The House of Favourite Newspapers

Aliyetelekeza Makontena 500 ya Shisha Bandarini Asakwa

0

Takribani makontena 500 yenye urefu wa futi 40 yametelekezwa katika bandari ya Dar es Salaam yakidaiwa kuwa na shehena ya malighafi za kutengeneza kilevi cha shisha ziliizikwisha muda wake wa matumizi.

 

Hayo yalibainishwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo wakati wa ziara yake katika bandari hiyo kujionea makontena hayo ambayo yaliingizwa nchini mwaka 2019.

 

Malighafi hizo za shisha (molasses) zinatumika kama kiburudisho ambacho kinawekwa kwenye vifaa maalumu na watu wanavuta mithiri ya sigara. Hivyo, endapo kitakuwa kimekwisha muda wake, watumiaji wanaweza kupata madhara ya kiafya.

 

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Waziri Jafo aliagiza kukamatwa kwa kwa raia mmoja wa kigeni aliyetambuliwa kwa jina moja la Kaissy kwa tuhuma za kuingiza nchini vitu hivyo ambavyo vimekwisha muda wake.

 

Jafo alisema ni dhahiri mzigo huo ni uchafu ambao umekuja kutupwa nchini, hivyo ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuhakikisha mtu huyo anakamatwa na anarudisha mzigo ulikoutoa kwa gharama zake mwenyewe.

 

“Nina taarifa ameingiza makontena zaidi ya 500 tangu mwaka 2019, sasa anaingiza bidhaa za shisha wakati hakuna hata kiwanda, kweli huyo ni mwekezaji? Tangu mwaka 2019 anaingiza makontena tu, lakini hakuna kiwanda, hilo sitakubali,” alisema Jafo.

Leave A Reply