Azam FC Waweka Mikakati ya Kuwamaliza Waarabu

KUELEKEA mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya kwanza dhidi ya Pyramids FC ya Misri, Azam FC wameweka mikakati ya kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye ardhi ya nyumbani.

 

Azam FC wanatarajia kucheza mchezo huo Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar, kabla ya marudiano wiki ijayo nchini Misri.

 

Akizungumzia maandalizi yao, Ofisa Habari wa Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’, alisema: “Kikosi kinaendelea na mazoezi na wapinzani wetu wanatarajia kufika leo (jana) saa tatu usiku.

 

“Pyramids watafanya mazoezi Oktoba 14 na 15, tayari kwa ajili ya mchezo wa Oktoba 16 kwenye Uwanja wa Azam Complex.

 

“Kocha wetu anayafanyia marekebisho makosa yaliyoonekana kwenye michezo iliyopita. Hakuna majeruhi zaidi ya Prince Dube, wachezaji wote waliokuwa kwenye timu za taifa wamerejea na wanaendelea na mazoezi.

 

“Mikakati ya ushindi tumeshaiweka kwa upande wa viongozi katika kuhakikisha ni namna gani Pyramids wanapigika hapa nyumbani.”

Leen Essau, Dar es Salaam


Toa comment