The House of Favourite Newspapers

Bao 3 za Simba zaitisha Stand

SAHAU kabisa kimataifa. Habari ya kwamba Simba aliwapiga Al Ahly iliyokamilika bao 1-0 ndani ya Uwanja wa Taifa, jifanye huijui kabisa. Ishu ni kwamba Stand United atakula tena tatu leo Jumapili pale Shinyanga?Takwimu haziongopi.

 

Simba katika mechi zake tano mfululizo za viporo ametupia mabao ya kutosha watu kibao wamekula tatu. Imekuwa kama fasheni.

Mwadui amekula tatu moja, Yanga akakaza akapigwa moja,African Lyon akapigwa tatu zingine, Azam na kikosi chake chote naye akaambulia tatu moja. Iringa yote ikajazana kwenye Uwanja wa Samora kuwashangilia Lipuli wakapigwa nao tatu moja.

 

Kocha wa Simba,Patrick Aussems ambaye leo hatamtumia Emmanuel Okwi kutokana na majeruhi amesisitiza kwamba ushindi kwa mchezo huo ni muhimu kuwaweka vizuri kisaikolojia kwa mchezo wa kimataifa wikiendi ijayo. Simba itarudiana na JS Saoura ya Algeria ugenini kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika Jumamosi ijayo saa nne usiku na itaondoka Dar es Salaam Jumanne
keshokutwa.

Msisitizo wa Kocha wa Stand United Amars Niyongabo ni kwamba watacheza mpira wao bila kujali wanakutana na timu gani na iliyo na mlolongo wa matokeo ya namna gani.

Ameongeza kwamba wanataka pointi muhimu kwenye uwanja wao ili kusogea kwenye msimamo wa Ligi kwani kukaa chini ya nafasi ya kumi ni hatari.

Mbali na mechi hiyo ya Simba,Singida itakuwa nyumbani kucheza na Prisons, Mbeya City itaikaribisha Ndanda huku Kagera wakicheza na Lipuli Bukoba.

 

Mtibwa ambao wameonekana kuyumba katika siku za hivikaribuni, watakuwa Manungu kucheza na Mbao ambayo ilitibua rekodi zake kwa kukubali kipigo dhidi ya Yanga hivi karibuni jijini Mwanza.

Comments are closed.