The House of Favourite Newspapers

Maadui wa JPM Watikisa Morogoro RPC Awafungia Kazi

 

WAKATI Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli ‘JPM’ ikipambana kwa kasi kubwa kuweka miundombinu kote nchini, baadhi ya ‘maadui’ wamejitokeza na kuhujumu miundombinu hiyo.

 

Maadui hao wa mipango ya JPM walijitokeza mwishoni mwa wiki iliyopita mjini hapa na kuiba taa tano za sola zilizowekwa kwenye Barabara ya Kola inayoelekea Nane-Nane mjini hapa.

Kwa mujibu wa mashuhuda wanaotumia barabara hiyo, awali, usiku wa kuamkia ljumaa iliyopita, watu hao waliangusha nguzo na kuiba taa hizo eneo la Makaburi ya Kola kisha kutimka nazo kusikojulikana.

 

Ilielezwa kuwa, siku iliyofuata wananchi waliokuwa wakipita eneo hilo la makaburi walisikitishwa mno na kitendo hicho huku wakiwalaani waliotekeleza uhalifu huo.

“Baadhi yetu sisi Waswahili hatujaelimika na hatujui umuhimu wa vitu kama hivi.

“Zamani ilikuwa ukipita hapa saa 1:00 usiku unakabwa, lakini tangu barabara hii itengenezwe miezi mitatu iliyopita na kuwekwa taa hizi, tunapita hata saa 5:00 usiku kukiwa na mwanga kama mchana.

 

“Pia kuna baadhi ya ndugu zetu wanaishi mikoa mingine, ikitokea wamekufa na kusafirishwa kuzikwa hapa, mara nyingine huwa wanafika jioni tunalazimika kuwazika usiku na taa hizi zinatusaidia sana, sasa kwa kuwa eneo hili la makaburi hakuna nyumba za watu, watu hao wameiba taa zote tano,” alisema Sharrif ambaye ni mtumiaji wa barabara hiyo.

 

Naye Asha Dimoso aliyekuwa eneo la tukio alisema:

“Mimi kama Mtanzania, nina uchungu sana kwani najua taa hizi ni kodi zetu, sasa niombe kwa umoja wetu tushirikiane kuwafichua hawa wahujumu uchumi wa taifa letu kwani Rais wetu anafanya kazi kubwa kututengenezea miundombinu, lakini watu wengine wasio na akili wanahujumu.”

Baada ya taa hizo kuibwa, Jeshi la Polisi mkoani Morogoro kwa kushirikiana na TARURA (Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini) siku iliyofuata waliweka ulinzi kabambe kwenye mitaa yote yenye barabara hizo mpya zenye taa.

 

Hata hivyo, siku hiyohiyo usiku, watu hao walirudi kwa lengo la kuiba taa nyingine ambapo walikamatwa.

Baada ya kupata taarifa za kukamatwa kwa watu hao, juzi Jumamosi, mwanahabari wetu alitinga Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Wilbrold Mutafungwa ambapo kamanda huyo alithibitisha kukamatwa kwa watu hao.

“Ni kweli tunawashikilia watu wanne baada ya kuwakamata usiku wa saa 9:00 wakiiba taa za barabarani eneo la Nane- Nane kuelekea Makaburi ya Kola.

 

“Watu hao ambao kwa sasa sitawataja kwa sababu za kipelelezi, walifika eneo hilo wakiwa na gari aina ya Toyota Hiace ambalo pia sitalitaja namba zake.

“Askari wetu walikuwa doria za kawaida kwenye mitaa yetu ya Mji wa Morogoro na kuwakamata watu hao wakiiba taa hizo.

“Niombe wananchi tushirikiane kulinda miundombinu yetu na ukimtilia shaka mtu yeyote, toa taarifa kwa Jeshi la Polisi,” alisema Kamanda Mutafungwa.

STORI: DUNSTAN SHEKIDELE, MORO

Comments are closed.