The House of Favourite Newspapers

Aliyedai Kutajirishwa na Freemason Anaswa, Aanika Ukweli – Video

0

 

Mwanamke aliyedai kutajirishwa na Freemason amefikwa na mazito ambayo hatoyasahau maishani mwake.

Mwanamke huyo ambaye wiki iliyopita alijitambulisha kwa jina la Glory, alidakwa baada ya video kusambaa mitandaoni akijinadi kutajirishwa na Freemason.

Katika video hiyo mwanamke huyo alisikika akieleza jinsi awali alivyoishi maisha magumu yaliyosababisha kuachika na mumewe na kudai kwa sasa amepata utajiri mkubwa baada ya kujiunga na Freemason.

 

“Naitwa Glory, napenda kuwaeleza wananchi kuwa awali baada ya kumaliza chuo niliishi maisha magumu sana, niliolewa kisha nikaachana na mume wangu baada ya maisha kuwa magumu sana. Lakini siku moja kwenye mitandao ya kijamii nililiona tangazo la Wakala Mkuu wa Freemason, Mustapha.

 

“Baada ya kuniunganisha nao maisha yangu kwa sasa ni yakitajiri kama hivi unavyoniona nna nyumba mbili; moja hii na nyingine ipo Mbezi Africana, nna magari matatu; kuna hii IST, nna Range na Carina.

“Hivyo, nawaomba wananchi wachukue namba ya Wakala Mkuu wa Freemason, Mustapha ili nao waweze kupata utajiri kama huu na waishi kitajiri”. Alionekana kusema kwenye video hiyo.

 

 

Baada ya video kusambaa kwa kasi mitandaoni, mijadala ilianza kuzuka wengi wakisema dada huyo alikuwa akitumiwa na matapeli kusambaza tangazo hilo lenye lengo la kuwaibia wenye tamaa ya utajiri wa njia ya mkato.

 

Wengine wakisema dada huyo ni miongoni mwa matapeli, wapo waliosema huwenda yaliyokuwa yakisemwa na dada huyo yalikuwa na ukweli hasa kutokana na muonekano mzuri wa mali alizokuwa akizionesha na kudai ni zake.

 

Wakati video hiyo ikisambaa, ikaanza kusambaa video nyingine ikionesha dada huyo kuwekwa chini ya ulinzi na kuhojiwa kuhusiana na tangazo lake alilokuwa akilitoa.

 

Mwanamke alinaswa kwenye mtego wa askari polisi ambapo baadaye ilionekana video nyingine akihojiwa baada ya kibano.

Wakati akihojiwa akiwa chini ya ulinzi alijitambulisha kwa jina la Hajia Salim na kusema yeye hahusiki lolote na masuala ya Freemason isipokuwa alipewa dili ya kutengeneza tangazo hilo kwa kupewa ujira wa shilingi 30,000.

 

Mwanamke huyo alisema maneno aliyokuwa akisema ni kwa ajili ya tangazo hilo tu na wala hana utajiri wowote zaidi ya biashara yake ya kupika keki.

Kufuatia sakata hilo, wanahabari waliifuatilia taarifa hiyo na kubaini kuwa mdada huyo alitiwa nguvuni na Polisi wa Kituo cha Kawe, Dar.

 

Hata hivyo, chanzo hicho kilisema kuwa mwanamke huyo alitiwa mbaroni kituoni hapo na mmiliki wa nyumba iliyooneshwa kwenye video hiyo na kudai ni yake aliyoipata baada ya kujiunga na Freemason.

Chanzo hicho kilidai kuwa mwenye nyumba huyo alimfungulia shitaka la utapeli kituoni hapo.

 

“Imedaiwa kuwa jamaa akiwa safarini ndipo akainasa video ya mwanamke huyo akionesha nyumba yake pamoja na mali zake zingine akijifanya ni zake kitendo kilichofanya arudi Dar haraka kutoka mkoani alipokuwa,” kilisema chanzo chetu.

 

Kufuatia sakata hilo, wanahabari wetu walizungumza na afisa mmoja kutoka Jeshi la Polisi Kitengo cha Kuzuia Uharifu Kimtandao (Siber Crime) ambaye alisema suala la kujitangaza kutajirika kupitia Freemason si kosa labda kama angewataka wananchi wamtumie pesa.

 

Afisa huyo alisema tangazo hilo linaonesha ushuhuda kama watu wanaotoa ushuhuda wa kufanikiwa kwenye nyumba za ibada na sehemu nyingine.

 

“Hapa ofisini hatujaletewa huyo mtu ila kama kosa ni kusambaza video hiyo bado hatujaona kosa lake labda kama kuna kosa lingine ndiyo limesababishwa akamatwe”, alimaliza kusema afisa huyo.

 

Wanahabari wetu hawakuishia hapo, walimtafuta Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi (ACP) Mussa Taibu na kumuuliza kinachoendelea kuhusiana na mwanamke huyo aliyetiwa mbaroni kwenye kituo cha Kawe kilichopo chini yake, lakini alisema halijamfikia.

 

Hata hivyo, aliahidi kulifuatilia na kurudisha majibu, lakini tangu muda huo kila alipopigiwa simu hakupokea tena mpaka tunakwenda mitamboni.

Richard Bukos na Neema Adrian

 

DADA ALIYE – TREND KUTAJIRISHWA NA FREEMASON, POLISI WAFUNGUKA – “HANA KOSA”

Leave A Reply