The House of Favourite Newspapers

Aliyenaswa wizi wa watoto atoa kioja kortini

0

BAADA ya mwishoni mwa mwaka jana kunaswa kwa wizi wa watoto wawili jijini Mbeya, Hawa Ally Mkalipa (40), mkazi wa Tegeta jijini Dar amezua kioja cha aina yake kortini, IJUMAA WIKIENDA linakupa habari kamili.  Hawa alitoa kioja hicho kwenye Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Mbeya alikopandishwa kwa ajili ya kujibu tuhuma hizo zinazomkabili za kuiba na kupatikana na watoto hao.

Akisoma hati ya mashtaka, mwendesha mashtaka wa Serikali, Ofmed Mtenga alisema, mshtakiwa Hawa alitenda kosa hilo Disemba 28, mwaka jana katika eneo la Ituha jijini Mbeya ambapo bila ridhaa ya wazazi na kwa nia ovu alimuiba mtoto wa kiume, Faisal Mashaka Juma (5) na wa kike, Farhan Mashaka (2), wote wa familia moja kisha kutokomea nao kusikojulikana hadi walipopatikana wiki moja baadaye huko mkoani Tabora.

Wakili Mtenga alisema kitendo hicho ni kinyume na kifungu namba 169 (1) A cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu hivyo kuieleza mahakama kwamba watawaita mashahidi wa kwenda kuthibitisha mshtakiwa Hawa kutenda kosa hilo.

Mshtakiwa Hawa alikana makosa yote mawili ambapo kwa mujibu wa upande wa mashtaka maelezo ya usikilizwaji hoja za awali yatakuja mahakamani hapo Februari 19, mwaka huu na tayari upelelezi wa shauri hilo umekamilika.

Dhamana ya mshtakiwa huyo iko wazi kwa kutimiza masharti kadhaa yaliyotolewa na mahakama ikiwa ni pamoja na kuwa na wadhamini wawili wenyeji wa mkoani Mbeya na kusaini hati ya mali isiyohamishika yenye thamani isiyopungua shilingi milioni tano.

AZUA KIOJA

Alipoulizwa kuhusu kutekeleza wizi huo, Hawa alisema hakuiba watoto, bali alikuwa njiani ndipo akasikia kunguru akikoroma na kubadilika kuwa mtu na kumkabidhi watoto hao kisha yule mtu akajibadilisha kuwa kunguru akapeperuka na kupotea ndipo akaondoka na watoto hao wawili aliopewa na kunguru.

Habari zilieleza kuwa, siku ya tukio alifika jijini Mbeya ndipo alipobeba watoto hao kisha kupandia gari katika kituo cha mabasi Nanenane kuelekea Tabora ambapo alimwacha mmoja Tabora mjini baada ya kumkataa na kuendelea na safari na mwingine ambaye naye alianza kuumwa hatua iliyomfanya atafute hospitali ili kwenda kumtibu ndipo alipokamatwa baada ya kutiliwa shaka.

Hakimu Zawadi Laizer aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 19, mwaka huu kwa ajili ya usomwaji hoja za awali na mshtakiwa alirudishwa mahabusu baada ya kutokuwa na wadhamini mbele ya mahakama hiyo.

STORI: EZEKIEL KAMANGA, MBEYA

Leave A Reply