The House of Favourite Newspapers

Ajibu aifungia vioo Simba

Stori: Na Mwandishi wetu | CHAMPIONI

MKATABA wa straika Ibrahim Ajibu na Simba unamalizika mwishoni mwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara, lakini hadi sasa bado mchezaji huyo hajasaini mkataba mpya licha ya uongozi kumuomba kufanya hivyo.

Ajibu alifuatwa na viongozi wa Simba hivi karibuni kwa mara nyingine ili kuongeza mkataba wake baada ya kurejea kwenye majaribio katika Klabu ya Haras Al Hadood ya Misri.

Simba imekuwa na shauku kubwa ya kutaka kumuongeza mkataba mpya mchezaji huyo kabla ya ule wa awali kufikia tamati ili wawe naye katika msimu ujao wa ligi na michuano mingine.

Mmoja wa mabosi wa Simba, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, walimfuata kwa mara nyingine Ajibu ili kuweza kumuongeza mkataba wakidhani anaweza kuwakubalia lakini hali imekuwa tofauti kwani ameendelea kuwagomea.

“Viongozi walimfuata Ajibu alipotoka Misri ili aongeze mkataba mwingine lakini hali imekuwa ni vilevile kwani amegoma katakata kuongeza mkataba.

“Nadhani kuna timu zimemuahidi kitu pindi atakapomaliza mkataba na Simba ndiyo maana anaendelea kukataa kwani awali tulijua angekubali lakini mambo yamebaki kuwa vilevile.

“Kwa sasa mtazamo wa viongozi ni kuwaangalia wachezaji wengine vijana ambao wanaonekana kuwa na uwezo zaidi wa kuisaidia Simba,” alisema bosi huyo.

Alipotafutwa Ajibu kuelezea mustakabali wake Simba, alisema bado hajajua iwapo ataongeza mkataba ama la.

 

Comments are closed.