The House of Favourite Newspapers

Unaposhindwa kuishi vizuri na watu, unajiamini kwa lipi?

0

Wakati f’lani nikiwa natoka kijijini kuja Dar, wazazi wangu waliniusia juu ya kuishi vizuri na watu. Waliniambia kuwa, watu nitakaokutana nao niwachukulie kama ndugu zangu. Niishi nao vizuri na kuwaheshimu kwani ndiyo wa kunisaidia pale yatakaponikuta mazito. Nakumbuka hata Bendi ya DDC Mlimani Park (Sikinde) iliwahi kutunga wimbo uliokuwa unahimiza watu kuishi vizuri na walimwengu.
Faida za wosio huo nilikuja kuziona mwaka 2000, nakumbuka nilikuwa naumwa sana. Pesa niliyokuwa nayo nilikuwa nimeitumia kwenye matibabu, nikabaki mtupu! Wakati huo sikuwa na simu hivyo ikawa ngumu sana kuwasiliana na ndugu zangu.

Mungu si Athumani, mmoja wa majirani zangu akaja kuniona chumbani kwangu, nikamweleza ukweli wa mambo. Huyo ndiye aliyenikoa na hapo ndipo nikathibitisha faida za kuishi vizuri na watu.
Ndugu zangu, Wazungu wana msemo wao unaosema, ‘Life is unpredictable’ yaani maisha hayatabiriki. Huo ndiyo ukweli wenyewe. Wapo ambao walikuwa na hali nzuri sana kifedha huko nyuma lakini leo hii ukiwaona huwezi kuamini.
Wanaishi maisha magumu sana tena kwa msaada wa watu wengine. Hayo ndiyo maisha! Ndiyo maana unaambiwa kuwa, leo hii ukiwa juu usijipe asilimia mia moja kwamba siku zote utakuwa juu. Upo uwezekano mkubwa wa siku moja kuwa chini na waliokuwa chini wakapanda.

Kwa mantiki hiyo basi tunapoli zungumzia suala la kuishiwa linamgusa kila mtu bila kujali tajiri wala maskini. Kimsingi kuishiwa ni hali ya kukosa pesa kwa ajili ya matumizi yetu ya kila siku.
Hali hii ni ya kawaida katika maisha ya binadamu. Hii inamaanisha kwamba unaweza ukawa unafanya kazi na kuwa na kipato kizuri tu, lakini katika mazingira fulani ukajikuta pesa ambayo ulikuwa nayo imekwisha.
Yawezekana ukawa umepata matatizo yanayohitaji fedha nyingi ukazitumia katika kutatulia matatizo hayo au unaweza kujikuta umeishiwa baada ya mshahara kuchelewa na ukajikuta huna kitu kabisa.

Wakati huohuo unahitaji chakula, matibabu, usafiri na mahitaji mengine ya msingi yanayohitaji pesa. Ufanyeje sasa ili uweze kuendelea kuishi? Katika kukabiliana na tatizo kama hili hapo ndipo umuhimu wa suala la kuishi vizuri na watu linapoonekana.
Nasema hivyo kwa sababu, katika mazingira hayo hakuna njia nyingine zaidi ya kuomba msaada kutoka kwa watu walio karibu yako. Sasa kama uhusiano wako na watu wanaokuzunguka siyo mzuri unatarajia nani atakusaidia?
Kwa ufupi hakuna na kama atajitokeza msamaria mwema wa kukusaidia basi atakuwa ni mtu ambaye hakufahamu tabia zako na uhusiano wako na watu kwa ujumla.
itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply