The House of Favourite Newspapers

Azam FC yawachuja vibaya Wasauz

0

Mohamed Mdose, Dar es Salaam
USHINDI wa mabao 4-3 ambayo Azam FC imeupata jana kwenye Uwanja wa Chamazi ilipocheza dhidi ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini umeiwezesha kusonga mbele katika hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho kwa jumla ya mabao 7-3.

Azam imepata ushindi huo mnono ambapo pia ilitawala mchezo huo wa pili wa hatua ya kwanza, lakini habari nzuri ilikuwa ni uwezo wa juu ulioonyeshwa na straika wa Azam, Kipre Tchetche ambaye alifunga mabao matatu katika mchezo huo wa jana.

Ikicheza kwa kuutawala mchezo huo, Azam ilipata mabao yake kupitia kwa Kipre dakika ya 23, 55 na 87 kisha John Bocco akafunga dakika ya 42, wakati mabao ya wageni hao yalifungwa na Jabulani Shongwe dakika ya 44, Mosiatlhga Koiekantse dakika ya 60 na Botes Henrico dakika ya 90.

Katika mchezo huo ambao ulishuhudiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye aliyekuwepo uwanjani hapo, Azam walionekana kuwa vizuri kwa kutawala muda mwingi lakini uzembe wa safu ya ulinzi ulifanya wapinzani wapate mabao matatu huku mara zote kipa wa Azam, Aishi Manula na mabeki wake wakiishia kulaumiana.

Katika mchezo huo ulioanza saa 9:15 alasiri wachezaji wengi wa Bidvest walionekana kuchoka hasa kipindi cha pili, mara baada ya mchezo huo, Jabulani aliipongeza Azam kwa ushindi huo huku akisema kuwa hali ya hewa ya joto kali ilichangia kuwaathiri kwa kuwa wametoka kwenye hewa ya baridi.

Upande wa Kocha Msaidizi wa Azam, Denis Kitambi alisema: “Tumecheza vizuri na ndiyo maana tumepata ushindi lakini tuna tatizo la kuridhika mapema na ndiyo maana tukaruhusu mabo ya kizembe.”

Kocha wa Bidvest, Hunt Gevin alisema timu yake haikutilia maanani michuano hiyo kwa kuwa haina fedha nyingi kama ilivyo ligi yao ambayo wanashiriki, ndiyo maana akapanga kikosi cha vijana wengi katika mechi zote mbili.

Azam sasa inatarajiwa kukutana na Espérance de Tunis ya Tunisia katika raundi ya pili ya michuano hiyo ambapo mechi ya kwanza itachezwa Dar es Salaam wiki ya Aprili 8 hadi 10 kisha kurudiana wiki mbili baadaye.

Leave A Reply