The House of Favourite Newspapers

Ayoub, Onana Wawajaza Noti Mastaa Simba

0

MABAO mawili aliyoyafunga mshambuliaj raia wa Cameroon, Willy Osamba Onana na michomo aliyokoa kipa, Ayoub Lackred imetosha kuwapa bonasi ya zaidi Sh 150Mil wachezaji wa timu hiyo.

Hiyo ni baada ya Simba juzi Jumanne kufanikiwa kuwafunga Wydad Casablanca mabao 2-0 katika mchezo wa nne wa hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam, Onana alifanikisha ushindi wa mabao 2-0 yote yakifungwa na yeye katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo.

Kivutio katika mchezo huo, alikuwa mlinda mlango wa Simba, Ayoub ambaye aliendelea kuonyesha ubora wake uliowashitua mashabiki wa Simba, kwa kuokoa hatari golini kwake ambazo kama angekosa umakini, basi matokeo yasingemalizika hivyo.

Taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, kutoka ndani ya wachezaji hao ni kuwa wachezaji hao waliahidiwa bonasi ya Sh 150Mil, kama watawafunga Wydad Casablanca katika mchezo huo wa marudiano.

Spoti Xtra, linafahamu kuwa bonasi hiyo walitarajiwa kupewa baada ya mchezo huo kumalizika, kwa lengo la kuwaongezea morali na hamasa ya kupambana katika michezo mingine wa kimataifa.

“Siku moja kabla ya mechi husika, kumekuwa na utaratibu wa viongozi, kufanya kikao na wachezaji na kikubwa zaidi kutoa hamasa ya sisi kupambana ili tupate ushindi.

“Na juzi kabla ya mchezo huu wa Wydad Casablanca, tulifanya kikao na viongozi na kutupa hamasa nzuri ya sisi kupambana sambamba na kutupa ahadi ya bonasi ya Sh 150Mil kama tukiwafunga wapinzani wetu.

“Tunashukuru tulifanikiwa kupata ushindi, kutokana na kila mchezaji kutimiza majukumu yake ya uwanjani kushambulia na kulinda goli tukapata matokeo hayo,” alisema mchezaji huyo mwandamizi katika timu.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Ahmed Ally alizungumzia hilo kwa kusema kuwa “Ahadi ya bonasi inakuwepo katika kila mchezo, ambayo imekuwa ikitolewa siku moja kaba ya mechi inayokuwa siri kati ya Viongozi na wachezaji wenyewe.

STORI NA WILBERT MOLANDI

Leave A Reply