadui kwa kugusa masilahi ya wakubwa na wenye nguvu na ushawishi.

mg1Rais Magufuli alipofanya ziara ya kushtukiza Wizara ya Fedha.

“Huyu ndiye rais tuliyekuwa tunamtaka, cha msingi aongezewe ulinzi kumnusuru na kifo maana mafisadi wanaweza kutumia nguvu ya pesa kufanya lolote,” alisema Shaban Nundu, mkazi wa Uyole, Mbeya.

Naye Innocent Kweka wa Moshi, Kilimanjaro alisema: “Kila mwenye nia njema na nchi yetu amuombee Magufuli kwa Mungu atumbue majipu bila woga. Watanzania tumeteseka kwa sababu ya ufisadi wa watu wachache.”

MAGUFULI ANAKATA MSHIPA
Akihojiwa na Runinga ya Channel Ten, Desemba 3, mwaka huu (juzi), mchambuzi maarufu wa mambo ya kisiasa nchini, Humprey Polepole alisema:
“Anachokifanya Rais Magufuli hivi sasa ni kama kukata mshipa wa damu wa mtu, hivyo ili mtu huyo asife huona ni bora akate mshipa wako wewe.”

Kauli hiyo imethibitisha ambacho wananachi wamekuwa wakiongea kuwa maisha ya Rais Magufuli yapo hatarini na inabidi aongezewe ulinzi.

Akitangaza vita hiyo bungeni mjini Dodoma, Novemba 20, mwaka huu alipotoa hotuba yake ya kwanza, rais aliomba Watanzania wamuombee
kwani kazi aliyoianzisha ni ngumu na ingesababisha maumivu kwa watu wengi.

Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli ameonesha uwezo mkubwa wa kushughulikia kero za wananchi wa Tanzania na kupunguza matumizi ya fedha za umma na zilizookolewa alizielekeza katika kuondoa kero na ameyafanya yote hayo bila Baraza la Mawaziri.

DUNIA YAMZUNGUMZIA
Dunia nzima imekuwa ikizungumzia utendaji wake huku baadhi ya vyombo vya habari nchini Uingereza na China vikiandika juu ya utendaji wake mzuri.

NCHI KENYA
Nchini Kenya wananchi wa nchi hiyo kwa mara ya kwanza katika historia wametamani kuwa na rais wa kariba ya Dk. Magufuli.

Kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, baadhi ya watu wamekiri kabisa kuwa Rais Magufuli ‘amemfunika’ Rais wa Rwanda, Paul Kagame anayejulikana kwa kuchapa kazi na akiendelea hivyo, hasa kwa utajiri mkubwa wa gesi ambao Tanzania inao, lazima itanyanyua sana uchumi wake ambao hivi sasa unakuwa kwa kasi ya asilimia 7.9%.

TAASISI ZILIZOONJA
JOTO YA JIWE
Taasisi ambazo mpaka sasa zimeonja joto ya jiwe tangu Dk. Magufuli aingie madarakani ni pamoja na Mamlaka ya Bandari Dar (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wizara ya Fedha (Hazina) na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii (Muhimbili) huku maeneo mengine yakisubiria matumbo yakiwa joto.

Leave A Reply