The House of Favourite Newspapers

Achomwa kisu akimtetea mkewe!

0

Chande Abdallah na Gabriel Ng’osha

Inasikitisha! Kijana aliyefahamika kwa jina la Khalid Abdallah (30) mkazi wa Kigogo Sambusa jijini Dar, amefariki dunia kwa kuchomwa kisu na mtu aliyefahamika kwa jina la Amani huku mkewe aitwaye Aisha akishuhudia.

Marehemu Khalid Abdallah enzi za uhai wake.

Tukio hilo lilitokea hivi karibuni saa 5 usiku maeneo ya kota za Karume jijini Dar ambapo inadaiwa Khalid alikuwa katika jitihada za kumtetea mkewe asidhuriwe na kijana huyo.

DADA ASIMULIA

Dada wa marehemu aliyefahamika kwa jina la Bahati alisema kuwa siku ya tukio akiwa nyumbani kwake alipigiwa simu na kijana mmoja na kuambiwa kuwa ndugu yake amechomwa kisu na tayari alikuwa amepelekwa Hospitali ya Amana.

“Nilielezwa kuwa mdogo wangu Khalid kachomwa kisu na amepelekwa Amana, ndiyo ikabidi niagize marafiki zake wafuatilie, wakakuta kweli ni yeye,” alisema Bahati huku akilia.

MSIKIE MKE

Mwandishi wetu akiongea na dada wa marehemu.

“Tulikuwa tunatoka kwenye matembezi yetu lakini tukiwa njiani tulikutana na kijana mmoja anayeitwa Amani, baada ya kumpita mita chache, aligeuka na kumfuata Khalid kisha kumuuliza kwa nini alimpita bila kumsalimia ndipo mume wangu akamwomba samahani.

“Wakati akijaribu kumzuia asinidhuru, yule kijana akamgeukia na kumwambia atoe kila kitu alichokuwa nacho, ndipo akachukua simu na shilingi 33,500 kisha akachomoa kisu kiunoni na kumchoma tumboni.
“Baada ya kuona mume wangu anaanguka chini nikajua amekufa, nikakimbia huku nikipiga kelele, tulisaidiwa na watu lakini hata hivyo hatukuweza kuokoa uhai wake,’’ alidai Aisha.

Waombolezaji wakiwa msibani.

Watu mbalimbali waliokuwa eneo la tukio walisema kuwa, baada ya mwanamke huyo kupiga kelele umati wa watu ulifika na kumchukua Khalidi hadi Kituo Kidogo Cha Polisi Pangani kwa ajili ya kupewa fomu ya matibabu ‘PF3’ kisha akapelekwa Hospitali ya Amana alikofariki dunia.

MTUHUMIWA MBARONI

Kwa mujibu wa chanzo chetu, vijana wawili wametiwa mbaroni kutokana na tukio hilo mmoja wao akiwa ni Amani na sheria inafuata mkono wake.Mwili wa marehemu Khalid ulizikwa Septemba 28, mwaka huu Maili Moja, Kibaha mkoani Pwani.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

Leave A Reply