The House of Favourite Newspapers

Utundu ulimfanya asiingie kwenye uhusiano wa kimapenzi

0

WIKI iliyopita nilishia pale ambapo Mkwere alipokuwa akisisitiza kila msomaji kujichunguza na kujiuliza nini anapaswa akifanye kwa kutumia kipaji chake halisi na si kwa kipaji cha kukurupuka
Sasa songa naye …mkwere

Hemedi Khalifan Maliyaga ‘Mkwere’


Nilikwambia kama ukifanya kitu kwa kukurupuka basi subiri kushindwa katikati ya safari yako. Kiukweli nikiwa bado shule ya msingi kuna mambo mengi sana nilikuwa nakutana nayo kama mwanafunzi mtundu na kutokana na utundu wangu nilikuwa  napewa adhabu ya kupiga magoti na kubebeshwa mawe wakati huo kosa lenyewe unakuta sijavaa soksi na makosa mengine.
“Moja ya matukio ambayo siwezi kuyasahau kipindi niko shule (msingi), nilikuwa mwizi sana wa mafagio pamoja na magaloni ya wanafunzi wenzangu na hii ni kwa sababu nilikuwa nakaa nyumba ya shule ambayo ilikuwa imetenganishwa na ukuta tu. Nilichokuwa nakifanya, ukifika muda wa mapumziko wakati wanafunzi wenzangu wanaenda kununua visheti, bagia, vitumbua na kadhalika basi mimi nilibaki na kuanza kuiba magaloni na mafagio kwa kuirusha juu ya ukuta na kudondokea uani kwetu.

“Niliendelea na tabia ile kwa muda mrefu kidogo, kwa kuwa za mwizi ni arobaini siku moja nilikamatwa na kubainika kutokana na madumu kuwa na majina ya wanafunzi husika. Nilisemwa kwa mwalimu wa darasa, nikachapwa na kupewa kazi ya kuyalinda magaloni na mifagio yote muda wa mapumziko yaani ni sawa na ule msemo wa mchawi mpe mwanao akulelee.
“Tangu siku hiyo nikawa siaminiwi tena shuleni, kwa hiyo wakati wa mapumziko wenzangu wanaenda kununua kashata, bagia na  visheti wakisharudi ndipo sasa na mimi naruhusiwa kutoka, kwa mazingira hayo nikajikuta naachana na tabia hiyo.

“Kwa upande wangu masomo, somo la hisabati lilikuwa ni kama janga la taifa, kiukweli sikuwa naelewa chochote katika somo hilo ila masomo ya jiografia, siasa na sanaa nilikuwa niko vizuri na hata kuyaelewa niliya-elewa. Pamoja na hesabu kusumbua darasani lakini sikuwahi kuwa wa mwi-sho wala wa kwanza katika matokeo ya mitihani yangu.
“Hata hivyo, pamoja na utundu wangu wote sikuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi wakati niko shuleni kuanzia chekechea mpaka kidato cha nne, zaidi ya kuwa mtundu tu na mcheshi sana. Ila kitu cha ajabu kutokana na utundu niliokuwa nao, nilikuja kupewa kazi ya ukilanja wa darasa, kiukweli ilinifanya kuwa mwanzilishi wa fujo na kelele.”
Mkwere anaendelea kusimulia kuwa baba yake ndiye aliyeanza kufariki dunia hiyo ilikuwa mwaka 1988 ambapo alimuacha akiwa na umri wa miaka nane.

“Hali ile ilinitia unyonge sana, hilo lilipita na maisha yakaendela ila mwaka uliofuatia tena mama yangu mzazi naye akatangulia mbele ya haki, duh! Kiukweli nikaona dunia chungu sana, kwani niliwapenda na nilitamani niwe na wazazi wangu
ili wale matunda ya malezi yao ila kwa kuwa kazi ya Mungu haina makosa basi nashukuru kwa kila jambo, nazidi kuwaombea Mwenyezi Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi,” anasema Mkwere.

Mkwere anaendelea kusimulia kuwa ilimchukua muda mrefu kukubaliana na ile hali ya kuondokewa na wazazi wake pengine ni kwa sababu ya utoto aliokuwa nao.

“Basi baada ya msiba kuisha nikachukuliwa na kaka zangu walionilea pamoja na baba yangu mdogo, Richard Rafael ambaye alishafariki dunia pia. Ngoja nikupe siri moja, ujue ukoo wetu tumecha-nganyika kuna Wakristo na Waislamu ndiyo maana baba mdogo ana majina ya Kikristo.
Simulizi hii ndiyo kwanza imeanza, kumjua zaidi Mkwere usikose kumsoma Alhamisi ijayo…

Leave A Reply