The House of Favourite Newspapers

Azam noma, yatinga fainali FA

0

PIC+AZAM

Wachezaji wa  azam wakishangilia

Johnson James, Shinyanga
Azam FC jana wametinga fainali ya Kombe la FA baada ya kuichapa Mwadui kwa penalti 5-3 kufuatia dakika 120 zenye upinzani mkali, kumalizika kwas are ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.

Dakika 90, zilimalizika kwa sare ya 1-1 na zilipoongezwa 30 nazo zilikuwa na upinzani mkali uliosababisha ziishe kwa sare nyingine ya 1-1, ndipo ikalazimika kutumika changamoto ya mikwaju ya penalti kuamua mshindi.
Hamis Mcha aliifungia Azam FC mabao mawili katika mchezo huo ndani ya dakika 120 huku Aggrey Morris akifunga penalti ya ushindi.

Hata hivyo, haikuwa kazi rahisi kwa Azam kupata ushindi huo, kwani walilazimika kucheza kwa dakika 120, baada ya dakika 90 za kawaida kumalizika matokeo yakiwa ni sare ya bao 1-1 huku Mwadui wakionyesha upinzani mkubwa.

Mcha ambaye muda mrefu msimu huu alikuwa majeruhi na hii ilikuwa mechi yake ya pili tangu arejee uwanjani, alifunga bao la Azam dakika ya nne tu ya mchezo huo kufuatia kupata pasi nzuri kutoka kwa Ramadhani Singano ‘Messi’. Aliongeza bao lingine dakika sita ndani ya zile dakika 30 za nyongeza.

Dakika nne baadaye, Mwadui walikuwa kwenye lango la Azam, wakafanya shambulizi zito lakini wakakosa bao la wazi. Mwadui walikuwa kama wamemwagiwa maji ya tindikali, kwani walilisakama lango la Azam kwa muda mrefu. Dakika ya 15, walikosa bao lingine la wazi kufuatia shuti alilolipiga Kelvin Kongwe kwenda nje.

Azam walifanya mabadiliko kwa kumtoa Singano na nafasi yake kuchukuliwa na Abdallah Kheri lakini mafanikio hayo yaliiumiza zaidi Azam FC kwani walipigwa bao dakika ya 83 lililofungwa na Hassan Kabunda. Matokeo hayo yalidumu hadi mwisho wa mchezo, mechi ikalazimika kuamuliwa kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.

Mwadui walisawazisha bao la pili dakika ya 120, kwa mkwaju wa penalti ya Jabir Aziz ‘Stima’ baada ya mchezaji wa Azam kuunawa mpira katika eneo la hatari.

Penalti za Azam zilifungwa na Wazir Salum, Alain Wanga, Himid Mao, John Bocco na Aggrey Morris huku kwa upande wa Mwadui zikifungwa na Jabir Aziz, Mfaume Bobi, Malika Ndeule wakati Kelvin Sabato alikosa.

Leave A Reply