The House of Favourite Newspapers

Baba P… Baba Pili… Baba Pilima!-8

0

ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA:
Ina maana akiamua kusema basi, halafu akaendelea na baba Pili atakuwa ameanza tabia ya kurukaruka…
“Kwani wewe kwa jina la mtoto wako yeyote yule unaitwa baba nani?” mama Pilima alimuuliza mwanaume huyo huku akimwangalia kwa macho yaliyojaa mahaba mazito…
“Naitwa baba P.”TAMBAA NAYO…

“He! Baba P! P ni kifupi au ndiyo jina lote?”
“Kifupi.”
“Kirefu chake?”

“Pilima. Kwa hiyo mimi unaweza kuniita baba Pilima.”
Mama Pilima alicheka sana, akasimama akiendelea kucheka na kusema…
“Haya ni maajabu makubwa kwangu…”
“Kwa nini?”

“Na mimi ni mama Pilima, nina mtoto anaitwa Pilima.”
“Hakuna kitu kama hicho.”
“Kweli kabisa, mtoto wangu anaitwa Pilima.”
“Kwa hiyo mimi mama Pilima, wewe baba Pilima?”
“Ndiyo maana yake.”

Mama Pilima alisahau yote yaliyopita. Alisahau alivyotendwa na mwanaume huyo! Moyoni alisema…

“Kwa hiyo sasa nina baba Pili, baba Pilima feki na baba Pilima orijino yule wa nyumbani.”
***
Uhusiano kati ya mama Pilima na baba Pilima ulipamba moto na kumsahau baba Pili kwa muda. Aliamua kumsahau baba Pili kwa sababu ya kukwepa kukutana naye kimwili wakati ameshajitolea kwa baba Pilima. Angekuwa mwanamke wa ajabu, wanaume watatu kwa wakati mmoja!

Kwa hiyo ikawa kila baba Pili alipompigia simu wakutane, mama Pilima alitoa sababu ya uongo ili kusogeza siku mbele.

Katika kipindi cha wiki mbili, akawa ameshakutana kimapenzi mara mbili na baba Pilima na alikolea kwelikweli. Wao sasa ndiyo walikuwa wakikaa kila jioni kwenye baa nyingine aliyoijua baba Pilima.

Mazungumzo yao walipokaa, mama Pilima alifurahia sana kumwita mwanaume huyo baba Pilima akijisikia kama anamuita mume wake nyumbani…
“Baba Pilima…”
“Niambie mama Pilima…”

“Hivi mapenzi yetu yatadumu kweli baba Pilima?”
“Kwa nini yasidumu mama Pilima, tatizo liko wapi kwani?”
“Sijaona tatizo, bali kama nilivyokwambia, sijazoea kusaliti na nimeshakusimulia mkasa mzima mpaka nilipokutana na wewe.”

“Mimi siwezi kuachana na wewe mama Pilima, kuwa na amani tu.”
Kuna siku, mama Pilima na baba Pilima wakiwa kwenye baa hiyo, mhudumu alijua ni wapenzi kutokana na mikao, kwani uzoefu wake, wanandoa hawakai kihasarahasara, lakini alikuja kushangaa, kumsikia mama Pilima akimuuliza baba Pilima…

“Eti baba Pilima, kwa nini usinywe pombe kali ukaachana na bia?”
“Mama Pilima, pombe kali zinataka watu wanene sana, mimi umbo langu si unaliona?”
“Mh! Kumbe hawa ni mke na mume? Mbona wako kama mtu na hawara yake?” alijiuliza mhudumu huyo baada ya kuwasikia wakiitana majina ya watoto wao.
***

Siku hiyo, akiwa nyumbani, sebuleni na mume wake, mama Pilima alijisahau katika mazungumzo…

“Baba Pilima…eee! Eti baba Pilima,” alikosea mama Pilima, akashtuka, lakini akaendelea kuita jina hilohilo bila mumewe kujua kwamba, hakumaanishwa yeye.
Usiku wa siku hiyo, wakiwa wamelala, baba Pilima alitaka haki yake, akafurukuta akafanikiwa. Lakini wakati mpambano ukiendelea, mama Pilima aliingiza mazoea yaleyale, alimwita mumewe kimahaba…

“Baba Pilima,” lakini alimaanisha yule feki…
“Niambie mke wangu,” aliitika kibabebabe baba Pilima bila kujua kuwa, hakukusudiwa yeye.
***
Ilikuwa Jumapili, mama Pilima alikuwa akijiandaa kwenda kanisani, simu yake ilikuwa mezani sebuleni. Baba Pilima alikuwa hajaamka. Wifi wa mama Pilima alishajiandaa kwa safari ya kanisani, kwa hiyo alikuwa akimsubiri yeye tu. Mara simu ya mama Pilima iliita, wifi yake akaitupia macho…
“Wifi kaka anapiga simu?” alisema wifi mtu huyo baada ya kuona Baba Pilima kwenye skrini ya simu.

Mama Pilima alikwenda mbio…
“Anapigaje wakati bado nipo humuhumu ndani?” aliuliza mama Pilima, akiamini ni kweli mume wake amepiga…

“Ooo! Kumbe huyu!” alisema mama Pilima, wifi yake akachezwa na machale. Kwamba, kwa nini mama Pilima aseme ‘ooo… kumbe huyu’.
Hata hivyo, mama Pilima hakupokea simu hiyo, akaikata na kutuma meseji…
“Ina maana si kaka aliyepiga?” aliuliza wifi huyo…

“Ngoja nitakwambia,” alisema mama Pilima akiwa na uso uliochunwa kwa kukosa aibu. Alijua nini ni nini!
“Mh!” aliguna wifi mtu huyo, lakini akaachana na maswali zaidi.

Ghafla, baba Pilima akatokea kutoka chumbani akiwa ndani ya nguo za kulalia…
“Mbona kama nasikia mimi nimempigia simu mama Pilima wakati sijashika simu yangu tangu kumekucha. Au sijasikia sawasawa?” alihoji baba Pilima huku akipiga miayo.
Je, unajua nini kilitokea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Ijumaa, siku ya Ijumaa.

Leave A Reply