The House of Favourite Newspapers

BAADA YA MUME WAO KUFARIKI… MBUNGE, MKE MWENZIYE PACHIMBIKA

ARUSHA: Pamechimbika! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), Josephine Sebastian Ole Lemoyani (Chadema) kuingia kwenye mgogoro wa kifamilia na mke mwenzake unaohusishwa na nyumba ya marehemu mume wao aitwaye Husein Ole Lemoyani Laizer aliyefariki mapema mwezi huu nyumbani kwake Njiro, jijini Arusha.

 

TUPATE HABARI KAMILI

Sakata hilo la aina yake ambalo limewaacha vinywa wazi wakazi wa eneo hilo, inadaiwa kuwa wawili hao akiwemo mke mwenzake aitwaye Precious Zalkha waliolewa kwa nyakati tofauti na marehemu na kila mmoja alibahatika kupata mtoto mmoja wa kiume.

 

ALIKUWA HAISHI NAO

Hata hivyo, hadi marehemu anafariki dunia Oktoba 2, mwaka huu hakuwa akiishi na mke hata mmoja badala yake aliishi na mtoto wake wa kiume aitwaye Lenana Hussein (22) ambaye ni mtoto wa mke mdogo, Precious Zalkha baada ya wake zake hao kila mmoja kuanzisha maisha yake.

 

TUMSIKIE MKE MDOGO

Akizungumzia tukio la Oktoba 28, mwaka huu, lililotokea nyumbani kwa marehemu, majira ya saa kumi jioni, mke mdogo wa marehemu ameeleza kusikitishwa na hatua ya kufukuzwa kwa mwanaye aitwaye Lenana aliyekuwa akiishi na marehemu mume wake huku akitishiwa na silaha za jadi na morani wa kimasai.

 

“Nilienda kumsalimia mwanangu hapo nyumbani kwa marehemu mume wangu kama kawaida yangu, lakini siku hiyo nilikuta vijana wa kimasai wakiwa na silaha za jadi na kuniambia siruhusiwi kuingia ndani huku wakidai hata mtoto wangu hatakiwi kufika hapa akija atakuta nguo zake nje ya geti,” alidai Precious.

 

ADAI KUKUTA ULINZI MKALI

Alidai kuwa wamasai hao wakiwemo wazee, walimwambia wametumwa na Mbunge Josephine kulinda eneo hilo na kwamba hatakiwi mtu yeyote kufika eneo hilo hadi pale shughuli za kimila zitakapofanyika.

 

POLISI WATINGA

Mama huyo alidai kuwa, wakati wanaendelea kubishana kwa maneno makali ndipo polisi kutoka Kituo Kidogo cha Engutoto walifika baada ya mbunge huyo ambaye hakuwepo eneo la tukio kudaiwa kuwapigia simu kwa maelezo kuwa, kuna watu wamevamia nyumbani kwake wakifanya vurugu.

 

“Polisi walituchukua hadi kituoni na baada ya kutuhoji walituachia huru mimi na ndugu zangu na kutakiwa kufika Kituo Kikuu cha Polisi kesho yake ambapo siku iliyofuata tulifika kituoni hapo pamoja na wale wamasai waliotishia kutupiga na katika mazungumzo na OCD (Mkuu wa Kituo), aliamuru mtoto wangu aendelee kuishi hapo hadi taratibu nyingine zitakapokamilika,” alidai Precious.

Image result for Josephine S. Lemoyan, EALA MP

MBUNGE ANASEMAJE?

Akizungumzia mgogoro huo, Mbunge Josephine ambaye ni mke mkubwa wa marehemu, alikana kuwatuma morani hao wa kimasai akidai kuwa hajui chochote kwa sababu hakuwepo eneo la tukio. “Unajua ndo kwanza tuna msiba na sasa tunasubiri 40 ifike tujue taratibu zikoje na hilo suala wakati linatokea mimi nilipata safari na kwenda Mwanza, kwa hiyo sijui chochote kilichoendelea kwa sababu nimeondoka jioni hii kukiwa shwari,” alisema mbunge huyo na kuongeza:

 

‘’Mimi ni mtoto wa kike na nipo chini ya wazee wa kimila na nina adabu ya kusikiliza wazee wangu wa ukoo, nimefundishwa na siwezi kwenda kinyume na taratibu za kimila na huyo anayekulalamikia mwambie afuate taratibu za kimasai.” Hata hivyo, siku iliyofuata mbunge huyo alionekana Kituo cha Polisi akiwapakia wazee wa kimasai kwenye gari lake baada ya kukamilika kwa mazungumzo katika Ofisi ya OCD, Arusha.

 

MTOTO WA MAREHEMU ANENA

Naye mtoto wa marehemu aitwaye Lenana ambaye ni mtoto wa mke mdogo wa marehemu alisema kuwa, kwa muda mrefu amekuwa akiishi na marehemu baba yake hadi kifo chake na amekuwa akipata misukosuko mingi tangu baba yake afariki.

 

Alisema siku ya tukio alitoka nyumbani kwenda kuangalia mpira na baadaye alipigiwa simu akiambiwa kuwa mama yake anapelekwa polisi na baada ya kufika nyumbani alikutana na morani wa kimasai waliomwambia hatakiwi kufika nyumbani hapo, jambo lililomshangaza. Mpaka gazeti hili linakwenda mtamboni lilikuwa halijapata muafaka uliofikiwa na hivyo mwandishi wetu anaendelea kufuatilia kwa karibu ili kujua hatma ya msuguano huo.

STORI: Joseph Ngilisho.

Comments are closed.