The House of Favourite Newspapers

Auawa Akigombania Mwanamke Usiku wa Pasaka

MKAZI wa Mji Mdogo wa Sirari tarafa ya Inchugu, wilayani Tarime mkoani Mara, Charles Mkono (26) aliyejulikana kwa jina la DJ ameuawa kwa kuchomwa kisu tumboni majira ya saa 2 usiku, wakati wa mkesha wa Pasaka katika nyumba ya kulala wageni ya Mzalendo ambayo ipo jirani na nyumbani kwao marehemu, mjini Sirari.

 

Imeelezwa kuwa, Mkono ameuawa kwa kuchomwa kisu na mlinzi wa nyumba ya hiyo aliyejulikana kwa jina moja la Juma, mkazi wa Kitongoji cha Nyamorege-Machinjioni kata ya Sirari, baada ya kutokea ugomvi unaosadikiwa ni wa kumgombea mwanamke.

 

Watu walioshuhudia mkasa huo walisema kwamba wawili hao walikuwa wakimgombea mwanamke aliyetambuliwa kwa jina moja la Happy ambaye ilidaiwa alikuwa rafiki wa Mkono.

 

Diwani wa Kata ya Sirari, Nyangoko Paulo, alisema tukio hilo la Mkono kuchomwa kisu tumboni na mlinzi lilitokea usiku saa 2 baada ya kukuta Happy akizungumza na mlinzi, jambo lililozua ugomvi. Mkono alisikika akidai kuwa mlinzi huyo alikuwa anamfanyia mwanamke wake mpango kwa mtu mwingine aliyekuwa amelala katika nyumba hiyo ya wageni.

 

Kamanda wa Polisi Tarime, Rorya, Henry Mwaibambe, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema Jeshi la Polisi linamsaka mtuhumiwa.

Comments are closed.