The House of Favourite Newspapers

AIBU YA MWAKA! Mchungaji Afumaniwa Kanisani! – Video

MCHUNGAJI wa Kanisa la Gospel Revival Assemblies of God lililopo Mlandizi, Julius Andrew mkazi wa Mlandizi, amekumbwa na aibu nzito baada ya kufanya jaribio la kumtosa mkewe, Maria Stoni na kwenda kuoa mke mwingine kwa siri.  

 

Lakini wakati mchunga kondoo huyo wa bwana akiwa katika jaribio hilo, mkewe alipata taarifa za kiitelijensia na kuvamia kwenye kanisa alilotaka kufungia ndoa hiyo.

 

Shughuli ya ndoa hiyo iliyotibuliwa na Maria, ilikuwa ifungwe katika Kanisa la Gospel Revival Assemblies of God, Mbagala Kuu – Tawi la Vianzi, Vikindu, wilayani Mkuranga, mkoani Pwani. Hata hivyo, awali ratiba iliyonyakwa na Maria ilionyesha kuwa ndoa hiyo ilikuwa ifungwe katika kanisa hilo, tawi lake la Mbagala Kuu, lakini baadaye mchungaji baada ya kuchezwa na machale akaamua kubadili kanisa.

HABARI MEZANI

Awali, chanzo chetu ambacho kilikuwa miongoni mwa kampani ya mke wa mchungaji, kilitutonya uwepo wa tukio hilo, hivyo tuungane nao ili kuchukua tukio hilo laivu bila chenga. Paparazi wa Uwazi, hakufanya kosa, alidandia bodaboda yake fasta baada ya kuweka mipango yote ya namna ya kukutana, kisha akafunga safari hadi Mbagala, alipokutana na mke wa mchungaji na timu yake.

 

Hata hivyo, wakiwa eneo la kanisa hilo, wakatonywa kuwa mchungaji ameamua ghafla kubadili kanisa na kwamba atafunga katika kanisa hilo tawi la Vianzi, ndipo kundi la watu akiwepo Paparazi wetu walitoka haraka kuelekea Vikindu kuwahi ibada ya ndoa hiyo ‘haramu’.

 

“Unajua nini? Kuna wambea wamempa taarifa mchungaji kuwa mkewe angekuja hapa kuipinga, ndiyo maana ameamua kwenda kufungia kanisa jingine. Sasa tunaelekea hukohuko,” mmoja wa watu kwenye msafara alisikika akisema. Awali, akizungumza na Uwazi, Maria ambaye ni mke wa ndoa wa mchungaji huyo, alisema: “Lazima niipate haki yangu. Huyo mchungaji ni mume wangu wa ndoa na tuna watoto wawili.”

 

Timu nzima ya Maria wakiwa na mwandishi wetu hatimaye walifika kwenye kanisa la Vianzi ambapo walifanikiwa kuwakuta maharusi bado hawajafunga ndoa.

 

MSAFARA WA BI HARUSI WAPOTEA

Hadi mishale ya saa 11 jioni msafara wa maharusi ulikuwa haujafika, lakini ilipokaribia saa 12 jioni ndipo uliwasili kwa maelezo kuwa walipotea njia ya kufika eneo hilo kwa vile walikuwa wageni.

 

MAMA MCHUNGAJI AVAMIA KANISANI

Maharusi wakiwa wanajiandaa kuingia kanisani mama Mchungaji (Maria) alimfuata Askofu wa Kanisa hilo, John Mzule na kumwambia kuwa Mchungaji Julius ni mumewe halali wa ndoa takatifu hivyo alifika kanisani hapo kwa ajili ya kuiwekea pingamizi ndoa hiyo.

 

Askofu huyo baada ya kumsikiliza vizuri na kumwelewa mama huyo alimuomba vielelezo vinavyothibitisha madai yake hayo, ambapo alitoa cheti cha ndoa na picha za matukio ya siku ya harusi yao. Baada ya kuona ushahidi huo, Askofu Mzule alimtaka mama huyo kuwa mtulivu na kuiacha ibada iendelee mpaka utakapofika muda wake, ataitwa.

IBADA YA NDOA YAANZA

Ibada ya ndoa hiyo ilianza ikiongozwa na Askofu Mzule ambapo kama kawaida ulipofika muda wa kukaribishwa mwenye pingamizi, mama Mchungaji alijitokeza mbele ya madhabahu ya kanisa hilo na kumwambia askofu huyo kuwa yeye ndiye mke halali wa bwana harusi aliyekuwa mbele ya madhabahu akitaka kufunga ndoa.

 

Askofu huyo alimuomba tena mama huyo ampe vithibitisho hivyo ambapo alitoa cheti cha ndoa na picha za kumbukumbu la tukio hilo.

 

KANISA LAFADHAIKA

Hali hiyo ilisababisha kanisa kuzizima na bibi na bwana harusi walianza kutokwa jasho katika hali iliyoonesha kutoamini macho yao baada ya mama mchungaji kuwavamia mafichoni walikotaka kufungia ndoa yao kwa siri. Askofu Mzule alimuuliza Mchungaji Julius kama anamfahamu mwanamke huyo ambapo alikiri kumfahamu.

 

Alipoulizwa kama ndiye mkewe au siye, mchungaji huyo alisema ni kweli alikuwa mkewe lakini waliachana kwenye vyombo vya sheria.

Alipotakiwa kutoa uthibitisho wa kuachana huko, alitoa barua aliyosema amepewa na mahakama (hakuitaja). Hata hivyo utetezi wake ulitupiliwa mbali na askofu huyo kwa maelezo kuwa, kama ni barua halali ya kuachana iliyotolewa mahakamani ilipaswa iwe na nakala mbili – moja ya mke na nyingine ya mume.

 

Kutokana na utata huo, Askofu Mzule aliahirisha kufunga ndoa hiyo hadi uchunguzi utakapokamilika; vikifutiliwa vitu mbalimbali kuhusu maisha ya wawili hao ikiwemo wachungaji waliowafungisha ndoa ya awali, wasimamizi, mashahidi wa ndoa na barua aliyoionesha bwana harusi akidai amepewa na mahakama kama hati ya kuvunja ndoa.

 

Katika hatua nyingine, Askofu Mzule alimuuliza Maria kama alikuwa tayari kuendelea kuishi na mumewe huyo; akaeleza yupo tayari. “Lakini kama mume wangu hanitaki tena basi tufanye mgawanyo wa mali tulizochuma pamoja. Tuna kiwanja kilichopo Mbande, pikipiki aina ya Boxer, friji, kitanda, godoro, vyombo vya ndani na pesa ya kuanzia maisha. Yakifanyika hayo, ndipo aendelee na mambo yake,” alisema Maria kwa sauti ya huzuni.

 

ASKOFU ATOA NENO KWA UWAZI

Askofu Mzule akizungumza na mwandishi wetu baada ya ndoa hiyo kusitishwa, alisema ndoa ya kikristo ni ya milele na haiwezi kuvunjwa na mahakama, ingawa wawili hao wanaweza kutengana kwa sababu za kiusalama lakini ndoa yao itatenganishwa na kifo pekee.

 

“Hakuna ndoa ya wake wengi kwa sisi Wakristo… na ikishafungwa, imefungwa hakuna kuachana hadi kifo. Wanaweza kutengana kwa sababu mbalimbali ikiwemo za kiusalama lakini siyo kuachana. Ni kifo pekee kinaweza kutengua ndoa ya Kikristo,” alisema Askofu Mzule.

BI HARUSI MPYA AKIMBIZWA HOSPITALI

Wakati sekeseke hilo likiendelea, bi harusi mpya aliyetajwa kwa jina moja la Stellah, aliishiwa nguvu na kuondolewa kanisani hapo kwa msaada wa wasaidizi wake na kupelekwa hospitalini. Taarifa zilizolifikia Uwazi baadaye, zilisema kuwa baada ya Stellah kufikishwa hospitalini na kufanyiwa uchunguzi wa awali alilazwa huku tatizo lililokuwa linamsumbua likifanywa siri.

 

MARIA ANA KWA ANA NA UWAZI

Baada ya kufanikiwa zuio la ndoa hiyo, Maria alizungumza kwa kina na mwandishi wa gazeti hili akieleza namna walivyofunga ndoa ya awali na maisha yao yalivyokuwa. Alisema, ndoa yao ilifungwa Septemba 25, mwaka 2010 katika Kanisa la Faith Church Missions lililopo Mbagala Kuu, jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kupata watoto wawili katika ndoa yao.

 

WAHAMIA MLANDIZI

Alisema, waliishi raha mustarehe lakini katika harakati za kusaka maisha walihamia Mlandizi ambapo kipindi hicho, Julius kabla ya kuwa mchungaji alikuwa mwalimu wa sekondari kwenye shule moja iliyopo Ruvu Stesheni.

SHETANI AANZA KUITIA NDOA MAJARIBUNI

Wakiwa katika harakati za kusongesha maisha, ilipofika mwaka wa saba wa ndoa yao (mwaka jana) Julis akiwa tayari ameshakabidhiwa uchungaji wa Kanisa la Gospel Revival Assemblies of God lililopo Mlandizi na Askofu wa Kanisa hilo, John Mzule, migogoro ya hapa na pale ilianza kujitokeza.

 

WATENGANA

Wahenga walisema ibilisi ana nguvu za ajabu hivyo ndivyo ilivyokuwa, migogoro hiyo ilipamba moto Machi, mwaka huu wawili hao walitengana, ambapo watoto walibaki kwa mwanaume na Maria aliamua kwenda kujipangia chumba chake Mlandizi Madafu na kumuacha Baba Mchungaji Mlandizi mjini.

 

Baada ya upweke wa miezi kadhaa, Mchungaji Julius alianzisha uhusiano na Stellah ambaye anadaiwa kuwa ni mtumishi wa taasisi moja mkoani Pwani. “Baadaye walianza michakato ya ndoa, mimi nilijua kila kitu. Kuna watu wanaonipenda walinieleza kila kinachofanywa na baba watoto wangu,” alisema Maria na kuongeza:

 

“Nadhani alihisi kuwa najua, ndiyo maana hakutaka kufunga ndoa hiyo kanisani kwake Mlandizi, badala yake akataka ifungwe Mbagala Kuu, huko napo kama unavyoona, akachezwa na machale na kuamua kuja kufunga hapa Vianzi, lakini Mungu mkubwa amemuumbua.” Maria alisema kuwa, anamshukuru Mungu kwa kuipigania haki lakini zaidi Askofu kwa kusimamia kweli ya Neno la Mungu.

 

“Namshukuru Mungu hajaniacha, lakini lazima nimshukuru pia Askofu Mzule ambaye ameonyesha kusimamia kweli ya Mungu, abarikiwe sana kwa hilo,” alisema. Uwazi halikufanikiwa kuzungumza na Mchungaji Julius ili naye aelezee tukio la ndoa yake kuvurugwa na kwamba jitihada za kumfanya.

AIBU YA MWAKA! Mchungaji Afumaniwa Akioa Mke Mwingine!

Comments are closed.