The House of Favourite Newspapers

Baada ya Kutoka Karantini, Mondi Adaiwa Mamilioni

0

RAIS wa lebo kubwa ya muziki Afrika ya Wasafi Classic Baby (WCB), Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, ameruhusiwa kutoka karantini alikokuwa na wenzake kwa siku 14 kutokana na janga la Virusi vya Corona na kukutana na msala mwingine wa kudaiwa mamilioni.

 

Mbali na kudaiwa mamilioni hayo, wakati akitoka karantini, Jumatatu ya wiki hii, pia ilikuwa ni siku ya kusikilizwa kwa kesi yake nyingine iliyokuwa ikiunguruma kwenye Kitengo cha Ardhi cha Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar.

 

Katika kesi hiyo, Diamond au Mondi anadaiwa shilingi milioni 33 za Kitanzania kutokana na uharibifu wa mali kwenye nyumba aliyokuwa amepanga maeneo ya Kijitonyama jijini Dar, zilipokuwa ofisi za Wasafi kabla ya kuhamia Mbezi-Beach, Dar.

 

Kesi hiyo iliahirishwa juzi Jumatatu kutokana na hakimu kuumwa, ambapo inaendelea tena leo (Jumatano).

 

TUJIUNGE SUMBAWANGA

Wakati hayo yakiendelea jijini Dar, ghafla tu yameibuka madai mengine kutoka kwa wakazi wa Kijiji cha Senti, Manispaa ya Sumbawanga, Rukwa.

 

Wakazi hao wanaiomba Halmashauri ya Mji wa Sumbawanga kumalizia ujenzi wa shule ya msingi ya kijiji hicho baada ya ujenzi wake kusimama zaidi ya mwaka mmoja kutokana na Mondi kushindwa kutekeleza kwa wakati ahadi yake ya kukamilisha ujenzi wa shule hiyo.

 

Ombi hilo walilitoa mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kuona kuwa, shule ya kijiji chao waliyokuwa wameanza kuijenga na kutarajia ingekuwa imekamilika tangu Januari mwaka huu na kuchukua wanafunzi, imeshindikana kujengwa.

 

Ujenzi huo ulisimama baada ya Mondi kufika shuleni hapo, Desemba 8, 2018 na kuahidi kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 68 za Kitanzania kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa ambavyo vingeanza kutumika mwaka huu, lakini mambo hayakuwa hivyo.

Ahadi ya Mondi ilisababisha furaha kubwa kwa wakazi hao hadi wakaamua shule hiyo ipewe jina la Diamond Platnumz Primary School.

MWENYEKITI WA KAMATI YA SHULE

Mmoja wa wakazi hao ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa shule hiyo; Aladin Mwasomola, alisema kuwa wananchi wa kijiji hicho walikuwa na ari kubwa ya kujitoa kuhakikisha ujenzi wa madarasa hayo unakamilika.

 

Alisema kuwa, ari hiyo ilitoweka baada ya Mondi kufika kwa ajili ya kufanya tamasha la muziki (Wasafi Festival) na kuombwa na Serikali ya wilaya kutembelea miradi ya maendeleo.

 

Mondi alitembelea maeneo tofauti na alitoa misaada, ikiwemo Kituo cha Kulelea Yatima cha Mtakatifu Martin de Pores kilichopo mjini Sumbawanga.

Baada ya hapo, alifika katika Kijiji cha Senti na kuahidi kukamilisha ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa alivyovikuta vikijengwa.

 

AHADI MIL. 68

Wakazi wa kijiji hicho walikuwa wameshajenga madarasa hayo kufikia kwenye linta ambapo Mondi aliwataka kuacha kuendelea na michango pamoja na nguvu kazi, kwani yeye atamalizia kwa kutoa pesa shilingi milioni 68 ambazo zitatosha kupaua, kununua mabati na kupiga ripu vyumba hivyo ili mwaka huu wanafunzi waweze kuvitumia na shule hiyo itakuwa imefunguliwa rasmi.

 

Tangu alipotoa ahadi hiyo, Mondi hajawahi kutoa fedha yoyote mpaka sasa, hali iliyosababisha watoto wa kijiji hicho kushindwa kuanza masomo katika shule ya kijiji chao na kulazimika kutembea umbali mrefu kufuata masomo.

 

Wakazi hao walisema kuwa, baada ya kuona hali hiyo, iliwalazimu kuuomba uongozi wa halmashauri hiyo kuwasaidia kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo kuliko kuendelea kusubiri msaada wa Mondi ambao haifahamiki utapatikana lini.

 

MKURUGENZI SASA

Mwishoni mwa wiki iliyopita, gazeti hili lilimuuliza Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga; Jacob Mtalitinya kuhusu ahadi hiyo.

Mkurugenzi huyo alikiri Mondi kutoa ahadi hiyo, lakini bado hajaikamilisha.

Alisema, halmashauri hiyo imekuwa ikimkumbusha Mondi kuhusu ahadi hiyo ambayo imechukua muda mrefu na amekuwa akisisitiza ataitoa.

 

Alisema kuwa, manispaa hiyo imeanza mpango wa kukamilisha ujenzi wa madarasa hayo ambapo Mondi atakapokuwa tayari kutoa ahadi yake hiyo, itaelekezwa kwenye maeneo mengine kwani bado halmashauri hiyo ina uhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa, takriban 800.

Jitihada za kumpata Mondi hazikuzaa matunda, hivyo zinaendelea ili kujibu madai hayo.

 

TUJIKUMBUSHE

Jumamosi ya Desemba 2, 2018 ilikuwa cherekochereko kwa wakazi hao baada ya Mondi kufika kijijini kwao na kuweka jiwe la msingi kwenye shule hiyo iliyopewa jina lake.

Katika ahadi yake, Mondi alisema; “Mimi nathamini sana elimu na niwaahidi kitu kimoja kwamba, ujenzi huu uliyobaki, nitaumalizia wote.”

 

USHAURI KWA MONDI

Gazeti hili linafahamu kwamba, Mondi amekuwa na ahadi nyingi za kusaidia makundi mbalimbali kwenye jamii, ikiwemo kusomesha wanafunzi, kujenga misikiti na shule, kusaidia mitaji na mengine mengi, lakini amekuwa akidaiwa kushindwa kutimiza ahadi zake.

 

Gazeti hili linamshauri Mondi kutoa ahadi pale anapokuwa na uwezo na uhakika wa kusaidia ili kuondoa malalamiko ya mara kwa mara. MHARIRI

Leave A Reply