The House of Favourite Newspapers

Kenya: Rais Ruto Amuonya Odinga Dhidi ya Maandamano ya Umma

0
Rais wa Kenya William Ruto

Rais wa Kenya William Ruto amemuonya kiongozi mkuu wa upinzani Raila Odinga dhidi ya kufanya maandamano ya umma yaliyopangwa na muungano wa upinzani wa Azimio Jumatatu ijayo 20,Machi,2023.

Rais Ruto amesema hatamruhusu Bwana Odinga kufanya maandamano yatakayohatarisha maisha ya Wakenya,uharibifu wa mali au kulemaza shughuli za biashara nchini akiongeza kuwa Kenya ni nchi inayoongozwa kwa misingi ya sheria na hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria hizo.

Mapema wiki hii,  Odinga alitangaza kuwa tarehe 20 Machi itakuwa siku ya mapumziko Kenya ili kuruhusu raia kushiriki maandamano ya kupinga utawala wa Rais Ruto na kuongezeka kwa gharama ya maisha nchini humo.

Kiongozi mkuu wa upinzani, Raila Odinga

Waziri kiongozi Musalia Mudavadi hata hivyo amekosoa tangazo hilo la Odinga akilitaja linalokiuka katiba ya nchi kwani hana mamlaka ya kutangaza siku ya kitaifa wala ya mapumziko

Kiongozi huyo wa upinzani ameendelea kusisitiza hatambui uongozi wa Bwana Ruto tangu alipotangazwa mshindi wa uchaguzi wa Rais uliofanyika Agosti mwaka jana,akidai kulikuwa na udanganyifu wa kura na kutaka Tume huru ya uchaguzi kutathminiwa upya licha ya mahakama ya juu kuthibitisha ushindi wa Bwana Ruto.

Tayari,kaunti kadhaa nchini Kenya katika kipindi cha siku chache zilizopita,zimeshuhudia maandamano ya umma kuitikia wito wa Bwana Odinga kwa wananchi kuipinga serikali. Miongoni mwa kaunti hizo ni Migori na Kisumu ambazo ni ngome za kisiasa za kiongozi huyo mkuu wa upinzani.

Viongozi wa muungano wa Azimio wakiongozwa na kinara wao wamekuwa wakifanya msururu wa mikutano ya hadhara kote nchini katika wiki chache zilizopita kuwashawishi wafuasi wao kugoma na kuipinga serikali kwa kile wanachokitaja kushindwa kushughulikia masuala muhimu yanayowaathiri Wakenya kama ugumu wa Maisha,kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu,ajira na ufisadi.

BOSI wa MASHA LOVE ALIYEMPELEKA UTURUKI KUFANYIWA OPARESHENI – ”MAZIWA YANAMPA KULA”…

Leave A Reply