The House of Favourite Newspapers

Jini Mauti-16

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Hata usiku wa siku hiyo tulipokutana kwenye uwanja wa wachawi, sikuonekana kuwa na furaha, nilionekana kuwa mnyonge sana, bibi alifahamu kila kitu kilichotokea, akaamua kunifuata. Endelea sasa…

“Davina…”
“Abeee.”
“Hongera sana,” alisema bibi.
“Hongera sana,” alinipongeza, kidogo nikashtuka.
“Hongera ya nini?” niliuliza.

Badala ya kujibu swali hilo, bibi akaanza kucheka, kicheko kikubwa kilichoonesha ni jinsi gani alifurahi. Sikujua ni kitu gani kilichomfurahisha, nilibaki nikimshangaa, alichokifanya ni kuondoka mahali hapo.

Baadaye kukaanza kutolewa taarifa kwamba kulikuwa na mtu miongoni mwetu ambaye alifanya kazi nzuri sana ya kumleta mtu mmoja pale uwanjani, mtu ambaye kwa siku hiyo angetumika na kuwa nyama kwa ajili ya wachawi.

Sikujua mtu huyo alikuwa nani, nikabaki nikiangalia tu kila kilichokuwa kikiendelea. Baada ya dakika kadhaa, akaletwa mvulana mmoja mbele yetu, nilipomwangalia, nilihisi kumfahamu ingawa sikuwa na uhakika kwa kuwa mahali pale kulikuwa na mwanga hafifu.

Nilichokifanya ni kusogea mbele ili nimuone vizuri. Sikuamini mara baada ya kufika mbele na kugundua kwamba yule mtu niliyekuwa nikimwangalia alikuwa Thomas.
“Thomas….” niliita huku nikionekana kushtuka.

Thomas hakuongea kitu, alibaki akiniangalia tu, alionekana kama zezeta. Nilimsogelea zaidi na kumshika, nikataka azungumze kitu chochote kile, alikuwa kimya, nilipomfumbua mdomo, ulimi wake ulikuwa umekatwa.

Nililia sana, niliumia sana lakini cha kushangaza wachawi wenzangu walikuwa wakicheka tu. Nilitamani Thomas azungumze kitu chochote kile lakini haikuwa hivyo, alibaki kimya tu kitu kilichonifanya nione kwamba tayari nilimpoteza mtu niliyekuwa nikimpenda sana.

Siku hiyo, hatukufanya kazi zaidi ya kusherehekea tu, nililazimishwa kuwa na furaha lakini ilishindikana kabisa. Sherehe ilipofikia mwisho, Thomas akachukuliwa na kupelekwa katika sehemu moja ambayo huko ndipo walipohifadhiwa misukule na hata watu walioandaliwa kwa ajili ya kuliwa nyama.

Asubuhi ilipofika, nikaamka, nikajiandaa na kwenda shule. Nilionekana kuwa na mawazo mno, njiani nilishindwa kuvumilia, nilikuwa nikibubujikwa na machozi tu, sikuamini kila kitu kilichokuwa kimetokea.

Nilipofika shuleni, kitu cha kwanza kabisa kukutana nacho, wanafunzi wengi walikuwa wakilia, vilio vilitawala kila kona, sikutaka kuuliza kulikuwa na nini, nilifahamu kila kitu nikajua tu kwamba taarifa zilikuwa zimetolewa kwamba Thomas alikuwa amefariki dunia.

Nilishindwa kuvumilia, nililia sana kwa ajili ya Thomas lakini nikashindwa kuyazuia tena machozi yangu mahali hapo, nikaanza kulia, tena kwa maumivu makali mno.
Kwa kuwa wengi walifahamu kwamba nilikuwa kwenye uhusiano na Thomas, wakaanza kunionea huruma, wakanifuata na kuanza kunibembeleza ninyamaze kitu kilichonifanya nilie zaidi.

Walimu wakatutangazia kwamba tulitakiwa kwenda msibani hivyo maandalizi yalitakiwa kufanyika. Baada ya dakika kadhaa tayari kila kitu kilikuwa tayari na hivyo kuanza kuelekea huko.

Tulipofika tukaanza kusikia sauti ya vilio mahali hapo, watu wengi walikuwa wakilia hali iliyoonesha kwamba Thomas alikuwa mtu aliyependwa mno, tukakaa katika sehemu maalum ambayo ilitengwa kwa ajili ya wanafunzi na walimu, tukakaa hapo huku tukiendelea kulia kama kawaida.

Msibani hapo hakukuwa na watu wa kawaida tu, nilipopiga macho huku na kule, nikafanikiwa kuwaona wachawi wengine nao wakiwa mahali hapo kuhakikisha amani inatawala. Katika hili ngoja nikwambie kitu kimoja, mara nyingi kunapokuwa na msiba wa mtu aliyechukuliwa msukule huwa wachawi waliohusika ambao walimchukua marehemu ni lazima wawepo hapo ili kuhakikisha kwamba kila kitu kinakuwa sawa.

Watu wanaposogea kule kulipokuwa na jeneza, kila mmoja alikuwa akimwagiwa unga usoni ili wale waliokuwa na nguvu ya kugundua kwamba yule aliyezikwa hakuwa mtu bali gogo au nyoka mkubwa, waweze kuuona mwili wa marehemu.
Je, kiliendelea nini? Usikose wiki ijayo.

Leave A Reply