The House of Favourite Newspapers

U.T.I; gonjwa linalosumbua wanawake -4

0

utiTIBA YA U.T.I NA USHAURI
Baada ya kuuchambua ugonjwa wa U.T. I (Urinary Tract Infection ) leo tunazungumzia tiba yake. Maambukizi katika njia ya mkojo hutibika kwa dawa mbalimbali za kisasa baada ya kufanyiwa vipimo na kuthibitika kuwa mgonjwa ana maambukizi hayo.

Dawa ambazo anaweza kupewa mgonjwa ni kama vile Ciprofloxacin, Monurol, Furadantin, Sulfam Ethoxazole, Co-trimax, Ampicillin, Gentamicin na kadhalika. Mgonjwa anayesumbuliwa na U.T.I hapaswi kutumia dawa yoyote bila kwanza kupata ushauri wa daktari.

Wanawake wanashauriwa kuepuka kujisafisha sehemu za siri na maji machafu na yasiyo salama, pia kuepuka kupaka marashi sehemu hizo, ama kutumia pamba zenye kemikali ya kukata harufu kwani hizo huua bakteria wa asili wa sehemu za siri hali ambayo hukaribisha bakteria wa maradhi kuzaliana kwa wingi.

Pia wanashauriwa wanapojisafisha baada ya kujisaidia kuanzia mbele kwenda nyuma ili kuepusha kuhamisha bakteria walio eneo la haja kubwa na kuingia njia ya mkojo.
Kwa wale walio katika kipindi cha ukomo wa hedhi, wanaweza kushauriana na daktari juu ya kutumia Oestrogen ya ukeni ili kuwasaidia kujikinga na maambukizi ya U.T.I.

Kwa mwanaume maambukizi haya huathiri nguvu za kiume na kujipenyeza hadi katika korodani na huathiri uzalishaji wa mbegu za kiume na kunaweza hata kusababisha ugumba. Hivyo wanashauriwa kuhakikisha wanatibu bila kuchelewa ugonjwa huo.

Pia maambukizi ya njia ya mkojo huweza kusababisha matatizo ya tezi ya kiume (prostate) kwani husababisha mrija wa mkojo kuziba, kutopitisha mkojo vizuri na kuruhusu bakteria kujenga makazi.
Hali hiyo ikitokea mgonjwa lazima akamuone daktari ili awekewe mrija wa kutolea mkojo.

Tunaweza kuudhibiti au kuponya ugonjwa huu kwa kunywa maji mengi pamoja na juisi itokanayo na matunda halisi, iwapo tutawahi kabla tatizo halijawa sugu. Kwa maana nyingine, unaweza kujikinga na ugonjwa huu kwa kuwa na mazoea ya kunywa maji ya kutosha kila siku.

Ukinywa maji ya kutosha yatakufanya uende haja ndogo kila mara na kwa njia hiyo wale bakteria watakuwa wakitoka na hatimaye kuisha kabisa.

Hivyo basi ukijisikia unaumwa tumbo chini ya kitovu, joto au maumivu wakati wa kukojoa mkojo kuwa na rangi ya njano kupindukia na kuwa na harufu kali, kutokwa na usaha wakati wa kukojoa, kabla au baada ya kukojoa, kutokwa na majimaji katika njia ya mkojo wakati wa kujisaidia haja kubwa,vichomi katika njia ya mkojo, au kuhisi kuwashwa sehemu hiyo, kuumwa kiuno, homa kali na kadhalika, nenda kamuone daktari.

Leave A Reply