The House of Favourite Newspapers

Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Majaba Kuingia Dar Leo

0

KIBABE! MSHINDI wa Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili, George Majaba leo anatarajiwa kuingia jijini Dar es Salaam kibabe kwa mapokezi makubwa kabla ya kukabidhiwa mjengo wake uliojengwa Bunju B nje kidogo ya jiji.

Kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho ambao ndiyo waendeshaji wa bahati nasibu hiyo, Majaba, ambaye ni kondakta wa mabasi ya abiria yanayofanya safari zake kati ya Dodoma Mjini na Dodoma Vijijini, anatarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam leo mapema.

Baada ya kuwasili Ubungo Terminal, Majaba atakwenda katika ofisi za Global Group, zilizopo Sinza Mori zinazotazamana na Wanyama Hotel, ambako atasalimiana na wafanyakazi wa Global Publishers na kufanya mahojiano mafupi na vyombo vya habari, kabla ya kupelekwa Bunju B, ilipo nyumba yake kwa ajili ya zoezi la kukabidhiwa.

“Tunataka kufanya kitu kidogo tofauti na cha kumtia faraja mshindi wetu, kwa maana hiyo tumeandaa mapokezi maalum, tumeandaa pikipiki na magari ambayo yatampokea Ubungo Terminal na kuja naye hadi ofisini kwetu (Sinza Mori, zamani Johannesburg Hotel).

“Pale kutakuwa na utambulisho rasmi wa mshindi wetu ikiwa ni pamoja na kufanya mahojiano na vyombo vya habari kisha tutaanza safari ya kuelekea nyumbani kwake kwa ajili ya kumkabidhi nyumba yake,” alisema.

“Tumeamua kumpa nyumba ikiwa kamili kabisa, atakachofanya yeye ni kuja na begi lake na kuanza maisha, hiyo yote ni kuonyesha jinsi gani Global Publishers imedhamiria kubadili maisha ya wasomaji wake, pamoja na thamani kubwa ya nyumba, lakini tumeona tumuongezee na nishati hii muhimu ili kumpunguzia jukumu la kuhangaika kuingiza umeme,” alisema Mrisho.

Hii ni mara ya pili kwa Global Publishers, kampuni pekee ya uchapaji magazeti katika historia, kuwahi kutoa zawadi ya nyumba kwa wasomaji wake.

Kabla ya kupatikana kwa mshindi wa awamu hii ya pili, bahati nasibu hiyo ilifanya droo ndogo tano katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, ambako wasomaji zaidi ya 30 walijipatia zawadi kemkem, zikiwemo pikipiki, ving’amuzi, televisheni ‘flat screen,’ simu za kisasa za mikononi, kofia na fulana.

Katika Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Kwanza, mshindi wake alikuwa ni mwanamke Nelly Mwangosi, mjasiriamali mwenyeji wa Iringa, ambaye nyumba yake ipo Salasala, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Nyumba hiyo ya kisasa, ina vyumba vitatu, kikiwemo cha Master Bed Room, sebule, jiko, choo, bafu na sehemu ya kulia chakula, ambayo pia imeunganishwa kabisa na nishati ya umeme.

Zitto: Nimeachiwa Huru, Naisubiri Serikali Mahakamani – Video

Leave A Reply