The House of Favourite Newspapers

Airtel Yatoa Elimu ya Afya Bure kwa Wajawazito

Meneja Huduma kwa Jamii wa Airtel, Bi Hawa Bayumi

Kampuni ya simu ya Airtel kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imewezesha kutoa elimu ya afya bure kwa wanawake wajawazito nchi nzima ambapo mpaka sasa, wanawake zaidi ya laki nne wamenufaika na mpango huo. Katika huduma hiyo, Airtel kwa kushirikiana na programu ya mHealth Tanzania Partnership inayoratibiwa na Cardno Tanzania chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Mradi wa Wazazi Nipendeni, huwaandikisha wanawake wajawazito na kuwasajili kisha kuanza kuwatumia ujumbe wa afya kuhusu ujauzito, dalili za hatari, tarehe za kliniki, tarehe za kujifungua na mambo mengine bure kabisa. Mradi wa Wazazi Nipendeni ulianzishwa kwa lengo la kutoa elimu ya afya na kuokoa vifo vya mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano ambavyo vilikuwa kwa kiwango cha juu hivyo Airtel imerahisisha zaidi kufikisha taarifa hizo kwa jamii. Akitoa tathmini juu ya mradi huo mpaka sasa, Mtasingwa Saulo kwa niaba ya mHealth Tanzania Partnership alisema wameshirikiana na Airtel tangu mwaka 2012 kuhakikisha taarifa mbalimbali za kiafya zinawafikia Watanzania bila gharama yoyote. “Mpaka sasa mradi huu umekuwa na mchango mkubwa sana, zaidi ya watumiaji laki 4 wameshajisajili na meseji zaidi ya milioni 27 zenye taarifa mbalimbali za afya zimetumwa bila gharama yoyote. Tunawashukuru sana Airtel kwa kushirikiana nasi katika kufanikisha mradi huu,” alisema. Kwa upande wake, Meneja Huduma kwa Jamii wa Airtel, Bi Hawa Bayumi alisema: “Sisi kama wadau wa huduma za mawasiliano tunatambua jinsi mawasiliano yalivyo na mchango mkubwa katika jamii na tunajisikia furaha kuwa mtandao wa kwanza ulioondoa gharama kwa wateja zaidi ya milioni 10 kupata taarifa hizi za afya bure bila gharama yoyote. “Lengo letu ni kuhakikisha tunatoa fursa mbalimbali kupitia huduma za mawasiliano  na kuokoa vifo vya akina mama na watoto wachanga vinavyochangiwa na ukosefu wa elimu ya kutosha.”

Comments are closed.