The House of Favourite Newspapers

Babu Miaka 85 Afungiwa Katika Ofisi ya Serikali Siku 3 Bila Kula

0

MZEE wa miaka 85, Masanja Mahubi, anadaiwa kufungiwa kwa siku tatu katika ofisi ya serikali ya mtaa bila kupewa chakula na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Msoba Mligo.

 

Akizungumza kwa shida baada ya Jeshi la Polisi likiongozwa na Mkuu wa Jeshi hilo wilayani Igunga, Ally Mkalipa, kuuvunja mlango wa ofisi hiyo na kumtoa nje, Mahundi alisema alikuwa amechoka sana kutokana na kutokula chakula kwa muda wa siku tatu.

 

Alidai kuwa Februari 18 alikuwa ametoka Kijiji cha Iyogelo, Kata ya Kining’inila, alikokuwa amefuata ng’ombe wake waliokuwa kwa ndugu yake na alipofika mtaa wa Mwamaganga maeneo ya Mwanzugi, saa tatu usiku aliamua kulala.

 

Alisema katika harakati za kutafuta nyumba ya kulala alikutana na mwenyekiti huyo akiwa na vijana watatu ambao walimuhoji alikotokea na anakokwenda.

 

Mahundi alisema, licha ya kuwajibu walimchukua na kumfikisha ofisi ya serikali ya mtaa wa Mwamaganga, ambako alifungiwa ndani ya ofisi hiyo.

 

Alidai kuwa Februari 19, saa nne asubuhi akiwa amefungiwa kwenye ofisi hiyo alipewa kikombe cha chai na chapati mbili na alipomwomba mwenyekiti huyo amwachie, alimpa masharti kuwa kama anataka kutolewa nje atoe kitu kidogo.

 

Anaeleza kuwa Februari 20, saa nne asubuhi akiwa mahabusu ya ofisi hiyo, alisikia sauti za wananchi waliokuwa wanamtaka mwenyekiti huyo amfungulie kwa kuwa ilikuwa siku tatu akiwa mahabusu. Mahundi alidai mlango wa ofisi hiyo ulivunjwa na polisi na yeye kutolewa nje.

Leave A Reply