The House of Favourite Newspapers

Arusha: Polisi Yaua ‘Majambazi’ Watano – Video

0

POLISI mkoani Arusha imewaua watuhumiwa wa ujambazi sugu watano usiku wa saa 3:45, Januari 29, 2020, eneo la njia panda ya Matevesi Kata ya Olmot mkoani humo baada ya kukaidi amri ya polisi ya kusimama wakati wakienda kufanya tukio la uhalifu wilayani Simanjiro.

 

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Jonathan Shanna,  amesema kikosi cha jeshi la polisi mkoani humo kimewaua majambazi sugu watano wakati wakijibizana risasi na polisi na kuwakuta na silaha aina ya Shotgun Pump Action 32265, Chinese Pistol, Bastola 1 bandia, risasi 11 pamoja na simu 2 na pikipiki 3.

 

Amesema msako unaoendeshwa na polisi hautaishia hapo, na watahakikisha kuwa tabia za kuvuna pasipo kupanda zinazofanywa na vikundi vya watu wachache ndani ya mkoa huo zinadhibitiwa.

 

Amesisitiza kuwa jiji la Arusha litakuwa shwari na akaonya kuwa wale wote wanaofanya vitendo vya uhalifu wataangukia mikononi mwa polisi.

 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo,  ameishukuru polisi kwa kuzidi kuimarisha ulinzi na usalama katika jiji hilo. Pia amechukua nafasi hiyo kutuma salamu na kumpongeza waziri mpya wa Mambo ya Ndani,  George Simbachawene,  kwa kuanza kazi vizuri.

 

“Sisi kama mkoa tutashirikiana na Wizara  ya Mambo ya Ndani kuona namna ya kuwapa zawadi askari hawa waliofanikisha jambo hili (la kuwaua majambazi sugu watano) maana wamenifanya niwe na furaha sana,” amesema  Gambo.

 

Leave A Reply