The House of Favourite Newspapers

Mume, Wewe Ndiye Sumu Ya Mkeo

0

Asalam alaikum wapenzi wasomaji wa safu hii, kwa upande wangu Shangingi Mstaafu, naendelea vema, namshukuru Mungu.

Leo nimekuja na mada hii maalum kwa ajili ya wanaume, hasa waliooa ambao pengine kwa sababu za mazoea, wanaamini kuwatolea lugha ya ukali, au maneno mabaya wake zao ni kuwafunza.
Wanafanya hivi wakiwa hawajui kama ni dosari kubwa inayosababisha upendo ndani ya nyumba kupungua kama siyo kwisha kabisa.
Wanaume wengi wanahisi upendo unatakiwa kuoneshwa na mwanamke tu, kwa sababu wao ni mwanaume, basi upendo hauwahusu. Wanasahau jambo hili ni la wote wawili kuonesha na kuliweka katika uhalisia wake.

Kikubwa kilichosababisha nikaandika mada hii ni ujumbe niliotumiwa na mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la mama Khadija. Alidai mumewe humjibu vibaya hata pale asipostahili.

“Siku moja alikuwa akiumwa, nikamwuliza umekunywa dawa mume wangu? akasema hajanywa na kumalizia kwa kuniambia wewe nikinywa dawa au nisipokunywa, inakuhusu nini?” alisema mama Khadija.
Mama huyo alisema kuwa huo ni mfano tu, kwani ameshajibiwa vibaya mara nyingi na mambo mengine ambayo hawezi kuyaanika, kwani ni mambo ambayo hakuyatarajia na wakati mwingine, humtaka anyamaze, asiongee pale anapohoji jambo f’lani.
Kwa sababu hiyo, nimeamua kuandika haya ili kuwaweka sawa wanaume wenye tabia hii na kuwaeleza kuwa hakuna mwanamke anayeongea na mumewe kwa lengo la kumuudhi, bali mara nyingi hufanya hivyo kwa lengo la kujenga upendo ndani ya familia.

Kama mume anahisi jambo analoelezwa na mkewe halipendi ni bora kunyamaza kuliko kumropokea maneno mabaya, maana ubongo huwa haufuti jambo baya. Kufanya hivyo kila mara huiweka akili ya mwanamke katika hali ya kuchoka taratibu.
Inafikia wakati mwanamke anamwambia mumewe kuwa amechoka na hivyo anataka waachane. Inapokuwa hivi, wanaume hupeleka mawazo yao katika kuamini kuwa wake zao wamepata wanaume wengine, kitu ambacho siyo kweli, kwani chanzo hasa huwa ni tabia ya maneno ‘ya shombo’ anayoyatoa mumewe kwake.

Kwa kuwa wanaume mmepewa roho ya uvumilivu hebu wavumilieni wake zenu na kuacha tabia ya kuwatolea lugha isiyofaa. Msipoacha tabia hiyo
watachoka na kuamua kuondoka huku mkiwa bado mnawapenda.
Wabembelezeni wake zenu kwa kauli nzuri ili mdumishe ndoa zenu! Tuonane wiki ijayo kwa mada mpya.

Leave A Reply