The House of Favourite Newspapers

Mkuki moyoni mwangu – 62

1

ILIPOISHIA…
BAADA ya Dracula kutoa ushahidi wote, yeye, Dragon na washirika wao wote ambao walihusika kuua watu wengi kwa matakwa ya bosi wao Jackson Motown, wanahukumiwa kufa kwa kudungwa sindano.
Wanafurahia kwa sababu wanaamini wanastahili kifo cha namna hiyo.

Upande wa pili, baada ya Kevin kujua ukweli wa Catarina, anaamua kumtafuta ili apate japo mifupa tu ya mpenzi wake huyo ili roho yake isuuzike. Kwa mujibu wa ushahidi wa Dracula, Catarina ametupwa kwenye mbuga ya wanyama ya American National Park iliyokuwa na wanyama wakali wengi sana. Lengo la kina Dracula waliomtupa mbugani humo wakiwa wamemuwekea dawa ya usingizi ni ili aliwe na wanyama hao.Je, Catarina amekufa? Je, Kevin anayekwenda kumfuatilia naye atajikuta akiliwa na simba? SONGA NAYO…

JAMAL Abdelkadri alikuwa ni raia wa Pakistan aliyezaliwa nchini Marekani, wazazi wake walikimbilia nchini humo kukimbia hali mbaya ya usalama wakati wa machafuko yaliyosababisha idadi kubwa ya watu kupoteza uhai, waliingia Florida wakitokea Uingereza na kuhamia New York miaka miwili baadaye ambako Jamal alizaliwa.

Akakulia katika jiji hilo ambako baba yake aliendesha teksi na mama yake akifanya kazi za kusafisha nyumba za watu mwisho wa wiki, zilikuwa ni kazi ngumu sana lakini walizifanya kwa sababu walitaka mtoto wao apate elimu bora ambayo ingekuja kuwabadilishia maisha mara akishapata kazi nzuri nchini humo.

Tangu utotoni mwake Jamal alionyesha kipaji kikubwa sana katika mambo ya Sayansi, wazazi wake wakaamua kumsaidia asome masomo hayo akiwa shule ya sekondari na baadaye kuingia Chuo Kikuu cha Manhattan kuchukua shahada ya kwanza ya udaktari wa binadamu, ndoto ya Jamal ikaelekea kutimia.

Akiwa mwaka wa pili katika chuo hicho alikutana na msichana mrembo mwenye asili ya Columbia, muonekano kama wa mwanamuziki Shakira, jina lake akiitwa Vivian, wawili hao bila kutarajia wakajikuta wakivutana mioyo yao na kuwa wapenzi, kila mmoja akavunja bikra ya mwenzake kwani hawakuwahi kukutana na binadamu kimwili kabla ya siku walipokutana kimwili kwa mara ya kwanza.

Ahadi yao ikawa ni kufunga ndoa mara tu wakimaliza masomo ya chuo kikuu na kuwa madaktari, mwezi mmoja kabla ya sherehe yao ya kuvishana pete ya uchumba, waliamua kwenda Afrika kutembelea Mbuga ya Wanyama ya Serengeti iliyopo nchini Tanzania pamoja na Mlima Kilimanjaro.

Ilikuwa ni safari ya kihistoria katika maisha yao ya uhusiano, kila mmoja alikuwa amefurahi mno, wakashuka Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) na kusafiri kwa gari la kukodi mpaka mjini Arusha ambako kampuni iliyojihusisha na shughuli za kuhudumia watalii ya Chocks Tours, chini ya Mkurugenzi wake Chocks Chokala ilichukua jukumu la kuwatembeza mbugani.

Kwa gari aina ya Land Cruiser lililotengenezwa vizuri kuhimili mabonde, waliondoka Arusha saa kumi na mbili asubuhi, Mkurugenzi Chokala mwenyewe ndiye akiliendesha gari hilo, kwenye lango la kuingilia mbugani, walifuata taratibu zote na kupewa mtu wa kuongozana naye mbugani, aliitwa James Ole Medei, kijana wa Kimasai aliyesomea mambo ya wanyamapori na kufanya kazi mbuga ya Serengeti kwa miaka zaidi ya kumi, alifahamu kila mahali walikopatikana wanyama mbalimbali.

Jamal na Vivian walifurahia kila kitu walichokiona, wakipiga picha karibu kila kitu kizuri kuanzia wanyama kama vifaru, tembo, simba, pundamilia na wengineo wengi, wakiwa safarini mara ghafla Vivian aliwaona Twiga wazuri kando ya njia, akaamuru gari lisimamishwe, alipenda Twiga kuliko wanyama wengine wote wa porini.

“Simama! Simama! Simama! Jamal unipige picha moja wakiwa nyuma yangu, nashuka harakaharaka, si kuna usalama hapa?”
“Siyo salama sana lakini, usiende mbali, simama tu hapo kando ya gari!”
“Sawa!” alijibu Vivian akishuka haraka kwenye gari, Jamal akiwa ameweka kamera yake vizuri.
“Tabasamu!” Jamal alisema Vivian akiweka pozi, nyuma yake wakiwepo twiga wawili.

Picha ilipopigwa haikuwa ya Vivian akiwa ameweka pozi na tabasamu bali ya chui akimrukia na kumwangusha chini, kumbe kwenye kichaka cha jirani alikuwepo chui aliyekuwa amejificha, meno yake akayazamisha shingoni! Wakati askari wa wanyamapori anapiga risasi kumuua chui, tayari Vivian alishaanza kukata roho, damu nyingi ikimtoka shingoni.

Huo ndiyo ukawa mwisho wa Vivian, Jamal alilia mno, picha aliyoipiga ilimtesa mno kila alipoiangalia, mwili wa Vivian ukasafirishwa na kwenda kuzikwa Manhattan, New York kwenye msiba uliowasikitisha watu wengi sana. Jamal akawa kama amechanganyikiwa, hakutaka tena kuendelea na masomo ya udaktari, akili yake yote ikamtuma kusoma mambo ya wanyamapori ili mwisho wa siku afanye kazi kwenye mbuga kuzuia ajali kama iliyompata mpenzi wake.

Hakutaka kuoa tena wala kuwa na mpenzi, kufanya hivyo kwake ingekuwa ni usaliti mkubwa kwa Vivian! Alimaliza masomo yake kwenye Chuo cha Wanyamapori cha Houston na kupata Shahada ya Wanyamapori miaka mitatu baadaye bila kuwa na uhusiano wa kimwili na mwanamke yeyote, akili yake yote ilikuwa imeishia kwa wanyama.

Ajira yake ya kwanza ikawa kwenye mbuga ya American National Park ambako kazi yake ilikuwa ni kuzunguka msituni kuangalia usalama wa wanyama akiwa na bunduki yake, hakuyaamini macho yake alipomwona mwanamke mrembo akikimbia katikati ya mbuga, nyuma yake akikimbizwa na simba, alichokifanya ni kunyanyua bunduki yake na kumlenga Simba yule, akaanguka chini kama mzigo, Jamal akashuka kwenye gari na kumsogelea msichana yule ambaye urembo wake ulimshangaza.

“What are you doing here?” (Unafanya nini hapa?)
“Someone wants to kill me, I don’t know how I got here!”(Kuna mtu anataka kuniua, sijui nimefikaje hapa!)

“Oh my God!” (Oh Mungu wangu!) Jamal aliongea kwa mshangao.
“Thank you! Thank you! A million times!”(Ahsante! Ahsante! Mara milioni moja!)
“What’s your name?”(Jina lako nani?)
“Catarina!”
“Who wants to kill you?”(Nani anataka kukuua?)
“Jackson Motown!”
“The rich guy?” (Yule tajiri?)
“Yeah!”(ndiyo!)

“Why?” (Kwa nini?)
“I used to be a super model, he raped me and so to keep that evil secret he wants to shut my mouth!”(Huko nyuma nilikuwa mwanamitindo, akanibaka na ili kuificha hiyo siri yake mbaya, anataka kuninyamazisha!)

“I will keep you in my house until your safety is guaranteed!” (Nitakutunza ndani ya nyumba yangu mpaka usalama wako utakapokuwa wa uhakika!)
“Thank you! What is your name” (Ahsante! Jina lako nani?)
“Jamal!”

“Thank you Jamal, I can’t thank you enough!”(Ahsante Jamal, sina shukurani za kutosha!)
“You are welcome!” (Karibu!)
Akamsaidia kupanda ndani ya gari lake na kuliendesha mpaka kwenye nyumba yake iliyokuwa pembeni kabisa na nyumba za wafanyakazi wenzake, kwa sababu ya giza lililokuwepo wakati anafika, hakuna mtu yeyote aliyemwona Catarina wakati anaingia ndani ya nyumba yake, akamkaribisha kwenye chumba cha wageni na kumpa kila kitu alichohitaji wakati wa kuoga.

“For what Jamal has done to me, he can be a late Kevin’s replacement in my heart!” (kwa alichonifanyia Jamal anaweza kuziba pengo la marehemu Kevin moyoni mwangu!) aliwaza Catarina wakati akioga.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Jumatano katika Gazeti la Championi Jumatano.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

1 Comment
  1. Aman Norbety says

    Wewe Catarina ww! Acha kubadilisha mawazo, Kelvin anakusubiri bwana. Actually God is Good

Leave A Reply