The House of Favourite Newspapers

Bahati Nasibu Shinda Nyumba Majaba Kukabidhiwa Mjengo Wake Wiki Ijayo

0
George Majaba akiwa na familia yake.

BAADA ya shughuli kubwa ya muda wa zaidi ya miezi sita ya Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili ambayo ilifikia tamati Septemba 27 mwaka huu kwa droo kubwa na George Majaba kuibuka kuwa mshindi, sasa imebaki wiki moja tu kwa Majaba kukabidhiwa mjengo wake, siku ya Jumanne ijayo.

Majaba, ambaye ni kondakta wa mabasi ya abiria yanayofanya safari zake kati ya Dodoma na Dodoma vijijini, atakabidhiwa nyumba hiyo ya kisasa, yenye vyumba vitatu, kikiwemo cha Master Bed Room, sebule, jiko, choo, bafu na sehemu ya kulia chakula, ambayo pia imeunganishwa kabisa na nishati ya umeme.

Majaba anatarajiwa kukabidhiwa nyumba hiyo katika hafla fupi itakayofanyika Oktoba 31 mwaka huu, itakayoanzia katika Ofisi za Global Publishers zilizopo Sinza Mori na baadaye katika eneo la tukio huko Bunju.

“Tunataka kufanya kitu kidogo tofauti na cha kumtia faraja mshindi wetu, kwa maana hiyo tumeandaa mapokezi maalum ikiwemo pikipiki na magari ambayo yatampokea Ubungo Terminal na kuja naye hadi ofisini kwetu, (Sinza Mori, zamani Johannesburg Hotel).

 “Pale kutakuwa na utambulisho rasmi wa mshindi wetu ikiwa ni pamoja na kufanya mahojiano na vyombo vya habari na kisha tutaanza safari ya kuelekea nyumbani kwake kwa ajili ya kumkabidhi nyumba yake,” alisema Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho.

“Tumeamua kumpa nyumba ikiwa kamili kabisa, atakachofanya yeye ni kuja na begi lake na kuanza maisha, hiyo yote ni kuonyesha jinsi gani Global Publishers imedhamiria kubadili maisha ya wasomaji wake.

Pamoja na thamani kubwa ya nyumba, lakini tumeona tumuongezee na nishati ya umeme ambayo ni muhimu ili kumpunguzia jukumu la kuhangaika kuingiza umeme,” alisema Mrisho.

Hii ni mara ya pili kwa Global Publishers, kampuni pekee ya uchapaji magazeti katika historia, kuwahi kutoa zawadi ya nyumba kwa wasomaji wake.

Kabla ya kupatikana kwa mshindi wa awamu hii ya pili, bahati nasibu hiyo ilifanya droo ndogo tano katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, ambako wasomaji zaidi ya 30 walijipatia zawadi kemkem, zikiwemo pikipiki, ving’amuzi, televisheni ‘flat screen,’ simu za kisasa za mikononi, kofia na fulana.

STORI: Na Mwandishi Wetu, Dar.

Usipitwe na Matukio, Install App Yako ya Kijanja na Namba Moja Tanzania ya Global Publishers

Android Bofya ===> Google Play

iOS Bofya ===>Apple Store

Leave A Reply